MOTO MV CHAMBO WATU 3 WAFARIKI ,ZAIDI YA 40 WAOKOLEWA ZIWA NYASA |Shamteeblog.

MV Chambo iliyoteketea kwa moto Ziwa Nyasa na kusababisha vifo vya watu watatu na majeruhi 40 alfajiri ya saa 10:30 katika eneo la Chiulu Wilayani Nyasa 
MV Chambo kabla ya kuteketea na moto ziwa Nyasa mkoani Ruvuma na kusababisha vifo vya watu watatu na majeruhi 40 
Na Regina Ndumbaro-Ruvuma 

Moto uliozuka ndani ya meli ya MV Chambo katika Ziwa Nyasa umesababisha vifo vya watu watatu wa mataifa tofauti, huku zaidi ya watu 40 wakifanikiwa kuokolewa baada ya tukio hilo lililotokea wakati meli hiyo ikisafiri kutoka Tanzania kuelekea Msumbiji.

Tukio hilo limetokea Jumapili, Oktoba 11, 2026, saa 10:30 alfajiri katika eneo la Chiulu, Wilaya ya Nyasa, mkoani Ruvuma, ambapo meli hiyo ilikuwa imebeba abiria 44 pamoja na tani 10 za mzigo.

 Kwa mujibu wa Mkuu wa Wilaya ya Nyasa, Mheshimiwa Peresi Magiri, abiria waliokuwamo ndani ya meli hiyo walikuwa raia 23 wa Msumbiji, 15 wa Tanzania, wanne wa Malawi na wawili wa Lesotho.

Magiri amethibitisha kuwa waliofariki katika tukio hilo ni mtoto wa kike raia wa Msumbiji, mwanamke raia wa Malawi na Mtanzania Yuston Chatanda, mkazi wa Nombe. 

Aidha, amesema juhudi za uokoaji na kuzima moto zinaendelea chini ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, huku mamlaka husika zikiendelea kufuatilia hali ya manusura na kutoa taarifa zaidi kuhusu tukio hilo.

Amesema mawasiliano yanaendelea kati ya mamlaka za Tanzania na nchi za Malawi na Msumbiji kuhusu hatua zinazopaswa kuchukuliwa, huku Msumbiji ikiwa tayari imetuma boti ndogo kwa ajili ya kuchukua mwili wa raia wake aliyefariki. 

Wakati juhudi za kukabiliana na athari za tukio hilo zikiendelea, chanzo cha moto na hali kamili ya meli hiyo vinatarajiwa kufahamika baada ya uchunguzi na taarifa rasmi za mamlaka husika.



By Mpekuzi

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post