Mamia ya waombolezaji wamejitokeza kuaga mwili na kushiriki mazishi ya aliyekuwa Diwani wa Kata ya Solwa, Mhe. Awadh Mbarak Aboud, aliyefariki dunia katika ajali ya barabarani iliyotokea Jumapili Julai 20, 2025.

Marehemu Awadh (PICHANI), ambaye pia alikuwa ameonyesha nia ya kugombea tena nafasi ya udiwani kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), alifariki dunia Julai 19,2025 katika ajali iliyotokea eneo la Ibadakuli, barabara kuu ya kuelekea Shinyanga Mjini, baada ya bajaji aliyokuwa akisafiria kugongwa na basi la abiria la Kampuni ya Frester, ambapo watu wawili walipoteza maisha.
Mazishi hayo yamefanyika Julai 21, 2025, yakihudhuriwa na viongozi wa serikali, vyama vya siasa, ndugu, jamaa, marafiki na wakazi wa Kata ya Solwa waliofika kumuaga kiongozi huyo kijana na mpenda maendeleo.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, akitoa salamu za pole kwa niaba ya Serikali, amesema kifo cha Awadh kimeacha simanzi kubwa kwa jamii, lakini pia ni ukumbusho kwa wote kuhusu maisha na muda tulionao duniani.
“Kila mmoja kwa imani yake amuombee pumziko la amani marehemu Awadh. Tumepoteza kijana mchapakazi, mwenye ndoto za maendeleo kwa wananchi wa Solwa,” amesema Mhe. Mhita.
Mbunge wa Jimbo la Solwa anayemaliza muda wake, Mhe. Ahmed Salum, kwa huzuni ameeleza namna marehemu Awadh alivyokuwa na moyo wa kujitolea na kushirikiana naye bega kwa bega katika kusukuma miradi ya maendeleo ya kata hiyo.
“Alikuwa kijana mwenye moyo wa kazi, alinisumbua kwa maendeleo ya wananchi. Tutamkumbuka daima,” amesema Mhe. Salum.
Ngasa Mboje, aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, alisema marehemu alikuwa kiongozi mwenye kujituma, mchangiaji wa hoja makini katika vikao vya madiwani na mfuatiliaji wa karibu wa miradi ya maendeleo ya kata yake.
“Alikuwa mfano wa kuigwa miongoni mwa madiwani. Aliweka mbele maslahi ya wananchi,” amesema Mboje.
Kwa mujibu wa taarifa za familia, marehemu ameacha mke na watoto, na jamii imeombwa kuendelea kuwaombea nguvu na faraja katika kipindi hiki kigumu.

















By Mpekuzi









Post a Comment