MRADI WA BARABARA YA LUTUKIRA-SONGEA WABUNGE WATAKA HAKI NA USALAMA KWA WAFANYAKAZI |Shamteeblog.

barabara ya Lutukira-Songea yenye urefu wa kilomita 100 pamoja na barabara ya mchepuko yenye kilomita 16 iliyotembelewa na wabunge wa mkoa wa Ruvuma yenye thamani ya shilingi bilioni 150
Meneja wa TANROADS mkoa wa Ruvuma mhandisi Saleh Juma wa kwanza kutoka kulia akiwa na wabunge wa mkoa wa Ruvuma walipotembelea na kukagua maendeleo ya mradi huo wa barabara ya Songea-lutukira yenye kilomita 100 na barabara ya mchepuko yenye kilomita 16

Na Regina Ndumbaro Songea-Ruvuma.

Wabunge wa mkoa wa Ruvuma wamezitaka taasisi zinazosimamia ujenzi wa barabara ya Lutukira–Songea yenye urefu wa kilomita 100 pamoja na barabara ya mchepuko ya kilomita 16, kuhakikisha haki za wafanyakazi zinalindwa kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo ya kazi.

Wabunge hao wametoa msisitizo huo walipotembelea na kukagua maendeleo ya mradi huo wenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 150, wakieleza kuwa ustawi wa wafanyakazi ni msingi muhimu wa utekelezaji wenye mafanikio.

Katika ziara hiyo wamesisitiza kuwa pamoja na kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati, ni muhimu utu, usalama na mazingira bora ya kazi kwa wafanyakazi vikapewa kipaumbele. 

Wamesema hatua hiyo itaongeza ari ya kazi, ufanisi na tija katika utekelezaji wa mradi, huku ikichochea maendeleo ya sekta ya miundombinu na uchumi wa mkoa wa Ruvuma.

Kwa upande wake, Meneja wa TANROADS mkoa wa Ruvuma, mhandisi Saleh Juma, amesema utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 10, ambapo kazi mbalimbali za awali zinaendelea kufanyika katika maeneo tofauti ya mradi kwa mujibu wa ratiba iliyopangwa.

Mhandisi Saleh  ameeleza kuwa TANROADS itaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa mradi huo ili kuhakikisha unakamilika kwa wakati, kwa viwango vya ubora vinavyotakiwa na kwa kuzingatia thamani ya fedha. 

Ameongeza kuwa kukamilika kwa barabara hiyo kutarahisisha usafiri na usafirishaji, kuchochea shughuli za kiuchumi na kuboresha huduma kwa wananchi wa mkoa wa Ruvuma.




By Mpekuzi

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post