Mwanamuziki nyota wa Tanzania maarufu kama Diamond Platnumz, ameweka bayana ukweli kuhusu baba yake mzazi.
Akizungumza katika mahojiano na Wasafi Radio,jana Diamond amesema licha ya kuishi vizuri na mzee Abdul ambaye awali alifahamika kama baba yake, lakini mwaka 2000 aligundua kuwa baba yake mzazi ni mzee Nyange ambaye kwa sasa ni marehemu.
''Nikiwa na kama miaka 11 hivi niliambiwa na mmoja wa majirani zangu kwamba nenda pale kwenye soko la Tandale, halafu muulizie Salum Bubu au Iddi Nyange, nikafika akanipa shilingi mia mbili na mchele, kwa sababu alikua anauza mchele wa ujumla'',alisema Diamond.
''Mwanzoni nilikuwa naona utofauti kwenye vitu vingi, lakini sikuweza kuelewa baadhi ya vitu kwa sababu ya utoto'' ,aliongeza Diamond.
Katika maelezo yake leo, Diamond amesema alilitambua suala hilo tangu mwaka 2000 baada ya mama mzazi wa msanii Rommy Jones ambaye pia ni ndugu yake kumuelekeza kuhusu Salum Nyange.
“Alinieleza kuwa kipindi hicho baba alikuwa anauza mchele katika soko la Tandale. Nilipofika Tandale sokoni nilionana naye na kumueleza kwamba nimeelekezwa kuwa yeye ni baba yangu akanipa mchele na Sh200, ule mchele niliupeleka nyumbani.”
“Kipindi hicho hawakuwa na ukaribu na mama yangu hivyo ukawa ndio utaratibu wangu naenda kila mara kumuona hali iliyopelekea yeye na mama wakarudisha mahusiano,” amesema Diamond.
Katika maelezo yake msanii huyo anayewania tuzo za MTV Mama mwaka 2021 amesema alipelekwa Kariakoo na kukutana na ndugu zake wengine akiwemo Ricardo na Iddy Santus na waliishi kwa upendo.
“Tukawa na upendo wa ajabu..., tangu kipindi hicho nikawa sikai tena Tandale nikawa nakimbilia Kariakoo. Ila kipindi hicho chote nilikuwa sina uhakika familia yangu halisi ni ipi,” amesema Diamond.
Amesema alipokuwa mkubwa alibaini kuwa wale ni ndugu zake kwa kuwa walikuwa wakiendana na kubainisha kuwa hakuwahi kuishi na msanii Queen Darlin ambaye ni mtoto wa mzee Abdul.
“Miezi minne iliyopita ndiyo nilizungumza na mama yangu kuhusu hili jambo na kupata uhakika kuwa baba yangu mzazi ni nani baada ya kuangalia tena zile picha za mzee wangu.”
“Kuna kipindi mzee Abdul alikuwa anaumwa na nilikuwa nikienda kumsalimia lakini mama yake (mzee Abdul) alikuwa ananifukuza. Kuna siku nilikwenda na Queen Darlin akatuambia tumetumwa na mama zetu kwenda kumchora tukidhani atakufa turithi mali. Nikawa nawaza mbona yanatokea hayo lakini upande ule mwingine (wa Nyange) wananipenda na mwanzoni hilo lilikuwa linanisumbua sana,” amesema.
Amedai licha ya mzee Abdul kutokuwa naye karibu hakikumzuia kumsaidia jambo ambalo mama Dangote hakulipenda kwa madai kuwa mzee huyo alikuwa anamzungumzia vibaya Diamond kwenye vyombo vya habari.
Siku ambayo mama Dangote alieleza kuhusu baba yake Diamond, mzee Abdul alihojiwa na televisheni mbalimbali na kusema kuwa kama jambo hilo limezungumzwa na mama Dangote, yeye hana cha kuongeza licha ya awali kupinga kwamba yeye si baba wa Diamond.
Takribani wiki mbili zilizopita, kulikuwa na gumzo mtandaoni kuhusu baba aliyefahamika kama mzazi wake Diamond kuwa si baba halisi wa mwanamuziki huyo.
Gumzo hilo lilianza mara baada ya mama yake Diamond kuongea kwenye radio kuwa baba ambaye anadai Diamond amemtelekeza si baba wa kumzaa, baba yake Diamond ni marehemu na alikuwa anaitwa Nyange na si Abdul.
Mama huyo aliweka picha ya Diamond ikiwa pamoja na Nyange, kuonesha jinsi wanavyofanana.
Hatua hiyo imeendelea kuzua mijadala katika mitandao ya kijamii nchini humo, haswa baada ya baba anayedai kuwa ndiye mzazi wake ''Abdul'' kutoridhishwa na tukio hilo kwa madai ya kwamba aliukataa ujauzito.
''Kama niliukataa ujauzito, iweje nimlee Diamond miaka yote hiyo? alihoji Mzee Abdul ambaye alimlea Diamond tokea akiwa mdogo na watu wengi kudhani kuwa ndiye baba yake mzazi.
By Mpekuzi
Post a Comment