Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame MbarawaNa Sheila Ahmadi – Dar es Salaam
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuzindua rasmi Bandari Kavu ya Kwala, mkoani Pwani, tarehe 31 Julai 2025.
Uzinduzi huo utahusisha pia upokeaji wa mabehewa ya mizigo, pamoja na safari za treni za mizigo ya SGR kati ya Dar es Salaam na Dodoma. Hii ni hatua muhimu katika kuboresha usafirishaji wa mizigo nchini na kuongeza ufanisi wa shughuli za bandari.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, amesema kuwa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta ya bandari, inaendelea kuboresha miundombinu kwa wakati ili kuchochea ukuaji wa uchumi na biashara nchini, hasa katika maeneo ya Dar es Salaam na Pwani.
“Bandari Kavu ya Kwala itasaidia kupunguza msongamano mkubwa wa magari katika barabara ya Mandela, sambamba na kuongeza ajira kwa wakazi wa maeneo ya jirani,” amesema Prof. Mbarawa.
Ameongeza kuwa serikali inatarajia pia ongezeko la viwanda katika eneo hilo, hali itakayoongeza mapato ya serikali kwa kiwango kikubwa.
Aidha, Prof. Mbarawa amefafanua kuwa serikali haijaitelekeza reli ya zamani ya MGR, ambapo katika hafla hiyo ya uzinduzi, Rais Dkt. Samia atapokea mabehewa mapya 50 kati ya 100 yaliyonunuliwa na Shirika la Reli Tanzania (TRC). Vilevile, mabehewa 20 ya MGR yamefanyiwa ukarabati na Wakala wa Uwezeshaji wa Ushoroba wa Kati.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, usafirishaji wa mizigo kati ya Dar es Salaam na Dodoma ulianza rasmi Juni 27, 2025 ambapo makontena 10 yenye jumla ya tani 700 za bidhaa mchanganyiko kutoka Kampuni ya Azania yalisafirishwa.
Julai 9, makontena 20 yenye tani 1,400 za saruji kutoka Kampuni ya Dangote nayo yalisafirishwa. TRC inatarajia kuongeza treni yenye mabehewa 30 ili kubeba mizigo ya tani 210,000 hadi kufikia uwezo wa juu uliosanifiwa.
Bandari hiyo ya Kwala inatarajiwa kuhudumia makasha 823 kwa siku, sawa na makasha 300,395 kwa mwaka, ambayo ni asilimia 30 ya makasha yote yanayohudumiwa kwa sasa na Bandari ya Dar es Salaam. Pia, bandari hiyo itakuwa kituo muhimu cha kusafirisha shehena ya makasha kwenda nchi jirani.
“Tunatoa wito kwa wadau wote wa usafirishaji, wafanyabiashara na wawekezaji kuchangamkia fursa ya gharama nafuu na usafiri wa uhakika kupitia Bandari Kavu ya Kwala,” amesema Prof. Mbarawa.

By Mpekuzi
Post a Comment