STAMICO YACHUKUA TAHADHARI YA MVUA ZA EL NIÑO |Shamteeblog.


NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

SHIRIKA la Madini la Taifa (STAMICO) limeanza kuchukua tahadhari kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua za El Niño, baada ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kueleza kuwa mvua hizo zinatarajiwa kuimarika katika maeneo mbalimbali nchini kuanzia wiki ya nne ya Septemba hadi Oktoba mwaka huu.

Hayo yameelezwa wakati Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Ladislaus Chan’ga aliipokutana na menejimenti, wafanyakazi na wataalamu wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), kwa ajili ya kutoa elimu kuhusu hali ya El Niño na namna ya kutumia taarifa za hali ya hewa katika kupanga shughuli zao.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Deusdedith Magara, amesema shirika hilo limechukua tahadhari kubwa kutokana na ukweli kwamba shughuli zake nyingi za uchimbaji, utafiti na uchenjuaji wa madini hufanyika katika maeneo ya porini ambayo yanaweza kuathiriwa na mvua kubwa.

Amesema mvua nyingi zinaweza kusababisha usumbufu katika shughuli za uchimbaji na shughuli nyingine zinazohusiana na madini, hali ambayo inaweza kuathiri uzalishaji na mapato ya STAMICO.

“Madini yanachimbwa porini, hayachimbwi mjini. Kwa hiyo watu wetu wametawanyika huko. Mvua ikinyesha sana sisi hatuwezi kuendelea na kazi kwa sababu kazi yetu ni kuchimba madini, kufanya utafiti wa madini na kuchenjua madini, na vyote hivyo mvua inaviathiri sana,” amesema.

Amesema mapato makubwa ya shirika yanatokana na shughuli zinazofanyika katika maeneo hayo, hivyo kuvurugika kwa operesheni kutokana na mvua kunaweza kuathiri pia mapato ya STAMICO.

Ameongeza kuwa STAMICO itaendelea kuwaelimisha watumishi wake waliotawanyika katika maeneo mbalimbali nchini na kuhakikisha wanafuatilia taarifa na maelekezo yatakayotolewa na TMA.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Chan’ga, amesema hali ya El Niño ipo na kwamba mamlaka hiyo inatarajia mvua kuanza kuimarika katika maeneo mbalimbali ya Tanzania katika kipindi cha mwisho wa Septemba na mwanzoni mwa Oktoba.

Amesema kuanzia wiki ya nne ya Septemba na wiki ya kwanza ya Oktoba, mvua zinatarajiwa kuanza kuimarika katika ukanda wa Ziwa Victoria, hususan mikoa ya Geita, Kagera, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Mara.

Dkt. Chan’ga amesema wiki ya kwanza na ya pili ya Oktoba mvua hizo zinatarajiwa kuanza katika Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki, zinazojumuisha mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara.

Amesema pia maeneo ya Pwani ya Kaskazini, yakiwamo Tanga, Dar es Salaam, kaskazini mwa Morogoro, Pwani, Mafia pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba, yanatarajiwa kuanza kupata mvua katika wiki ya kwanza na ya pili ya Oktoba.

Kwa mujibu wa Dkt. Chan’ga, katika maeneo hayo mvua zinatarajiwa kuwa juu ya wastani hadi wastani.

Hata hivyo, amesema wananchi na taasisi mbalimbali wanapaswa kuendelea na shughuli zao za kawaida huku wakizingatia taarifa za hali ya hewa zinazotolewa na TMA.

Amesema TMA itaendelea kutoa utabiri wa msimu pamoja na taarifa za utabiri wa siku 10, siku tano na taarifa za kila siku ili kuwawezesha wadau kupanga na kutekeleza shughuli zao za kiuchumi na kijamii kwa kuzingatia mwenendo wa hali ya hewa.

“Wananchi waendelee na shughuli zao za kiuchumi na kijamii, lakini tuendelee kufuatilia ipasavyo taarifa za hali ya hewa zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania,” amesema.

Dkt. Chan’ga pia amewataka wananchi kuzingatia maelekezo ya viongozi wa Serikali pamoja na ushauri wa wataalamu wa sekta mbalimbali ili kuimarisha mipango na maandalizi ya kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mwenendo wa hali ya hewa.

Amesema ushirikiano kati ya TMA na taasisi kama STAMICO ni muhimu katika kuhakikisha taarifa za hali ya hewa zinatumika ipasavyo katika kupanga na kutekeleza shughuli za uzalishaji.

Kwa upande wa STAMICO, Magara amesema elimu iliyotolewa na TMA imewasaidia watumishi kuelewa zaidi hali inayotarajiwa na namna ya kuendelea na shughuli zao huku wakizingatia tahadhari.

Amesema shirika litaendelea kufuatilia taarifa za TMA na kuchukua hatua kulingana na ushauri wa wataalamu ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza katika shughuli zake za uchimbaji, utafiti na uchenjuaji wa madini.



By Mpekuzi

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post