HESHIMA! Simba, Yanga zagawana pointi moja moja zikiwapa mashabiki pambano safi |Shamteeblog.

NA ASHA KIGUNDULA-DAR ES SALAAM

TIMU za Simba na Yanga, zimegawana pointi moja moja, katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara iliyochezwa jana Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.

Yanga ndio ilikuwa ya kwanza kupata bao kupata bao la kuongoza dakika ya 31 kwa mkwaju wa penalti wa Michael Sarpong, baada ya beki wa Simba Joash Onyango kumwangusha Tuisila Kisinda ndani ya eneo ya hatari.

Simba ilisawazisha dakika ya 89 kupitia kwa Onyango, aliyefunga kwa kichwa akiunganisha kona iliyochongwa na Kuis Miquisonne.

Kwa matokeo hayo, Yanga imefikisha pointi 24 na kuendelea kukamata nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu, baada ya kushuka dimbani mara 10, ikishinda michezo saba na sare tatu.

Simba baada ya sare ya jana, imefikisha pointi 20, baada ya kucheza michezo 20, ikishinda michezo sita, sare mbili na kupoteza michezo miwili.

Vinara wa ligi hiyo ni Azam iliyojikusanyia pointi 25,  baada ya kushuka dimbani mara 10, ikishinda michezo nane, sare moja na kuchapwa mara moja.

Dakika ya kwanza ya mchezo  Yanga ilifanya shambulizi lakini  mabeki wa Simba walikuwa makini na kuokosa mpira wa krosi ya Farid Mussa.

Yanga ilionekana kuwa na mpango kazi ya kupata bao la mapema kwani dakika ya saba, Kisinda alilimina krosi safi lakini  Sarpong alichelewa hivyo kuokolewa na mabeki wa Simba.

Yanga iliendelea kutawala mchezo na kufanya mashambulizi ya mara kwa mara kwenye lango la Simba.

Dakika ya 14 mkwaju wa Kisinda baada ya kupokea pasi ya  Farid ulipanguliwa na kipa wa Simba, Aishi Manula.

Dakika ya 28, Kisinda alimzidi kasi Onyango ambaye aliamua kutumia mbinu ya ziada kumsukuma hatua  iliyosababisha aanguke ndani ya  eneo la hatari na mwamuzi muamua ipigwe penalti.

Penalti hiyo ilipigwa kwa ufundi na Sarpong, ambaye alimhadaa Manula na kupeleka mpira upande wa kulia na kumwacha aangukie kushoto  na kuipa Yanga uongozi.

Licha ya Simba kujipanga upya ili kusawazisha bao, safu  ya ulinzi ya Yanga ilionekana kuwa imara kumlinda kipa wao Metacha Mnata asifikiwe.

Dakika 45 za kipindi cha kwanza zilikamilika kwa Yanga kwenda mapumziko ikiwa mbabe kwa bao 1-0 dhidi ya Simba.

Kipindi cha pili kilipoanza, Simba ilionekana kuingia uwanjani na nguvu zaidi ili kusaka bao la kusawazisha na pengine kufunga mengine.

Wakati huo, Yanga ilionekana kubadili mpango kazi ikionekana kuwaachia mpira wapinzani wao waumiliki na yenyewe ikifanya mashambulizi ya kushtukiza.

Dakika ya 47, mkwaju wa Miquissone ulitoka nje ya lango la Yanga.

Dakika ya 48, krosi ya Mohamed Hussein ilimkuta John Bocco  ambaye alitandika kichwa lakini mpira ulipaa juu ya lango la Yanga.

Yanga ilijipanga na  kufanya shambulizi dakika ya 78, ambapo mkwaju wa Feisal Salum ulionekana laini kwa Manula.

Ilifanya shambulizi jingine dakika ya 80, ambapo mkwaju wa Tuisila ulipanguliwa na Manula na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.

Wakati mashabiki wa Yanga wakiamini wataondoka na pointi tatu, Onyango alisawazisha kosa lake la kusababisha penalti kwa kufunga bao kwa kichwa akiunganisha kona na Miquissone.

Dakika ya 90 zilikamiribia  chungu kwa Simba, baada ya mkwaju mkali wa Feisal kupanguliwa Manula na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.

Dakika 90 za pambano hilo zilikamikika kwa  timu hizo kufungana bao 1-1.

Katika mchezo huo, Jonas Mkude na Onyango walionyeshwa kadi za njano kutokana na mchezo usio wa kiungwana, adhabu kama hiyo iliwakuta pia Tuisila na Feisal.

Kikosi Simba: Aish Manula,Shomari Kapombe,Mohamed Hussein,Pascal Wawa,Joash Onyango,Jonas Mkude,Luis Miqussone,Clatous Chama,Mzamiru Yassin,John Bocco, Lary Bwalya/Hassan Dilunga.

Kikosi Yanga:Metacha Mnata, Kibwana Shomari,Yassin Mustapha,Lamine Moro/Said Juma,Bakari Mwamnyeto,Mukoko Tonombe,Farid Musa,Feisal Salum,Michael Sarpong/Yacouba Sogn,Ditram Nchimbi,Tuisila Kisinda



from Author

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post