Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amekutana na kufanya mazungumzo na Mwenyekiti na Mtendaji Mkuu wa Dangote Group, Alhaj Aliko Dangote, Ikulu jijini Dar es Salaam, ambapo wamejadili fursa za kuimarisha uwekezaji nchini.
Katika mazungumzo hayo, Dangote ameonyesha nia ya kampuni yake kupanua uwekezaji wake nchini kupitia sekta mbalimbali za kimkakati zenye mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi.
Maeneo yaliyojadiliwa ni pamoja na miundombinu ya usafirishaji, uzalishaji wa mbolea na nishati, ambayo yanatajwa kuwa na uwezo wa kuchochea maendeleo ya viwanda, biashara na shughuli za kiuchumi nchini na katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Dangote amesema Tanzania ina mazingira mazuri ya uwekezaji na fursa nyingi za kukuza viwanda vinavyoongeza thamani ya malighafi za ndani pamoja na kuimarisha biashara ya kikanda.
"Tumetambua maeneo yenye manufaa makubwa kwa Tanzania na tuko tayari kushirikiana na Serikali kuyaendeleza kwa manufaa ya pande zote," amesema Dangote.
Kwa upande wake, Rais Dkt. Samia amesema Serikali imepokea mapendekezo hayo na imezielekeza wizara pamoja na taasisi husika kuendelea na majadiliano ya kitaalamu ili kutathmini utekelezaji wake kwa kuzingatia sera, sheria na vipaumbele vya maendeleo ya taifa.
Aidha, Rais Samia amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi katika kuvutia uwekezaji wenye tija unaochochea ukuaji wa uchumi, maendeleo ya viwanda, uhamishaji wa teknolojia na ujenzi wa ajira kwa Watanzania
By Mpekuzi



Post a Comment