EWURA CCC YATOA ELIMU YA HAKI NA WAJIBU WA WATUMIAJI WA HUDUMA ZA NISHATI NA MAJI |Shamteeblog.



Na Dotto Kwilasa, Dodoma

Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA CCC) limewataka watumiaji wa maji, umeme, mafuta ya petroli na gesi asilia kufahamu haki na wajibu wao ili kulinda maslahi yao, kupata huduma salama na kudai stahiki wanapokutana na changamoto.

Wito huo umetolewa Septemba 18, 2026, jijini Dodoma wakati EWURA CCC ikitoa elimu kwa wanafunzi wa Chuo cha VETA Dodoma.

Akizungumza katika zoezi hilo, Afisa Huduma kwa Wateja Mwandamizi wa EWURA CCC, Amani Mbogo, amesema mtumiaji ana haki ya kupata huduma za msingi kwa kuzingatia viwango vya ubora, usalama na bei zilizoidhinishwa na mdhibiti.

Mbogo amesema miongoni mwa haki za watumiaji ni kupata taarifa sahihi na za kutosha kuhusu huduma wanazotumia, ikiwemo taarifa za mabadiliko ya bei au kusitishwa kwa huduma kutokana na matengenezo. Pia mtumiaji ana haki ya kuchagua huduma kwa kuzingatia bei na ubora.

Amesema watumiaji pia wana haki ya kupata huduma salama na kulindwa dhidi ya bidhaa au huduma zinazoweza kuhatarisha afya na maisha yao. Aidha, mtumiaji anaweza kudai utatuzi wa malalamiko na fidia pale anapopata hasara kutokana na huduma, kwa mujibu wa taratibu zinazohusika.

Mbogo amesema EWURA CCC inaweza pia kumsaidia mtumiaji mwenye changamoto ya kusoma na kuandika, mgonjwa au mzee katika kuwasilisha malalamiko na kufuatilia haki yake.

Kwa upande wa wajibu, watumiaji wametakiwa kufuata taratibu halali wakati wa kuomba kuunganishiwa huduma za maji au umeme na kuepuka njia zisizo rasmi.

Pia wametakiwa kutoa taarifa kwa watoa huduma wanapoona changamoto katika miundombinu, kama bomba lililopasuka, majitaka yanayovuja, nguzo ya umeme iliyoanguka au nyaya hatarishi, ili hatua zichukuliwe mapema na kuzuia madhara zaidi.

Vilevile, watumiaji wana wajibu wa kutunza miundombinu ya maji na nishati na kutoa taarifa kuhusu vitendo vya uharibifu, wizi au hujuma. Mbogo pia amewataka watumiaji kujielimisha kuhusu huduma wanazotumia, ikiwemo namna ya kusoma mita, kutunza kumbukumbu za matumizi na kuzingatia usalama.

EWURA CCC imesema itaendelea kutoa elimu kwa makundi mbalimbali ya wananchi jijini Dodoma na maeneo mengine ili kuongeza uelewa kuhusu haki na wajibu wa watumiaji wa huduma za nishati na maji.







By Mpekuzi

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post