
Na Regina Ndumbaro Masasi-Mtwara
Victor Thomas (39), mkazi wa Kijiji cha Lupaso wilayani Masasi, Mkoani Mtwara, anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za mauaji ya mchungaji wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG), Thomas Mkasimangwo (58), tukio lililotokea Juni 27, 2025 katika Mtaa wa Misheni, kijijini hapo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Mtwara, siku ya tukio mtuhumiwa alienda kanisani akiambatana na baadhi ya ndugu zake kwa ajili ya kupatiwa huduma ya kiroho (maombi), kutokana na matatizo yanayodaiwa kuwa ni ya kiafya, ikiwemo ugonjwa wa kifafa.Taarifa hiyo imeeleza kuwa baada ya maombi kufanyika kwa muda mrefu, mtuhumiwa alionekana kuchoka, hivyo ndugu kwa kushirikiana na marehemu walimrejesha nyumbani kwa ajili ya kuendelea na maombi.
Hata hivyo, walipofika karibu na nyumbani, Victor aliruka kutoka kwenye pikipiki, akaingia ndani ya nyumba na kutoka akiwa na panga.
Alimkimbiza mchungaji Mkasimangwo, kisha kumshambulia kwa panga sehemu mbalimbali za mwili wake, na kusababisha majeraha makubwa yaliyosababisha kifo chake.
Jeshi la Polisi limesema kuwa Victor ni muumini wa Kanisa la TAG na amekuwa akipatiwa huduma za kiroho kwa zaidi ya mwaka, ikiwa ni pamoja na kuombewa na mchungaji huyo aliyepoteza maisha.
Uchunguzi wa tukio hilo bado unaendelea, na mtuhumiwa atafikishwa mahakamani mara baada ya taratibu za awali kukamilika.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mtwara limewataka wananchi na waumini wa Kanisa la TAG kuendelea kuwa watulivu na kuvuta subira wakati uchunguzi ukiendelea.
By Mpekuzi
Post a Comment