HOFU YATANDA KWA WATOTO WANAOISHI NA KUFANYA KAZI MTAANI |Shamteeblog.

Na Avila Kakingo, Globu ya jamii
HOFU yatanda kwa watoto wanaoishi na kufanya kazi mtaani katika stendi kuu ya mabasi yakwenda Mikoani ya Ubungo jijini Dar es Salaam baada ya kusikia kuwa itahamia Mbezi Luis.

Emmanuel Frenk miaka 13 Kutoka jijini Mwanza (Sio jina halisi) akizungumza na Michuzi Blog amesema kuwa amekuwa na wasiwasi juu ya kituo cha mabasi ya kwenda mikoani kuhamia mbezi kwani anahofia hawataruhusiwa kufanya kazi zao zinazowaingizia kipato kama ilivyo kwa sasa katika kituo cha Ubungo.

"Kule mbezi kutakuwa na mazingira magumu kujipati liziki sisi watoto tunaofanya kazi katika stendi hii ya Ubungo, kule mbezi sipaelewi kabisa patakuwa mazingira mageni, ulinzi tofauti na viongozi watakuwa wengine sijui itakuwaje na sasa tushapazoea ubungo." Amesema Emmanuel

Amesema kuwa aliondoka nyumbani kwao jijini Mwaza mara baada ya kuona maisha magumu ya kuishi yeye na kaka zake nyumbani bila ya wazazi ingawa wazazi wao wapo lakini wametengana na kuwaacha watoto nyumbani peke yao bila mwangalizi.

Amesema kuwa kutengana kwa wazazi wao ndio chanzo cha yeye kuanza kutafuta kazi ndogondogo katika stendi ya mabasi ya Nyegezi jijini Mwanza na baadae kuondoka na kufika Ubungo jijini Dar es Salaam.

Amesema kuwa nyumbani kwao wapo watoto wengi sana na yeye ndio wamwisho na waliofanikiwa kusoma ni watoto wanne tu lakini wengine waliobaki hawajasoma, yeye akiwa mmoja wapo. Akiwa hapo nyumbani ilifika wakati wanakosa mahitaji mhimu ndipo aliamua kwenda stendi ya mabasi Nyegezi kutafuta chakula.

*Alifikaje fikaje jijini Dar es Salaam
Emmanuel amesema kuwa jijini Dar es Salaam alifika kwa kujificha kwenye uti wa gari (Chesesi) akiwa na lengo kuwa jijini Dar es Salaam ndiko kunamaisha mazuri zaidi na hana ndugu yeyote ndipo alipondondokea kufanya kazi ndogo ndogoo katika stendi ya Ubungo.

"Siku moja nikaona niondoke nyumbani niende pale stendi ya Nyegezi nikaanangalie hata chakula halafu nirudi lakini nilivyoenda ndio nikawa nimepata kishawishi moja kwa moja na ndio nikakutana na wenzangu nikajiunga nao, nimekaa hapo Nyegezi kama miezi mitano ndio nikapata rafiki yangu mmoja akaniambia tuje huku Dar es Salaam kwa kuzamia chini ya gari (Chesesi) ndio tukaja mpaka huku ndani." Ameelezea Emmanuel

Hata hivyo Emanuel amesema kuwa alikutana na watoto wengine ambao anafahamiana nao na kumwambia kuwa kuna kituo cha Babawatoto ambacho kinatoa huduma ya chai, chakula cha mchana, sehemu ya kufua nguo pamoja na kutoa mafunzo.

Katika kutekeleza mradi wa USAID-Kizazi Kipya ambao unatekelezwa na Railway Children Africa kwa kushirikiana na taasisi ya Babawatoto wameweza kusaidia watoto wanaoishi na kufanya kazi mtaani kwa kuwapa bima za afya, kupima afya zao, kuwapa msaada wa kisheria bure pamoja na kuwasimamia umezaji wa dawa.

Akizungumza na Michuzi Blog Afisa Mawasiliano wa Railway Children Africa, Henry Mazunda amesema kuwa watoto wengi wanatoroka nyumbani kwao kutokana na sababu mbalimbali hasa wazazi kutengana, unyanyasaji, kukosa mahitaji muhimu pamoja na ukatili unaofanyika katika ngazi ya familia na jamii.

"Ukiwaangalia watoto wale ni watoto kama watoto wengine, wanahitaji kupendwa na kulindwa kama watoto wengine na ni wajibu wetu sisi sote kuhakikisha watoto wote wakiwemo watoto wanaoishi na kufanya kazi mtaani wanawezeshwa ili watimize ndoto zao." Amesema Mazunda

Amesema kuwa Railway Children Africa kwa kushirikiana na wadau wengine ikiwemo taasisi ya Babawatoto wanawawezesha watoto hao kutimiza ndoto zao kwani wengine wanataka kurudi shule, wanataka kujifunza vitu mbalimbali, kupata huduma za afya na chakula.

Kwaupande wake Mratibu wa Mradi katika Taasisi ya Babawatoto, Johnson Mtango amesema kuwa katika kituo cha muda (drop-in Centre) kilichopo Mburahati jijini Dar es Salaam wanahudumia watoto zaidi ya 25 kwa siku kwa kuwapatia mahitaji muhimu na kuwasaidia waweze kutimiza ndoto zao. Ikiwa watoto hao wamepangwa katika makundi mawili tofauti.

Katika Makundi hayo wapo watoto wanaojiandaa kwenda kupata mafunzo ya ufundi katika Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) pamoja na wale wanaojifunza kusoma na kuandika kituoni hapo.

Uhalisia katika kituo cha Babawatoto kilichopo Mburahati jijini Dar es Salaam kinapokea watoto wanaofanya kazi mtaani kwaajili ya kuwapa mahitaji muhimu hasa chai ya asubuhi, chakula cha Mchana pamoja na kufua nguo zao wawapo kituoni hapo.

Watoto hao mara baada ya kupata chakula cha Mchana ndipo huondoka kituoni hapo na kuelekea sehemu zao wanazofanya kazi ndogondogo pasi na kujua hatima yao huko waendako.

Kwa upande wake Afisa Ustawi wa Jamii wa Stendi ya Mabasi ya Ubungo, Grace Kasusa amesema kuwa wao kama serikali wanashirikiana na taasisi ya Babawatoto ili kuhakikisha watoto wanaofanya kazi ndogo ndogo mtaani wanapata haki zao.

Amesema kuwa watoto hao huwapata kutokana na kuwaona katika kituo cha ubungo na kuwashauri kurudi nyumbani kwao.

"Sisi tukishirikiana na Taasisi ya Babawatoto tunawakusanya watoto wanaofanya kazi ndogo ndogo hasa kituo cha mabasi cha Ubungo na kuwashauri kurudi nyumbani, wengine hukubali na wengine hukataa kwani wanaamini watafanikiwa katika katika kufanya kazi hizo." Amesema Grace.

Mikoa ya mwanza, Mbeya, Mara na Singida inaongoza kwa watoto wanaotoroka katika familia zao na kukimbilia jijini Dar es Salaam kwaajili ya kufanya kazi ndogondogo hasa katika Stendi ya mabasi ya Ubungo.

Amesema kuwa kwa wastani wanapokea watoto atatu hadi watano kwa wiki wa umri wa miaka 10 hadi 17.

"Sisi tukiwapata watoto tunawaunganisha moja kwa moja na taasisi ya baba watoto ili wapewe ushauri kwa haraka kwani wakiwa bado wageni ni rahisi kurudi kwao kuliko wale waliozoea katika mazingira ya mtaani." Amesema Grace.


By Mpekuzi

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post