
Katika taarifa hiyo, Mtatiro amesema kuwa baada ya tukio hilo, alifika eneo la ajali mara moja akiwa na timu za uokozi, na kwa kushirikiana na wananchi, waliendesha zoezi la uokoaji kwa kutumia mashine za kisasa za migodini.
Mashine zaidi ya 10 zilikuwepo, lakini ni mashine 4 pekee zilizohitajika kukamilisha kazi hiyo.
"Tumefanikiwa kuwaokoa watu 11 wakiwa hai, na watu 6 tumewatoa wakiwa wamefariki. Ukiwa pale eneo la ajali utaona tulihamisha kifusi chote kilichowaangukia watu na kukichambua kwa mashine na mikono, hakukuwa na mtu mwingine yeyote aliyebakia ndani ya kifusi," amesema Mtatiro.
Ameeleza kuwa eneo la ajali ni wazi na pana kiasi kwamba hata mashine 20 za kuchimba zinaweza kuingia kwa wakati mmoja, hivyo wananchi walishuhudia moja kwa moja hatua zote za uokoaji.
Aidha, Mtatiro amesema hakuna mtu yeyote anayekosekana katika eneo la Mwakitolyo na Shinyanga, na familia zote zimethibitisha kuwa watu waliokosekana ghafla ni wale waliopatikana—yaani, 6 waliofariki na 11 wanaoendelea na matibabu.
"Ukiwa pale eneo la ajali utaona tulihamisha kifusi chote kilichowaangukia watu na kukichambua kwa mashine na mikono, hakukuwa na mtu mwingine yeyote aliyebakia ndani ya kifusi, na zoezi la uokoaji lilifanyika wananchi wote wakiwa wanaangalia kwa sababu lile ni eneo la wazi na ni eneo pana ambalo zinaweza kuingia excavators hata 20 kwa wakati mmoja, siyo kwamba ni eneo finyu lisilo na nafasi.
Pia, na bahati nzuri, eneo la Mwakitolyo na Shinyanga halina mtu yeyote ambaye labda anakosekana "missing person", majirani, ndugu, jamaa, marafiki, wapangaji, wenye nyumba na familia zote za Mwakitolyo na Shinyanga, zinakiri kuwa watu waliokosekana ghafla walikuwa wale 6 waliofariki na wale 11 wanaotibiwa",ameeleza.
"Kwa hiyo siyo tu kwamba tumekamilisha uokoaji huu kwa uzito wa kipekee, lakini pia tumeongoza kufuatilia ikiwa kuna mtu hapatikani, watu wote wa eneo la ajali wameridhishwa kuwa hakuna mwenzao aliyebakia kwenye kifusi",ameongeza Mkuu huyo wa wilaya.
Mtatiro amesema kuwa majeruhi walioko hospitalini walithibitisha kuwa wakati ajali inatokea, walikuwa watu takribani 17 mgodini na walikuwa wanajuana.
Aidha, mashine zilifanikiwa kuhamisha kifusi chote, na watu wote walipatikana kutoka humo.
"Kifusi chote kilitolewa eneo la ajali na kuhamishiwa upande mwingine kabisa na ndipo tukapata hao watu 17 kwa mchanganuo huo. Kama hiyo haitoshi, hata majeruhi walioko hospitalini walitueleza waziwazi siku ya ajali kuwa wakati ajali inatokea mgodini kulikuwa na watu takribani 17 ,wanajuana",amefafanua.
Amesisitiza kuwa taarifa zinazodai kuwepo kwa watu waliobaki chini ya kifusi si sahihi na zinapaswa kupuuzwa.
"Naomba tupuuze taarifa zozote zinazoeleza eti kuna watu, wenzetu, wameachwa chini ya kifusi. Taarifa hizo siyo sahihi, ni potofu, zinalenga kuzua taharuki na zenye malengo yasiyo sahihi - tuzipuuze", amesema Wakili Mtatiro.
By Mpekuzi
Post a Comment