DKT. NDUGULILE AIPA SIKU 90 SHIRIKA LA POSTA KUBORESHA UTENDAJI NA UFANISI WAKE |Shamteeblog.

 Posta Masta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania, Hassan Mwang’ombe akitoa maelezo kwa Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile (wa kwanza kulia) kuhusu utendaji kazi wa kamera maalumu zinazofuatilia usalama wa ofisi za Posta, Dar es Salaam

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile (aliyenyoosha kidole) akihoji utendaji kazi wa skana ya kukagua usalama wa vifurushi na vipeto vinavyoingia na kutoka nchini katika ziara yake ya kutembelea Shirika la Posta Tanzania, Dar es Salaam.

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile akizungumza na menejimenti ya Shirika la Posta Tanzania wakati wa ziara yake kwenye Shirika hilo, Dar es Salaam. Katikati anayesikiliza ni Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika hilo ni Kanali mstaafu Dkt. Haruni Kondo.


  • Aitaka iongeze matumizi ya mifumo ya TEHAMA kuhudumia wananchi

  • Aikumbusha kutumia vizuri rasilimali zake kuongeza mapato ya Shirika


Na Prisca Ulomi, WMTH

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile ameipa siku 90 Shirika la Posta Tanzania (TPC) kuboresha utendaji kazi na ufanisi katika kuhudumia wateja na wananchi kwa ujumla katika shughuli za kila siku za uendeshaji wa Shirika hilo


Dkt.Ndugulile ameyasema hayo kwa Bodi, Menejimenti na wafanyakazi wa Shirika la Posta Tanzania wakati wa ziara yake ya kutembelea Shirika hilo, Dar es Salaam ambapo aliambatana na Naibu Waziri wake, Mhandisi Kundo A. Mathew, Katibu Mkuu, Dkt. Zainab Chaula na Menejimenti ya Wizara hiyo kwa lengo la kufahamu utendaji kazi wa Shirika ili kuhakikisha kuwa linahudumia vema wananchi


Ameongeza kuwa TPC ipitie mikataba yake ambayo haina maslahi kwa Shirika na isimamie vizuri rasilimali zake ikiwemo viwanja, ofisi na magari kwa kuwa rasilimali ni mtaji na mtaji sio fedha ili rasilimali hizo zitumike kuongeza mapato ya Shirika


Vile vile ameiagiza  Wizara yake kushirikiana na TPC kufanya mapitio ya sera na sheria ya posta ili ziweke kuendana na wakati kuendana na mabadiliko ya teknolojia duniani ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi


Pia, amewakumbusha kuwa na mahusiano mazuri baina ya viongozi, wafanyakazi, menejimenti na wajumbe wa bodi katika mazingira ya mahali pa kazi ili kuboresha na kuongeza utendaji kazi wa Shirika


Naye Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mhandisi Kundo A. Mathew amelipongeza TPC kwa kutengeneza Mfumo wa Taarifa wa Posta ambao unasimamia na kufuatilia uendeshaji wa Shirika; malipo na ukusanyaji wa mapato; na taarifa za watumishi


Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Zainab Chaula, ameueleza uongozi wa TPC kuwa Wizara itaendelea kushirikiana nao ili kufanikisha utendaji kazi wa Shirika katika kuhudumia wateja


Mwenyekiti wa Bodi wa TPC, Kanali mstaafu, Dkt. Haruni Kondo na Posta Masta Mkuu wake, Hassan Mwang’ombe wamemshukuru Dkt. Ndugulile kwa ziara yake na kulitaka Shirika liboreshe utendaji kazi wake na wako tayari kufanyia kazi yaliyoelekezwa 


Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari



By Mpekuzi

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post