
Na: OWM–TAMISEMI, Arusha
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, amehimiza usimamizi mzuri wa fedha za miradi ya maendeleo aliyoitembelea na kuikagua jijini Arusha ya ujenzi wa miundombinu ya barabara za AFCON na miradi ya TACTIC, akisisitiza kuwa hatua stahiki zitachukuliwa dhidi ya watakaobainika kutumia fedha hizo kinyume na malengo yaliyokusudiwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Miradi aliyoikagua Prof. Shemdoe Novemba 28, 2026 ni ya ujenzi wa miundombinu ya barabara za kuelekea na kuzunguka uwanja mpya wa AFCON, ikiwemo barabara ya Mateves–Bondeni City yenye urefu wa kilomita 6.50, Lendita (km 2.75), Essuri (km 2.45), barabara inayozunguka uwanja huo (km 1.5), pamoja na daraja lenye urefu wa mita 100 katika barabara ya Essuri. Miradi mingine ni ya TACTIC inayohusisha ujenzi wa barabara za mjini zenye urefu wa kilomita 10.23, Kituo Kikuu cha Mabasi yaendayo Mikoani (Bondeni City Bus Terminal) na Soko la Kilombero.
Akizungumza wakati wa ukaguzi huo, Prof. Shemdoe amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutoa fedha hizo kwa ajili ya kuboresha miundombinu jijini Arusha, huku akisisitiza kuwa ni wajibu wa kila msimamizi kuhakikisha uwekezaji huo unaleta manufaa yaliyokusudiwa kwa wananchi.
“Mhe. Rais ameelekeza fedha zinazoletwa zitumike kwa malengo yaliyokusudiwa ili wananchi wanufaike na miradi kwa kupata huduma bora, hivyo hatutamfumbia macho yeyote atakayebainika kutumia fedha hizo tofauti na malengo yake,” amesisitiza Prof. Shemdoe.
Katika hatua nyingine, Prof. Shemdoe amesema ameridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa miundombinu ya barabara za kuelekea na kuzunguka uwanja mpya wa AFCON, ambao umefikia asilimia 71, ukiwemo ujenzi wa daraja lenye urefu wa mita 100 katika barabara ya Essuri. Kutokana na hatua hiyo, ameupongeza uongozi wa Mkoa, Wilaya na Jiji la Arusha kwa usimamizi mzuri wa utekelezaji wa miradi hiyo ambayo ikikamilika itawezesha wananchi kupata huduma bora.
Kuhusu miradi ya TACTIC, Prof. Shemdoe amesema ameridhishwa na kiwango cha ujenzi wa barabara za mjini zenye urefu wa kilomita 10.23, pamoja na hatua iliyofikiwa katika ujenzi wa Kituo Kikuu cha Mabasi yaendayo Mikoani (Bondeni City Bus Terminal) na Soko la Kilombero, ikilinganishwa na hali aliyokuta wakati wa ziara yake iliyopita.
Hata hivyo, amemtaka mkandarasi wa miradi ya Bondeni City Bus Terminal na Soko la Kilombero, kampuni ya Mohammedi Builders Limited, kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi hiyo ili ikamilike kwa wakati na kuanza kutoa huduma zilizokusudiwa kwa wananchi wa jiji la Arusha.











By Mpekuzi
Post a Comment