Na Marco Maduhu, Stela Paul, SHINYANGA
Mbunge wa Jimbo la Itwangi Azza Hillal Hamad, amesema wananchi wa Kijiji cha Ngaganulwa Kata ya Usanda wilayani Shinyanga, hivi karibuni wataondokana na adha ya ukosefu wa maji, baada ya yeye kuzungumzia bungeni changamoto hiyo ya ukosefu wa maji, na kisha serikali kuanza kutoa fedha kwa ajili ya usambazaji wa maji kutoka Ziwa Victoria.
TAZAMA VIDEO👇👇
Amebainisha hayo leo Septemba 30, 2026, wakati akizungumza na wananchi wa kijiji hicho katika mkutano wa hadhara wa kuwashukuru, pamoja na kusikiliza kero zao na kuzitolea majibu.
Amesema, maji hayo yatatoka katika Tenki la Buchama, ambayo yatapita kijiji cha Jomu, na kisha kufika kijiji hicho cha Ngaganulwa hadi Usanda.
“Awamu ya kwanza katika Kijiji cha Ngaganulwa vitawekwa vituo vya kuchotea maji, ili wananchi muanze kutumia hayo maji. Baada ya hapo, awamu ya pili mtaruhusiwa sasa kila mwenye uwezo wa kuvuta maji nyumbani kwake avute,” amesema Azza.
Katika hatua nyingine, amewapongeza wananchi wa kijiji hicho kwa kuanzisha ujenzi wa zahanati kwa nguvu zao wenyewe, na kufikia hatua ya renta pamoja na kuweka jamvi, huku akiwaunga mkono kwa kuwapatia fedha Sh. 405,000 ambazo wanadaiwa katika ujenzi huo.
Aidha, ameahidi kuwa katika bajeti zake mwakani ataingiza zahanati hiyo ili iweze kupauliwa.
Naye Meneja wa RUWASA wilayani Shinyanga, Mhandisi Emmael Nkopi, akizungumza kwa njia ya simu kwenye mkutano huo, amesema baada ya maagizo ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, walitembelea maeneo ya Itwangi, ikiwamo Kata ya Usanda, na tayari wamefanya usanifu.
Amesema watatoa maji katika Tenki la Buchama, na tayari wamepewa kibali cha kupeleka maji Kijiji cha Singita na kufika Kijiji cha Ngaganulwa, kwa sababu kipo njiani kuelekea Singita, huku akibainisha kuwa, tayari wametangaza ununuzi wa mabomba.
Changamoto nyingine zilizozungumziwa kwenye mkutano huo ni pamoja na ubovu wa miundombinu ya barabara, na ukosefu wa umeme katika ngazi ya vitongoji.
TAZAMA PICHA👇👇
Mbunge wa Jimbo la Itwangi Azza Hillal Hamad akizungumza kwenye mkutano wa hadhara na wananchi wa Kijiji cha Ngaganulwa.

By Mpekuzi

























































Post a Comment