MAVUNDE AZUNGUMZIA TUKIO LA MAITI KWENYE PIKIPIKI LILIVYOMGEUZA KUWA MTUMISHI WA WATU |Shamteeblog.




Na Dotto Kwilasa, Dodoma

Akiwa njiani kutekeleza majukumu yake kama Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini, Anthony Mavunde alikutana na jambo lililobadili kabisa mtazamo wake kuhusu uongozi  mtu mmoja aliyekuwa akibeba maiti ya mpendwa wake juu ya pikipiki, akisaka msaada wa kuisafirisha kwa heshima ya mwisho.

Tukio hilo lilimgusa kwa undani na kuacha alama ya kudumu moyoni mwake. Akieleza kwa sauti ya huzuni na huruma mbele ya hadhira iliyojitokeza kwenye hafla ya uzinduzi wa mfumo wa kidigitali wa kupokea kero za wananchi, Mavunde alisema:

“Moyo wangu uliniuma sana. Nikajiuliza, mimi ni mbunge, nitawezaje kulikalia kimya jambo kama hili? Nikasema hapana,badala ya kuchangia shilingi laki tatu kila siku kwenye misiba, ni bora ninunue gari la kusaidia watu wangu kusafirisha miili ya wapendwa wao.”

Uamuzi huo ulimuweka katikati ya mvutano wa mitazamo. 

Alitukanwa, alipingwa, lakini hakutikisika. Alisimama kidete kama kiongozi wa vitendo na siyo wa hotuba, na leo anasema bila hofu kuwa maumivu hayo ndiyo yaliyomfanya avae rasmi vazi la “utumishi wa watu”.

“Niliamua kuishi utumishi, siyo uongozi. Kuna tofauti kubwa kati ya kiongozi na mtumishi. Mimi ni mtumishi wa watu – niliamua kuitikia kilio cha jamii yangu,” amesisitiza.

Katika kuendeleza azma yake ya kuhudumia watu, Mavunde leo amezindua rasmi mfumo wa kidigitali wa kusikiliza na kushughulikia kero za wananchi wa Dodoma Mjini mfumo wa kwanza wa aina yake nchini.

Wakati huo huo, amegawa simu janja kwa wenyeviti wa mitaa 222 wa jimbo hilo, kwa lengo la kurahisisha mawasiliano baina ya viongozi na wananchi.

“Kupitia mfumo huu, hata kama kiongozi mmoja hapokei simu, taarifa ya mwananchi itafika kwa wengine wote kwa wakati mmoja. Hii ndiyo teknolojia tunayopaswa kutumia kwa maendeleo ya watu wetu,” alieleza kwa msisitizo.

Mavunde amesema mfumo huo utaendelea kutumika hata baada ya yeye kuondoka madarakani, na tayari maandalizi yamefanyika kuhakikisha mbunge ajaye anaelekezwa na kuendeleza huduma hiyo muhimu kwa wananchi wa kata zote 41 za Dodoma Mjini.

“Naondoka bila deni. Huu ni mwisho wa safari yangu kama Mbunge wa Dodoma Mjini, lakini mwanzo wa zama mpya za utumishi kwa teknolojia. Nawashukuru kwa kuniamini kwa miaka kumi,” amesema kwa hisia.

Aidha, Mavunde ametangaza kuchangia shilingi milioni 10 kwa ajili ya kuanzisha SACCOs ya wenyeviti wa mitaa  hatua itakayowawezesha kiuchumi na kuwaongezea uwezo wa kuwahudumia wananchi kwa ufanisi zaidi.

Amesisitiza kuwa simu walizopewa si za anasa, bali ni nyenzo muhimu za kutatua matatizo ya wananchi. Simu hizo zimetengenezwa nchini kwenye kiwanda cha Mkuranga, ikiwa ni hatua ya kuunga mkono ajira na uzalishaji wa ndani.

“Tutatenganishwa na mipaka ya kijiografia tu, lakini roho yangu itaendelea kuwa nanyi. Nawashukuru kwa safari hii ya kipekee, nitaendelea kuwa mtumishi wa watu hata nje ya ubunge,” alihitimisha huku akipigiwa makofi ya heshima.







By Mpekuzi

Post a Comment

Previous Post Next Post