Kongamano la wanawake wa Kiislamu wakiwa katika kituo cha watoto yatima cha Luhila kwa Mangoma Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma wakiburudika kwa pamoja Na Regina Ndumbaro Songea-Ruvuma
Kongamano maalum la wanawake wa Kiislamu kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara na Zanzibar limefanyika katika kituo cha watoto yatima cha Luhila kwa Mangoma, Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, likiwa na lengo la kusaidia watoto yatima, wanaoishi katika mazingira magumu pamoja na wajane.
Kongamano hilo limeandaliwa kwa ushirikiano wa taasisi mbalimbali na kikundi cha Umoja wa Wanyonge kinachosaidia jamii kwa moyo wa kujitolea.
Akizungumza katika kongamano hilo, Bi Aziza Issa, mwanzilishi wa kituo cha watoto yatima cha Luhila, amesema kuwa kituo hicho kinahudumia watoto 59 na kwa sasa kinakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa nyumba ya mwalimu na fensi kwa usalama.
Ameeleza kuwa jumla ya shilingi milioni 56 zinahitajika kukamilisha ujenzi huo wa nyumba ya mwalimu pamoja na fensi amewaomba wadau kujitokeza kuchangia chochote walichonacho.
Kwa yeyote atakayeguswa, anaweza kuwasiliana naye moja kwa moja kupitia namba 0784 856 649.
Bi Zena Mtamba kutoka wilaya ya Masasi, ambaye ni amirathi wa kanda ya kusini na muhamasishaji wa kulea watoto yatima na wasiojiweza.
Amekabidhi mchango wa shilingi milioni 1 na laki moja kwa kituo hicho na kusisitiza kuwa malezi ya watoto si jukumu la serikali pekee bali kila mwanajamii anapaswa kushiriki.
Aidha, ametangaza kuwa kongamano lijalo litafanyika wilayani Masasi mwezi Oktoba au Novemba.
Kwa upande wake, Bi Lulu Ramadhani, mjane mwenye watoto wanne, ameeleza kwa hisia namna kituo hicho kilivyomsaidia baada ya mume wake kufariki dunia akiwa mjamzito wa miezi saba.
Amemshukuru Bi Aziza kwa moyo wake wa huruma na kujitolea, akisema kuwa kupitia msaada wa kituo hicho, yeye na mke mwenzie wameweza kulea watoto wao kwa heshima na utu pamoja na kupatiwa mahitaji muhimu.
Kongamano hili limekuwa jukwaa muhimu la kujadili changamoto mbalimbali zinazowakumba watoto yatima na wajane, huku likiwaunganisha wanawake wa dini tofauti kwa lengo la kusaidia jamii.
Wanawake hao wametoa wito kwa viongozi wa serikali, vyama vya siasa na wananchi kwa ujumla kujitokeza kusaidia kundi hilo lenye uhitaji mkubwa, ili kuepusha watoto kuingia katika mazingira ya hatari na ukatili wa kijinsia.
Mjane aliesaidiwa na kituo cha Luhila kwa Mangoma Bi Lulu Ramadhani pichani akiwa na mwanae ambaye aliachwa na mumewe akiwa na ujauzito wa miezi saba pindi mume wake anafariki dunia
By Mpekuzi
Post a Comment