
Na Regina Ndumbaro, Ruvuma
Katika kipindi ambacho matumizi ya nishati yanaendelea kuwa sehemu muhimu ya maisha ya kila siku na shughuli za uzalishaji, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Ruvuma limewataka wananchi kuacha kuutazama umeme kama huduma ya kawaida pekee, bali kuutumia kama nyenzo ya kuongeza uzalishaji na kukuza uchumi wa familia na jamii.
Wito huo umetolewa wakati mkoa huo ukianza kuadhimisha Wiki ya Huduma kwa Wateja kuanzia Oktoba 5 hadi 9, 2026, yenye kaulimbiu isemayo “Extra Mile”, inayolenga huduma za viwango na bora zaidi na kuhakikisha wateja wanaridhika.
Mkuu wa Kitengo cha Huduma kwa Wateja TANESCO Ruvuma, Allan Njiro, amesema shirika limejipanga kuhakikisha wananchi wanafikiwa kwa karibu na kupewa elimu itakayowawezesha kutumia umeme kwa ufanisi.
Njiro amesema TANESCO itaendelea kuwafikia wananchi katika maeneo mbalimbali, ikiwemo maeneo ya Msamala, Stendi ya Zamani na Bombambili, kwa ajili ya kusikiliza changamoto zao na kutoa elimu kuhusu matumizi ya umeme.
Amesema miongoni mwa mambo yatakayopewa msukumo ni matumizi ya nishati safi pamoja na vifaa vinavyotumia umeme kwa ufanisi.
Amesema Jumatano itakuwa siku maalumu ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi, ambapo wataalamu watapita kwa wananchi kutoa elimu kuhusu nishati safi na namna ya kutumia vifaa vya umeme vinavyotumia nishati kidogo.
Akisisitiza umuhimu wa matumizi ya umeme katika shughuli za kila siku, Njiro amewataka wananchi kutokuwa na hofu ya kutumia umeme kwa matumizi ya majumbani na shughuli nyingine za uzalishaji.
Ametoa mfano wa matumizi ya pressure cooker katika kupika maharage, akieleza kuwa matumizi yake yanaweza kuwa nafuu na kutumia takribani Unit moja, kulingana na matumizi.
Amesema wananchi wanapaswa kuutazama umeme kama sehemu ya maisha inayoweza kusaidia kuongeza ufanisi na kuchochea shughuli za kiuchumi, badala ya kutumia njia mbadala ambazo zinaweza kuwa na madhara kwa jamii.
Njiro amesema TANESCO inaendelea kufanya maboresho ili huduma ya umeme iwe rahisi na ipatikane kwa ukaribu zaidi, huku akiwataka wananchi kutumia njia rasmi za mawasiliano wanapohitaji huduma au wanapokutana na changamoto.
Amesema namba 180 ya huduma kwa wateja imeendelea kurahisisha mawasiliano, hivyo mteja anaweza kutoa taarifa bila kulazimika kufika ofisini.
Kwa upande wake, Meneja TANESCO Mkoa wa Ruvuma, Mhandisi Elisius Mhelela, amesema kazi ya shirika hilo inahitaji matokeo yanayoonekana, akisisitiza kuwa wananchi wanahitaji umeme na si maneno, huku akieleza kuwa ushirikiano wa timu ni muhimu katika kuhakikisha kila changamoto ya mteja inapata ufumbuzi.
Maadhimisho hayo yamehusisha viongozi na watendaji mbalimbali wa TANESCO Mkoa wa Ruvuma, wakiwemo mameneja wa wilaya zote za mkoa huo, kwa lengo la kuunganisha nguvu katika utoaji wa elimu na huduma kwa wananchi.
Wananchi wa Songea wameeleza kuona maboresho katika huduma, huku Saidi Mohamed Malowa akisema kwa sasa huduma inapatikana kwa haraka zaidi na foleni zimepungua.
Evodia Luambano naye amewataka wananchi kutoa taarifa mapema wanapopata changamoto ili TANESCO iweze kuchukua hatua kwa wakati, huku akiwahimiza wale ambao bado hawajaunganishiwa umeme kufuata taratibu ili waweze kupata huduma hiyo.




By Mpekuzi

Post a Comment