Na MWANDISHI WETU
KWA kutambua mchango wa sekta ya mifugo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi iliamua kuwekeza katika mashamba ili kuyapa uwezo wa kuzalisha mifugo bora itakayosaidia kukuza kipato cha taifa na wananchi kwa ujumla.
Ngerengere ni miongoni mwa mashamba matano ya Serikali yaliyo chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi lililopo Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro mkoani Morogoro.
Historia ya Shamba
Meneja wa Shamba la Serikali (LMU) Ngerengere, Saita Ole Kimosa anasema shamba hilo lilianzishwa mwaka 1975 kama shamba la ng’ombe wa maziwa ambalo kabla lilifahamika kama Dairly Farm Company lililokuwa chini ya watu binafsi na baadaye kufilisika na kubadilishwa jina na kuitwa LMU, mwaka 2004 chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi.
Anasema lengo la kuanzishwa kwa shamba hilo kuwa ni pamoja na kuzalisha mifugo bora yenye tija na kuuziwa wananchi kwa bei ambayo ni rafiki na kujiingizia kipato na kusaidia wananchi kupata mbegu bora za mifugo.
Saita anasema hadi Mei, mwaka huu shamba hilo lilikuwa na mifugo mbalimbali ikiwamo ng’ombe 771, mbuzi 234, nguruwe 201 na limekuwa na uzalishaji mzuri, pia anasema kuwa aina ya mifugo iliyopo kuwa ni ng’ombe aina ya borani, fresian na chotara, kwa upande wa mbuzi anataja aina ya boa ambayo asili yake ni Afrika ya Kusini na nguruwe aina ya landress na large white.
Mafanikio
Akizungumzia mafanikio ya shamba hilo ambalo lina mifugo takribani 1,206, anasema shamba hilo limefanikiwa kuzalisha mifugo mingi na kuisambaza kwa kuwauzia wafugaji wadogo wadogo kwa bei ambayo ni rafiki mikoa ya Morogoro na Dar es Salaam.
Anasema shambani hapo kuna mifugo ya aina tatu ikiwa ni ng’ombe, mbuzi na nguruwe ambayo yote inauzwa kwa wanachi kwa bei rafiki ili kusaidia wananchi kupata mbegu bora za mifugo.
Kimosa anaendelea kufafanua kuwa, kila aina ya mfugo uliopo shambani hapo kwa kusema, wana ng’ombe aina ya borani, frishian na chotara na kusema kuwa chotara wanapatikana kwa kupandisha borani na freshian na kuongeza kuwa chotara wanaopatikana hapo wana sifa ya kutoa maziwa mengi.
Aidha, kuna mbuzi aina ya bora asili yake ikiwa ni Afrika ya Kusini, ni mbuzi wa nyama na wanatumika kama mbegu kwa wafugaji na wanaweza kupandishwa na mbuzi wa kienyeji na kupata chotara wazuri na wanaokua haraka sana.
“Pia kuna nguruwe aina ya largewhite na landres ambao wanatumika kwa lengo la kuuzwa kwa wananchi kwa ajili ya mbegu bora,” anasema Kimosa.
Mchango kwa jamii
Kwa upande wa mchango, Kimosa anasema kuwa wameweza kuwapatia wafugaji mitambo bora kwa bei nafuu, baadhi ya wananchi kupata ajira ndani ya shamba la hilo la serikali, kuwauzia maziwa wananchi wanaozunguka shamba hilo pamoja na kuwapa masai kwa ajili ya kulimia.
Pia, wafugaji wananufaika kwa kupata tiba ya mifugo na ushauri kutoka kwa wataalam wa shamba la mifugo la serikali la Ngerengere.
“Wananchi wanahamasishwa kutenga mifugo yao na kufanya uhimilishaji kwa mifugo hiyo pamoja na kuuziwa madume bora ili kuboresha ng’ombe wa asili na kuwauzia chotara.
“Kipindi cha kiangazi kuna lambo linafahamika kama Mkobora limetengwa kwa ajili ya wananchi kunyweshea mifugo yao ili kusaidia ng’ombe na mifugo mingine isife kwa kukosa maji maeneo hayo,” anasema Kimosa.
Changamoto.
Kimosa anabainisha changamoto ambazo zinakabili shamba hilo ikiwemo miundombinu mibovu pamoja uchakavu wa vitendea kazi ambavyo hupelekea kushindwa kutimiza baadhi ya majukumu ya kila siku na kutoka eneo moja kwenda lingine kutokana na ubovu au kutokuwepo kabisa kwa usafiri.
“Kipindi cha doria wananchi hukasirishwa na wakati mwingine kuamua kuchoma moto baadhi ya maeneo ya shamba hili, pia kuna uvamizi mdogo sana wa wafugaji kuigiza mifugo na kulisha ndani ya shamba na kutoka,” anasema Kimosa.
Mikakati
Kwa upande wa mikakati, Kimosa anasema wanatarajia kila mwaka kufanya uzalishaji mkubwa wa mifugo wauze na kupata hela kwa ajili ya kurekebisha miundombinu ya shamba na kutatua changamoto zilizo ndani ya uwezo wao.
Wito kwa wadau
Kimosa anatoa wito kwa wadau wa mifugo, kwa kusema kuwa mifugo ni rasilimali inayotoa ajira na ni malighafi ya viwanda, hivyo wananchi watumie malighafi hizo vizuri.
“Ni vyema wafugaji kutibu mifugo yao kwa wakati ili kuepusha magonjwa yasiyo ya lazima kwa wanyama na kuogesha angalau mara moja kwa wiki pamoja na kuchanja kwa wakati.
“Pia wajitahidi kufuga kisasa kisasa na kwa tija kwani mifugo ndio ajira yenyewe, kuchagua mifugo iliyo bora kuitunza na kutunza pia ngozi kwani kila kilichopo kwa ng’ombe ni mali pamoja na kuhimilisha mifugo yao ili kupata koo tofauti, na kuepuka kudumaza mifugo kwa kuwa na koo moja inayozunguka kwenye boma.
“Hii husaidia kupata mifugo bora na mizuri zaidi,” anasema Kimosa.
Kifuto Kimanga, ni mkazi na mfugaji wa Kiwege, amabaye anasema kwa muda mrefu amekuwa akifanya ufugaji wa kuhamahama ambao ulisababisha yeye na familia yake kutokuwa na makazi maalumu maana kila siku wapo barabarani kutafuta maeneo ya kulishia mifugo yake na wakati mwingine kuingia kwenye migogoro na watumiaji wengine wa ardhi kutokana na mifugo kufanya uharibifu.
“Nimeamua kuachana na adha ya kuhamahama na kuamua kutafuta eneo la kudumu kwa ajili ya makazi na kufanya ufugaji wa kisasa ambapo shamba la LMU Ngerengere limenisaidia kupata mbegu bora za mifugo na za kisasa,” Kimanga.
Kimanga anasema kuwa uwepo wa shamba hilo umewasaidia wafugaji kupata mbegu bora za mifugo kama ng’ombe, mbuzi na nguruwe kwa bei nzuri na mifugo hiyo inakuwa haraka, nyama nyingi na maziwa mengi.
“Kutokana na uwepo wa shamba hili tunapata msaada wa kitabibu kwa mifugo yetu kutoka kwa wataalam wa mifugo waliopo shambani hapo na elimu juu ya utunzaji bora wa mifugo yetu,” anasema Kimanga.
Aidha,Kimanga anaeleza kuwa, mafanikio aliyopata kutokana na ufugaji bora na wa kisasa kwani mwaka 2013 ameweza kujenga nyumba kubwa ya kisasa yenye uwezo wa kubeba watu 24 inayokidhi haja zao na kuweza kupeleka watoto shule nzuri na za kisasa.
Hata hivyo ameendelea kufaidika na mifugo hiyo kwani ameweza kuzalisha mbuzi kwawingi na kuiuza kwa bei inayompa faida ambapo hapo awali alinunua mbuzi kwenye shamba la LMU Ngerengere kwa bei nafuu sana kwa dume moja alinunua Sh 150,000 na kwa sasa yeye anauza kuanzia Sh 250,000 – 300,000 kwa mbuzi mmoja ambapo anapata faida kubwa na ya kutosha kwa kuendesha maisha yake ya kila siku na kufanya maendeleo.
“Mbuzi hawa ni wakubwa sana, wanakuwa kwa haraka na wana nyama nyingi sana pia hawana tofauti na mbuzi wa Tanzania wa asili zaidi sana ni kuzingatia matunzo,chanjo, dawa za minyoo na chakula cha kutosha chenye virutubisho vyote kwa mifugo.
“Kwa upande wa ng’ombe wanatoa maziwa kwa wingi kwa kutoa kuanzia lita 14 kwa siku kila mmoja, pia wana nyama nyingi pindi wanapochinjwa,” anasema Kimanga.
Kimanga anaongeza kuwa wanawapa matunzo mazuri kwa kuzingatia kuwachanjo kwa wakati, na kutoa huduma zote za matibabu kwa wakati ili kuepuka kupoteza ng’ombe kwa magonjwa yasiyo ya lazima.
Pia, Esther Kilinga mfugaji wa Kiwenge jirani na shamba la LMU Ngerengere, anasema namna alivyonufaika, ambapo ameweza kujipatia madume kutoka shambani hapo na kwa sasa ana jumla ya ng’ombe 200 na kutokana na mifugo hiyo amefanikiwa kujenga nyumba ya kisasa ya kuishi, nyumba za wageni (gesti) zinazowaingizia kipato na kuweza kuendesha maisha yao ya kila siku.
“Pia tumeweza kujenga kanisa na kuwasomesha watoto kwenye shule nzuri na za kisasa.
“Lakini pia nauza maziwa, samli na mifugo iliyo hai kwa wanakijiji wa Ngerengere na maeneo jirani na hii hupelekea kunufaika na ufugaji wangu na kuweza kuchangia pato la Taifa,” anasema Esther.
Aidha, mfugaji mdogo, Athumani Ramadhani anasema kuwa alianza ufugaji mwaka 2018 akiwa na ng’ombe watatu na kufika sasa amefikisha ng’ombe 10 na kuainisha faida alizozipata kutokana na ngombe hao kuwa ni pamoja na kujenga nyumba ya kisasa, kukidhi maitaji ya familia yake ambapo awali hali ilikuwa mbaya.
Aidha, Athumani anashukuru uwepo wa shamba la LMU Ngerengere kwani limeweza kuwasaidia wafugaji wengi kupata mbegu bora za mifugo inayowasaidia kuzalisha kwa wingi na kufundishwa kanuni za ufugaji bora na tiba kwa mifugo yao na kuweza kupata lita nane za maziwa kwa ng’ombe mmoja kwa siku.
“Ombi langu kwa Serikali itusaidie kutujengea josho wafugaji wa majumbani kwani kwa kutumia solo kwa ng’ombe wengi ni kazi ngumu kidogo, kwani pia dawa haiwafikii vizuri na wakati mwingine mifugo mingine hukwepa dawa hivyo kutofanikisha lengo la kuogesha.
“Pia nawashauri wafugaji wengine kutumia vizuri shamba la LMU Ngerengere kwani lipo kwa ajili yao na watapata mifugo bora na mizuri sana inayotoa maziwa lita nane kwa siku kwani kama tunavyotambua kuwa ng’ombe ni mali,” anasema Ramadhani.
Ramadhani nahitimisha kwa kusema kwua anawashauri wafugaji wenzake kufuga mifugo michache na yenye tija kuliko kulundika mifugo mingi ambayo haipati huduma nzuri na chakula na pia kutafuta maeneo ya kufugia na kuacha ufugaji wa kuhamahama kwani pia uharibu mazingira na kusababisha migogoro kati yao na watumiaji wengine wa ardhi.
from Author
Post a Comment