Serikali imesema ipo kwenye mchakato wa kuongeza uzalishaji wa mafuta ya kula nchini kwa mazao yote yanayotoa mafuta ikiwemo alizeti, na michikichi ili kupunguza gharama za kuingiza mafuta kutoka nje ya nchi.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dodoma na Mkurugenzi wa udhibiti ubora {TBS} Bw.Lazaro Msasalaga wakati akitoa mafunzo kwenye semina kwa wazalishaji,wasambazaji,na wauzaji wa mafuta ya kula.
Mafunzo haya yamelenga kuwaelimisha wadau hao juu ya uzalishaji bora, uhifadhi sahihi wa bidhaa za mafuta haswa sehemu za kuuzia, ufungashaji sahihi na salama na umuhimu wa kuzingatia na kuweka taarifa sahihi na muhimu katika vifungashio.
Amesema lengo kubwa la serikali ni kuzingatia mahitaji makubwa ambayo kwa sasa wananchi wanahitaji ili kuweza kuzalisha mafuta ya kula kwa wingi nchini.
“Waziri ana mradi mkubwa wa kupanda michikichi kule Kigoma lengo kubwa ni kuongeza uzalishaji wa mafuta nchini, na si kwenye michikichi tu inaenda kuangalia na uzalishaji wa mazao mengine kama alizeti na namna Mkoa husika unavyoweza kuzalisha zao hilo“ amesema Msasalaga
Aidha amesema katika mafunzo hayo wamepita wilaya zote za mkoa wa Dodoma, Singida na Tabora ili kuweza kuwaelimisha wazalishaji na wauzaji namna ya kuyatunza mafuta ili yawe na ubora.
By Mpekuzi
Post a Comment