MKURUGENZI MTENDAJI TANESCO JACOB TWANGE AMTAKA MKANDARASI UJENZI WA UMEME JUA KISHAPU KUKAMILISHA KWA WAKATI |Shamteeblog.


Na mwandishi wetu - Malunde 1 blog

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Lazaro Jacob Twange, ametoa maagizo kwa mkandarasi wa mradi wa umeme wa jua unaotekelezwa katika kijiji cha Ngunga, kata ya Talaga, wilayani Kishapu, kuhakikisha anakamilisha kazi hiyo kwa mujibu wa makubaliano ya mkataba.

Twange ametoa kauli hiyo leo Jumapili, Juni 8, 2025, wakati wa ziara ya ukaguzi wa maendeleo ya mradi huo mkubwa wa nishati jadidifu unaolenga kuongeza upatikanaji wa umeme safi na wa uhakika katika mkoa wa Shinyanga na maeneo ya jirani.

“Tunamtaka mkandarasi kutekeleza wajibu wake na sisi tutatekeleza wajibu wetu kwa sababu sisi ndio tumemuajili na hatudai bali tunamdai”  amesema Twange.

Akizungumza katika ziara hiyo, Mkandarasi wa mradi huo, Daniel Xu kutoka kampuni ya Sinohydro, ameeleza kuwa mwaka 2024 utekelezaji wa mradi ulikumbwa na mvua nyingi ambazo ziliathiri shughuli za kiutendaji kutokana na maji mengi kujaa kwenye eneo la ujenzi.

“Tunatambua kuchelewa kumaliza mradi huu, lakini kulikuwa na changamoto nyingi nje ya uwezo wetu, zilizopelekea kushindwa kumaliza kwa wakati, tumepewa muda wa nyongeza na tunaahidi kutekeleza maagizo ya serikali kuhakikisha mradi unamalizika kwa wakati kwa muda tuliongezewa” amesema Xu.

Naye Meneja wa mradi wa umeme jua Emmanuel Anderson katika taarifa yake ameeleza kuwa mradi huo unaogharimu kiasi cha Bilioni 323 ulianza Desemba 2023 na ulitakiwa kumalizika mwezi Februari, 2025 lakini kwa sababu zilizo nje ya uwezo mkandarasi aliomba kuongezewa muda na kupewa hadi Oktoba, 2025.

“Kwa sasa mradi huu wa awamu ya kwanza umefikia asilimia 63, ambao ulitarajiwa kumalizika Februari, 2025 lakini kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo kama upungufu wa vifaa kwa ajili ya kupasua miamba na kusimika sola umepelekea kuchelewa kukamilika kwa mradi huu, katika mradi usanifu ni asilimia 92.7, manunuzi 78.3 na ujenzi 54.9”, amesema Anderson.

“Mradi huu umegharimu kiasi cha Sh. bilioni 118 kwa awamu ya kwanza ambapo sola paneli hizi ni sawa na megawati 50 kwenye eneo la hekta 64” amesema Anderson.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Lazaro Jacob Twange akizungumza wakati wa ziara hiyo kwenye mradi wa umeme jua Kishapu - Shinyanga.
Mkandarasi wa mradi huo, Daniel Xu kutoka kampuni ya Sinohydro akizungumza wakati wa ziara hiyo.
Meneja wa mradi wa umeme jua Emmanuel Anderson akizungumza wakati wa ziara hiyo.
Mradi wa umeme jua Kishapu - Shinyanga.
Mradi wa umeme jua Kishapu - Shinyanga.
Mradi wa umeme jua Kishapu - Shinyanga.
Mradi wa umeme jua Kishapu - Shinyanga.

Picha na Mpiga picha wa Malunde 1 blog


By Mpekuzi

Post a Comment

Previous Post Next Post