Na Immaculate Makilika- MAELEZO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amekitaka kiwanda cha mpunga kinachozalisha bidhaa za Korie kuwa na bidhaa zenye jina la kitanzania ili zisaidie kuitangaza nchi kimataifa.
Rais Magufuli ameyasema hayo leo mkoani Morogoro wakati akifungua kiwanda cha Kukoboa Mpunga cha Murzar Wilmar Mill, kilichopo Kihonda mkoani Morogoro.
“Natoa rai kwa muwekezaji kutengeneza bidhaa zenye jina linalohusu nchi yetu kwa sababu Tanzania tumekuwa tukizalisha vitu vingi lakini hatutangazi nchi yetu. Siwazuii kuendelea na jina la Korie lakini kuwe na jina jingine linalotangaza nchi”, alisema Rais Magufuli.
Aidha, Rais Magufuli alisema kuwa bila kuwa na viwanda hakuna uchumi, viwanda ndio sehemu pekee inayotengeneza ajira za watanzania, na kuwa alipoingia madarakani aliamua kuhakikisha kuwa katika kipindi cha miaka mitano Serikali inajenga jumla ya viwanda 8,477, sambamba kufikia azma yake ya kutengeneza ajira milioni 8.
“Natoa wito kwa wizara zote zinazohusika na uwekezaji zishirikiane katika kuhamasisha ujenzi wa viwanda na kuleta wawekezaji wa kutosha, watanzania kuwekeza hakuhitaji fedha nyingi, tuzitumie taasisi zetu za fedha katika kuanzisha viwanda”, alisisitiza Rais Magufuli.
Vilevile Rais Magufuli alimpongeza mwekezaji wa kiwanda hicho kwa kutoa ajira za moja kwa moja 75,000 na ajira nyingine zisizo za moja kwa moja kwa wakulima, na kuongeza kuwa Tanzania ni mahali pazuri kwa ajili ya kuwekeza na kuwa huu ni mwelekeo muafaka wa kuingia uchumi wa kati.
Naye, Afisa Tawala wa Kiwanda hicho, Martha David alisema kuwa kiwanda hicho kilichojengwa kwa gharama ya dola milioni 21, kina uwezo wa kukoboa mpunga tani 288 kwa siku, na bidhaa zake zinazozalishwa zinauzwa nchini pamoja na nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
“Katika mwaka wa mazao 2020, kampuni ilipokea zaidi ya tani 65,000 za mpunga kutoka mikoa mbalimbali, pia tumetengeneza ajira za moja kwa moja kwa wananchi 75,000 na zisizo rasmi 250”, alisema Martha.
By Mpekuzi
Post a Comment