Na: OWM (KAM), Dodoma
Watumishi wa umma vijana na wanawake katika wizara na taasisi wamepatiwa mafunzo maalum ya kuwajengea uwezo katika kukuza tija na kuimarisha utendaji kazi kwa lengo la kuongeza ufanisi wa utoaji huduma bora na kuchochea maendeleo .
Mafunzo hayo yametolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira na Mahusiano kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Korea Kusini (KOICA) jijini Dodoma 16 Julai 2026 ambapo watumishi vijana na wanawake kutoka Ofisi ya Rais Utumishi na Maendeleo ya Vijana pamoja na wanufaika wa programu za KOICA (Almni)
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo Kaimu Mkurugenzi wa Ajira na Ukuzaji Ujuzi Bi. Alana Nchimbi aliyemwakilisha Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira na Mahusiano Bi.Mary Maganga amesema vijana na wanawake wana mchango mkubwa katika ukuzaji tija kwenye utumishi wa umma.
Bi. Alana aliongeza kusema vijana na wanawake ni sehemu muhimu ya nguvu kazi na kwa kuwa wana uwezo mkubwa wa kuchangia ukuaji wa tija, kuongeza ufanisi na kuboresha utendaji wa sekta ya umma huku ikihakikisha vikwazo vya kiutendaji vinaondolewa
“Yatupasa kwa pamoja kuongeza jitihada za kuondoa vikwazo kwa vijana na wanawake, hivyo Ofisi ya Waziri Mkuu itaendela kushirikiana na Korea Kusini kutoa nafasi za mafunzo ya kuongeza tija kwa watumishi wa umma ili wananchi wapate huduma bora” alisisitiza Bi.Alana.
Kwa upande wake Balozi wa Korea Kusini nchini Tanzania Mheshimiwa Eunju Ahn amesema kuwa Serikali ya Jamhuri ya Korea kupitia Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Korea (KOICA) itaendelea kufanya kazi kwa karibu na Serikali ya Tanzania katika kuimarisha uwezo wa sekta ya umma kwa kutoa programu za mafunzo kwa vijana na wanawake.
Balozi Ahn aliongeza kusema watanzani wengi wameendelea kufadhiliwa kushiriki mafunzo ya aina mbalimbali nchini Korea Kusini ambayo yamewajengea ujuzi na maarifa ya kukuza tija kwenye utumishi wa umma.
Katika hatua nyingine Balozi huyo aliwapongeza wanufaika wa programu za mafunzo za KOICA kwa kuandaa mafunzo haya nchini Tanzania hatua inayoonesha kwa dhati kukuwa kwa uhusiano baina ya nchi hizi mbili.
Naye mmoja wa wanufaika wa mafunzo hayo ambaye pia ni Mhadhiri Msaidizi wa Chuo cha Mipango na Maendeleo Vijijini (IRDP) Dominic Joseph amesema mafunzo hayo yamelenga la kubadilishana uzoefu na kujengeana uwezo wa kukuza tija kwenye utekelezaji wa maeneo yao ya kazi kufuatia mafunzo waliyoyapata nchini Korea Kusini kwa miaka tofauti tofauti.
Kadhalika aliongeza kusema mafunzo hayo yanatarajiwa kuwa chachu ya mabadiliko kwa washiriki waliopata mafunzo kwa kuwapa maarifa na mbinu zitakazowawezesha kuhamasisha wanawake na vijana kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya sekta ya umma na kuongeza mchango wao katika maendeleo ya taifa.
By Mpekuzi



Post a Comment