KAIMU KATIBU MKUU MPYA YANGA AFUNGUKA HAYA |Shamteeblog.

Zainab Iddy, Dar es salaam

KAIMU Katibu Mkuu mpya wa Yanga, Hajji Mfikirwa,ametaja mambo matatu atakayoyasimamia kuhakikisha yanafanikiwa wakati wa utekelezaji wa majukumu hayo mapya.

Akizungumza mara baada ya kutambulishwa kwa waandishi wa habari Makao Makuu ya Klabu ya Yanga jijini Dar es Salaam jana,Mfikirwa aliyataja mambo hayo kuwa ni kuhakikisha timu hiyo inatwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, ujenzi wa hosteli na uwanja wa mazoezi na mabadiliko ya mfumo  wa uendeshaji ya klabu hiyo.

“Najua changamoto ni kubwa kiutendaji, lakini naushukuru uongozi wa Yanga kwa kuniamini maana sina muda mrefu ndani ya Yanga, niliingia hapa June mwaka huu lakini nimeaminiwa kupewa nafasi kubwa.

“Nafahamu klabu ina mipango na malengo yake na mimi kazi yangu itakuwa kuisimamia kikamilifu ili ifanikiwe tukianzia na mambo mkuu matatu ambayo ni kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu, mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji, ujenzi wa hosteli na uwanja wa mazoezi, na hilo nitalifanya kwa kushirikiana na wenzangu,”alisema Mfikirwa.

Akizungumza wakati akimtambulisha Mfikirwa,Makamu Mwenyekiti Yanga, Fredrick Mwakalebela alisema kuwa,uamuzi wa kumteua Mfikirwa kukaimu nafasi hiyo ulifikiwa na Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo iliyokutana kwa dharura baada ya kusimamishwa kazi kwa Wakili Patick Simon ambaye alikuwa akikaimu nafasi hiyo.

Simon alisimamishwa kazi hivi karibuni, baada ya kukutwa na tuhuma za kuihujumu klabu hiyo.

“Kama ambavyo Kamati ya Utendaji ilikutana kwa dharura na kutoa uamuzi wa kumsimamisha Patrick, ndivyo ilivyoamua kumteua Mfikirwa kukaimu nafasi ya katibu mkuu.

“Mfikirwa ameanza majukumu yake leo(jana) na mgeni katika kuongoza klabu kubwa kama Yanga, uongozi tunaahidi kumpa ushirikiano wa kutosha, lengo ni kuipa maendeleo klabu yetu.”alisema Mwakalebela.

Kabla ya kukabidhiwa majukumu hao mapya, Mfikirwa alikuwa anahudumu pia nafasi ya Mkurugenzi wa Fedha wa Yanga

Yafufua sakata la Morrison, Kabwili

Mwakalebela ulilitaka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF),kusikiliza madai yao kuhusiana na uhalali wa mkataba wa mchezaji Bernard Morrison na Simba kabla ya dirisha dogo la usajili kufunguliwa Desema 15.

Yanga iliwasilisha malalamiko yake TFF, ikidai mkataba kati ya mchezaji huyo na Simba ulisajiliwa katika taasisi hiyo una kasoro, hivyo haupaswi kutambuliwa.

Mwakalebela alisema wamekumbushia suala hilo w akati huu wakihofia mkataba huo kurekebishwa wakati wa dirisha dogo la usajili kwakuwa mfumo huwa uko wazi.

Alisema kilichowashangaza zaidi ni  kitendo cha mchezaji wao huyo wa zamani kuwasilisha mkataba wake na Simba  katika  Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Michezo (Cas), ukiwa umesainiwa na pande zote, wakati kasoro za kutosainiwa ndizo zilizowafanya wao wapeleke malalamiko TFF.

“Yanga tuliwasilisha malalamiko TFF kuhusu tuhuma za rushwa za Kabwili aliyekuwa akishawishiwa na viongozi wa timu pinzani ili kuihujumu timu yetu, na hili tulilipeleka pia Takukuru (Taasisia ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa) lakini TFF kama baba wa mpira hapa Tanzania wamekaa kimnya hadi sasa,”alisema Mwakalebela.

Mabadiliko

Katika hatua nyingine, Mshauri wa Mabadiliko wa klabu hiyo, Senzo Mbatha alisema kuwa, mchakato wa mabadiliko uko kwenye hatua nzuri.

“Suala la mabadiliko ya uendesheji wa klabu lipo kwenye hatua nzuri na Jumatatu au Jumanne, timu ya watu kutoka Kamati ya Utendaji na wadhamini GSM itaelekea nchini Hispania kuchukua ripoti kamili kutoka La Liga katika hatua ya kwanza.

“Watarejea Tanzania mwanzoni mwa mwezi ujao na ripoti hiyo itawekwa hadharani kwa wanachama ili kila Mwanayanga ajue nini kinachofanyika katika mchakato huo.”



from Author

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post