SERIKALI YAOKOA TRILIONI 4.9 KATIKA SAKATA LA IPTL |Shamteeblog.






Na Woinde Shizza, Arusha

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeandika historia mpya baada ya kufanikiwa kuokoa kiasi kikubwa cha fedha za umma Shilingi Trilioni 4.9 katika sakata lililohusisha Kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL).

Hatua hiyo imetokana na juhudi za Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupitia mkataba wa maridhiano pamoja na amri ya Mahakama, ambazo zimepelekea serikali kulipa kiasi cha Shilingi Bilioni 8.5 tu, badala ya kulipa mabilioni ya fidia yaliyokuwa yakidaiwa awali.

Akizungumza leo jijini Arusha wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku tatu kwa Mawakili wa Serikali, Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Ally Possi, amesema hatua hiyo ni ushindi mkubwa kwa taifa na ushahidi kuwa serikali imejipanga kulinda rasilimali za wananchi.

Katika mafanikio mengine, Dkt. Possi amesema kuwa kati ya Julai 2024 hadi Aprili 2025, serikali imeshinda jumla ya mashauri 750 kati ya mashauri yote yaliyomalizika, sawa na asilimia 77.6. Kupitia ushindi huo, serikali imefanikiwa kuokoa Shilingi Bilioni 51.02.

Aidha, kwenye mashauri ya usuluhishi, jumla ya mashauri 209 yameendeshwa, ambapo 180 ni ya kitaifa na 29 ni ya kimataifa. Kati ya mashauri 21 yaliyohitimishwa, 16 yameshinda na kuokoa Shilingi Bilioni 16.9 (sawa na Dola za Kimarekani Milioni 63.3).

Mafunzo hayo, yanayofanyika jijini Arusha, yanalenga kuwawezesha Mawakili wa Serikali kuongeza ufanisi katika kushughulikia mashauri mbalimbali yanayogusa uchumi, jamii na teknolojia. Wakufunzi wa mafunzo hayo ni pamoja na Majaji wa Mahakama ya Rufani, Mahakama Kuu, Majaji wastaafu na wataalamu wa sheria kutoka ndani na nje ya nchi.

Kwa upande wake, Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro, ametoa wito kwa Mawakili wa Serikali kuendelea kuwaelimisha wananchi na wanasiasa juu ya umuhimu wa kufuata sheria wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
“Sheria hazichukui likizo wakati wa uchaguzi ni wajibu wetu kuhakikisha wanasiasa na wananchi kwa ujumla wanaielewa na kuzingatia sheria wakati wote,” amesema Dkt. Ndumbaro.

Mafunzo hayo yanatarajiwa kuongeza ufanisi wa kazi kwa Mawakili wa Serikali na kuongeza uwezo wa taifa katika kushinda mashauri yenye maslahi ya kiuchumi na kijamii kwa Watanzania.


By Mpekuzi

Post a Comment

Previous Post Next Post