DC ARUMERU ATOA WITO KWA WAKULIMA KUACHANA NA KILIMO CHA MAZOEA |Shamteeblog.


Bwana shamba kutoka kampuni ya Bayer crop Mussa Bakari akitoa elimu kwa wakulima kutoka kata ya Sambasha wilayani Arumeru mkoani Arusha walioudhuria Katika Maadhimisho ya siku ya kilimo biashara katika viwanja vya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI Selini)na kujionea teknolojia mbalimbali za kilimo.


Na Woinde Shizza , Arusha

Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Mwinyi Ahmed Mwinyi, amesema kuwa wakati umefika kwa Watanzania kuachana na kilimo cha mazoea na kukumbatia teknolojia, maarifa ya kitaalamu, na tafiti za kisasa ili kukuza tija, kipato na usalama wa chakula nchini.


Akizungumza wakati akifungua rasmi Maadhimisho ya siku ya kilimo biashara katika viwanja vya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) mkoani Arusha, mkuu wa wilaya ya Arumeru aliwapongeza TARI kwa kuandaa kwa mafanikio hafla hiyo muhimu inayowakutanisha wakulima, watafiti, wanafunzi, sekta binafsi na wadau wengine muhimu wa kilimo.


“Niwapongeze TARI kwa maonyesho haya ya kitaifa yanayolenga kuelimisha jamii kwamba kilimo si kazi ya mazoea tena, bali ni biashara yenye tija, ajira na msingi wa maendeleo ya viwanda na Taifa letu kwa ujumla,” alisema.


Alisema mwaka huu ni mara ya 14 tangu kuanzishwa kwa maadhimisho haya mwaka 2012, na kwamba yamekuwa jukwaa la mafunzo na ubunifu kwa wadau wa sekta ya kilimo.

Aidha alisisitiza kuwa ushiriki wa wanafunzi katika maonyesho hayo ni hatua muhimu ya kuandaa kizazi kipya cha wakulima na watafiti wa baadaye.

“Kwa kuwashirikisha wanafunzi, tunawapa dira mapema ya kwamba kilimo ni ajira na chanzo halali cha kipato, hii itawasaidia kuiona sekta hii kwa macho mapya,” alieleza.

Katika kumaliza hotuba yake, Mkuu huyo wa Wilaya alitoa ahadi ya kuendelea kushirikiana na TARI, wakulima na sekta binafsi, akieleza kuwa ushirikiano huo ndio utakaosaidia kufanikisha ajenda ya kuongeza tija, kipato na ajira kupitia sekta ya kilimo.


Kwa upande wake, Mkurugenzi mkuu wa TARI Dkt Thomas Bwana, akizungumza kwenye maonyesho hayo, aliweka bayana mwelekeo wa ajenda ya taifa ya Kilimo Biashara 2010–2030, akiweka msisitizo kuwa mafanikio ya kilimo yatawezekana tu endapo jamii itahamasika kutumia mbegu bora, teknolojia sahihi, pamoja na kufuata kanuni za kisasa za kilimo.

Aidha, aliainisha juhudi zinazofanywa na taasisi hiyo katika kuzalisha mbegu bora zinazostahimili mabadiliko ya tabianchi, akitoa wito kwa wakulima kushirikiana na watafiti kuhakikisha tafiti hizo zinawafikia walengwa.

“Hatuwezi kuwa na kilimo biashara kama hatutalinda ardhi ya tafiti, kuwekeza kwenye maarifa, na kuhakikisha teknolojia zetu zinatumiwa na wananchi,” alisema.

Aidha alieleza pia kuwa serikali imeendelea kutoa kipaumbele kwa sekta ya kilimo kwa kuongezeka kwa bajeti ya wizara hiyo kutoka Shilingi bilioni 294 mwaka 2021 hadi kufikia zaidi ya trilioni 1.24 kwa mwaka wa fedha 2024/25.

Kwa upande wake mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, ambaye ni kaimu mkurugenzi wa utafiti na mafunzo Godfrey Edward alisisitiza kwamba ajenda ya Kilimo biashara sio ya serikali pekee bali ni ya kila mdau, kuanzia wakulima wa vijijini hadi viwanda vikubwa vya kuchakata mazao.


“Teknolojia za kilimo zisibaki kwenye makabrasha ,ni lazima ziifikie jamii siku kama hizi ni jukwaa sahihi la kufanikisha hilo,” alisema Katibu Mkuu huyo kupitia ujumbe wake uliosomwa kwa niaba yake.


Aidha, aliwataka wananchi wa mkoa wa Arusha na hasa wa Wilaya ya Arumeru waliombwa kulinda kwa wivu mkubwa maeneo ya utafiti wa kilimo ya TARI ili kuwezesha kazi za kisayansi kufanyika kwa uhuru na ubora, kwa masilahi ya vizazi vya sasa na vijavyo.

“Miundombinu hii ya utafiti ni hazina ya taifa Tunapozungumzia benki ya ardhi kwa tafiti za mbegu, tunamaanisha usalama wa chakula kwa vizazi vijavyo,” alisisitiza.

Maonyesho hayo yalishirikisha wadau kutoka taasisi mbalimbali ikiwemo Silcom, Meru Agro, Suba Agro, Bora Seed, NFRA, Kibo Seed, pamoja na vikundi vya wakulima, taasisi za pembejeo, na mashamba darasa yaliyoweka wazi teknolojia bunifu za umwagiliaji na uzalishaji wa mazao bora.



By Mpekuzi

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post