Kamusi ya kwanza ya Lugha ya alama ya Kigitali yazinduliwa Tanzania |Shamteeblog.

Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imezindua Kamusi ya kwanza ya lugha ya alama ya kidijitali yenye lengo la kupunguza changamoto ya mawasiliano katika ufundishaji na ujifunzaji kwa wanafunzi viziwi.

Akizindua kamusi hiyo Mkoani Tabora, katika kilele cha maadhimisho ya wiki ya viziwi yenye kauli mbiu “Kuhakikisha upatikanaji wa haki za binadamu kwa Viziwi”, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Ave Maria Semakafu amesema serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa makundi yote yenye ulemavu kupata elimu na huduma nyingine za kijamii.

Dkt Semakafu amesema pamoja na maboresho makubwa yaliyofanyika katika sekta ya elimu, kundi la viziwi lilikuwa limeachwa nyuma huku changamoto kubwa ikiwa ni mawasiliano na kutokuwepo kwa walimu wa kutosha hasa katika ngazi ya sekondari ndio maana imeandaa kamusi hiyo kuwe na lugha moja ya alama na kutoa mafunzo kwa walimu wanaofundisha katika shule zinazopokea watoto viziwi.

“Serikali inatambua umuhimu wa kuwa na lugha moja ya alama kwa ajili ya kuwezesha mawasiliano ya watumiaji wa lugha hiyo, hivyo itaendelea kusimamia uendelezaji na usanifishaji wa lugha ya alama ili kuwezesha utoaji elimu, kurahisisha ujifunzaji na kuboresha mawasiliano katika jamii.,”alisema Naibu Katibu Mkuu huyo.

Nae Kamisha wa Elimu
Dkt. Lyabwene Mtahabwa amesema kilele cha maadhimisho ya wiki ya viziwi duniani ndio mwanzo wa mafanikio katika mchakato wa ujifunzaji na ufundishaji nchini kwani ni siku ambayo kamusi ya lugha ya alama ya kwanza nchini tena ya kidijitali inazinduliwa pamoja na mwongozo wa utekelezaji wa mtaala wa elimu ya sekondari kwa wanafunzi viziwi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu Tanzania(TET)Dkt. Aneth Komba anasema Taasisi anayoisimamia ndio walipewa jukumu la kuandaa Kamusi hiyo na kwamba imeandaliwa kwa kufata taratibu zote ikishirikisha wadau wote na kwamba itatumiwa na wanafunzi viziwi kutoka Tanzania Bara na Visiwani.



By Mpekuzi

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post