Mwandishi Wetu
MOJA kati ya habari ambayo imeonekana kushtua wengi ni hatua ya Kamati ya Bunge la Umoja wa Ulaya kuhoji juu ya uminyaji wa haki za binadamu lakini pia vigezo vya kuipa Tanzania msaada wa Euro Milioni 27 takribani Shilingi bilioni 74 mapema mwaka huu kutoka Umoja wa Ulaya (EU) kukabiliana na athari za corona.
Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje wa Bunge hilo Dk. David McAllisster ndiye aliyehoji hayo.
Kitendo cha kamati ya Bunge hilo kuhoji tu masuala hayo, sisi tunaona kilipaswa kuzuiwa mapema kama ambayo tumekuwa tukishauri kupitia maoni kama haya ya mhariri.
Pamoja na kwamba tayari Serikali ya Tanzania imefafanua kuhusu kikao kilichojadili masuala hayo zikiwemo taarifa zilizosambaa mara moja kwenye mitandao ya kijamii kwamba EU imekusudia kuifutia Tanzania mikopo na misaada yote ambayo imeomba kwenye umoja huo na mashirika yake, lakini ilipaswa kufafanua kuhusu mambo mengine yaliyojadiliwa kama hilo la uminyaji wa haki za binadamu na vigezo vya kupewa fedha hizo kwa ajili ya kukabiliana na janga la corona ambalo ukweli ni kwamba katika miezi ya mwanzo ilitikisa nchi na hata vipato vya watu.
Pamoja na kwamba taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na kusainiwa na Sheiba Bulu ambaye ni Kaimu Mkurugenzi-Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, mbali na kukana taarifa za EU kukusudia kuifutia Tanzania misaada ilisisitiza kuwa kikao kilichojadili masuala hayo ni utaratibu wa kawaida.
Hata hivyo Taarifa hiyo ya Mambo ya Nje haikufafanua lolote kuhusiana na hoja ya fedha zilizotolewa na EU kwa ajili ya kukabiliana na corona au uvunjifu wa haki za binadamu uliojadiliwa katika kamati hiyo.
Zaidi taarifa hiyo ilihakikishia umma kwamba uhusiano kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya ni mzuri na kwamba unazidi kuimarika na wanashirikiana katika maeneo mbalimbali ili kuleta maendeleo kwa pande zote mbili.
Dk. David McAllisster ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje wa Bunge hilo la EU alihoji vigezo vilvyoitumiwa na uongozi wa EU kutoa msaada kwa Tanzania ambayo ameituhumu kwa kutokuwa wazi juu ya taarifa za corona na kutofuata miongozo ya Shirika la Afya Duniani (WHO).
Mwenyekiti huyo pia aligusia juu ya kuminywa kwa haki za binadamu na kutaka EU na washirika wake wahakikishe watetezi wa haki za binadamu wanalindwa Tanzania.
Tumekuwa tukiandika na leo tunarudia tena kushauri kwamba kama taifa linahitaji kuponya vidonda vinavyoisumbua ikiwamo vile vilivyotokana na uchaguzi mkuu.
Kama taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ilivyoeleza kwamba hatua ya EU kujadili hayo ni utaratibu wa kawaida wa kufanya tathimini kwa nchi washirika zake ambazo zimetoka kwenye uchaguzi, sisi pia kama taifa ilipaswa tathimini ifanyike na viongozi kuangalia naona ya kutibu majeraha.
Sisi tunadhani hilo lingefanyika mapema hata EU wasingepata nafasi ya kujadili hoja zilizojadiliwa sasa.
Pamoja na kwamba siku zote tumekuwa tukisisitiza suala la kutenda haki na kutimiza wajibu, pia tumekuwa tukishauri sualala kuendelea kujenga umoja wa kitaifa ili wale waliochaguliwa waweze kuongoza sawasawa.
Tuliandika na leo tunarudia tena kusisitiza kujenga umoja wa kitaifa kwa sababu kabla na baada ya uchaguzi kumekuwa na manung’uniko kila mahali.
from Author
Post a Comment