Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mjumbe wa Kamati ya Siasa CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Mhandisi James Jumbe, aliyekuwa akiwania kupitishwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kugombea ubunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini, ameishukuru CCM kwa kumpa nafasi ya kushiriki katika mchakato wa awali wa kura za maoni ndani ya chama.
Kupitia taarifa yake kwa umma, Jumbe amesema kuwa ingawa jina lake halijarudi katika orodha ya waliopitishwa, mchakato huo umempa uzoefu mkubwa kisiasa na umemjenga zaidi katika uelewa wa chama.
“Nashukuru chama changu kwa kunipa nafasi ya kushiriki mchakato huu bila vikwazo vyovyote. Nimejifunza mengi na nimepata fursa ya kuimarika zaidi kisiasa. Nipo tayari kuendelea kuwa mwanachama mwaminifu na kupigania ushindi wa chama chetu katika uchaguzi mkuu,” amesema Jumbe.
Ameongeza kuwa ataendelea kushirikiana na wagombea waliopitishwa na kutoa ushirikiano wote unaohitajika kuhakikisha CCM inabaki imara.
“Uongozi ni wa wakati, na naamini chama chetu kimetoa nafasi kwa watu sahihi,” amesisitiza.
Kwa sasa, Jumbe amewataka wanachama na wafuasi wake kuungana na chama katika kuhakikisha ushindi wa CCM unaendelea kushamiri Shinyanga Mjini na taifa kwa ujumla.
Katika hatua nyingine, Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa imempitisha Naibu Waziri wa Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi, kugombea tena ubunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini. Katambi sasa atachuana na wagombea wengine waliopitishwa, akiwemo mwanasiasa mkongwe Stephen Masele, aliyewahi kulitumikia jimbo hilo kwa miaka 10 (2010–2020) na kushika nafasi ya Makamu wa Rais wa Bunge la Afrika na Naibu Waziri wa Nishati na Madini.
Aidha, mchakato huu unaelezwa kuwa unatarajiwa kuwa na ushindani wa hali ya juu, kwani Katambi na Masele wanatajwa kuwa na ushawishi mkubwa kisiasa. Imeelezwa kwamba iwapo jina la Jumbe, ambaye pia alikuwa akipewa nafasi kubwa kutokana na nguvu alizojijengea kwa wananchi, lingerejea, Shinyanga Mjini ingeshuhudia mapambano makali ya kisiasa kati ya vigogo hao watatu.
Wengine waliopitishwa ni Abubakar Gulamhafiz Mukadam, aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, pamoja na Eustard Athanace Ngatale, Hassan Athuman Fatiu, Hosea Muza Karume na Paul Joseph Blandy, ambao kwa pamoja wanatajwa kuongeza mvuto na msisimko wa kisiasa katika kinyang’anyiro hicho.
Mchakato wa kumpata mgombea atakayepeperusha bendera ya CCM katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 unaendelea.
By Mpekuzi


Post a Comment