Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Nyerere na Mkuu wa kanda ya kusini Kamanda Deogratus Ndelolia akijibu hoja ya Mheshimiwa Mbunge na Waziri wa Katiba na Sheria Dkt.Juma Zuberi Homera baada ya kuombwa kutekeleza na kudhibiti wanyama wakali wanaoingia katika maeneo ya wananchi kijiji cha Mandela na uharibifu wa mazao ya chakula
Wananchi waliojitokeza katika ziada ya Mheshimiwa Waziri wa Katiba na Sheria na Mbunge wa Jimbo la Namtumbo Dkt.Juma Zuberi Homera kwa lengo la kutoa kero zao ili zifanyiwe kazi kwa vitendo Na Regina Ndumbaro
Namtumbo-Ruvuma
Waziri wa Katiba na Sheria na Mbunge wa Jimbo la Namtumbo, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera, amemuomba Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Nyerere na Mkuu wa Kanda ya Kusini, Kamanda Deogratus Ndelolia, kuongeza nguvu katika kudhibiti wanyama wakali wanaoingia katika maeneo ya wananchi na kusababisha uharibifu wa mazao na kuhatarisha usalama wao.
Dkt. Homera ametoa ombi hilo wakati wa ziara yake katika Kijiji cha Mandela, akieleza kuwa wananchi wanahitaji kuona hatua zaidi za kuzuia wanyama hao kufika katika makazi na mashamba yao.
Akijibu hoja hiyo, Kamanda Deogratus Ndelolia amesema kuna changamoto ya mgongano kati ya binadamu na wanyamapori, lakini TANAPA imeendelea kuchukua hatua mbalimbali kukabiliana nayo.
Amesema eneo la Selous lililokuwa pori la akiba kabla ya mwaka 2019 kwa sasa limegawanywa, huku TANAPA ikiendelea na jukumu la kuhifadhi na kulinda Hifadhi ya Taifa Nyerere pamoja na maeneo muhimu ya vyanzo vya maji.
Amesema wanyama wamegundua maeneo salama ya kuishi na kuzaliana, hivyo wakati mwingine hukaribia makazi ya wananchi, lakini mikakati ya kupunguza migongano hiyo inaendelea kutekelezwa.
Ndelolia amesema kwa sasa kuna kituo cha kudhibiti wanyama wakali Nambecha chenye askari, gari na pikipiki, pamoja na kituo cha muda cha kudhibiti wanyama kilichopo Likuyu Seka.
Aidha, amesema askari wa wanyamapori wa vijiji wanalipwa na TANAPA, huku Hifadhi ya Taifa Nyerere ikiwa na magari mawili katika eneo hilo, pikipiki moja upande wa Likuyu na ndege nyuki kwa ajili ya shughuli za udhibiti.
Ameahidi kupokea ombi la Dkt. Homera la kuongeza vituo vya kuzuia wanyama wakali katika maeneo ya Mchomoro, Likuyu na Ligela na kulifikisha sehemu husika kwa hatua zaidi.
Kwa upande wake, kwa niaba ya wananchi, Johackim James Mapunda amesema changamoto ya wanyama pori, hususan tembo na fisi, imekuwa kubwa kutokana na kuingia katika mashamba na makazi ya wananchi.
Amesema wanyama hao wamekuwa wakiharibu mazao na ametolea mfano wa shamba lake la mbaazi lililoharibiwa na tembo.
Pia ameiomba serikali kuimarisha udhibiti wa wanyama katika barabara ya Likuyu-Mandela, akieleza kuwa wananchi na wanyama hukutana mara kwa mara katika eneo hilo.
Amesema wananchi wanahitaji nguvu zaidi katika kukabiliana na changamoto hiyo, ikiwemo kuimarishwa kwa vituo na hatua nyingine za kuzuia wanyama kufika katika makazi yao.






By Mpekuzi

Post a Comment