Na.Charles James,Michuzi
Askofu Mkuu wa Kanisa la Evangelistic Assemblies of God Tanzania (EAGT) Dkt. Brown Abel Mwakipesile amesimikwa rasmi hii leo Februari 12, 2021 ili kuliongoza kanisa hilo kwa miaka mitano tena mara baada ya kuchaguliwa mwishoni mwa mwaka jana kwa nafasi hiyo pamoja na wasaidizi wake.
Askofu Mwakipesile amekuwa kiongozi wa nafasi hiyo tangu mwaka 2016 ambapo alichaguliwa na kupewa nafasi hiyo ya kuliongoza kanisa hilo kwa weledi na uadilifu ili kuyafikia malengo yake.
Aidha kwa mujibu wa miongozo ya kanisa hilo, uchaguzi mkuu wa kumpata Askofu Mkuu, Makamu Askofu Mkuu, Katibu Mkuu, Mhazini Mkuu pamoja na Mshauri wa kanisa hilo hufanyika kila baada ya miaka mitano.
Halfa ya kumsimika ilifanyika katika kanisa la EAGT Mlimwa West lililopo eneo la Maili Mbili Dodoma huku mgeni rasmi akiwa Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu wa Makanisa ya Kipentekoste (CPCT) Bw. Peter Nkonki.
Akizungumza wakati wa Hafla ya kumsimika askofu huyo, Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu wa Makanisa ya Kipentekoste, Bw.Peter Nkonki alieleza furaha yake kwa namna kanisa lilivyoweza kujisimamia vyema na kuhakikisha linapata viongozo wake katika ngazi ya taifa kwa njia ya haki kama taratibu za kanisa zinavyoeleza.
“Mmejipatia kiongozi mwenye sifa zote muhimu ikiwemo; ushujaa, umahili, uchapa kazi, mwenye uadilifu pamoja na hofu ya Mungu ambaye tunaamini ni Mungu amemteua ili kulisaidia kanisa kwa miaka mitano tena,”alisema Nkonki.
Alieleza kanisa lina kila sababu za kuendelea kumshukuu Mungu kwa kuwapatia viongozi wenye hofu ya Mungu kwa makusudi ya kiroho pamoja na masuala ya kijamii ili kuwa na taifa lenye watu wanaoishi kwa kumtegemea Mungu na kufanya kazi kwa bidii ili kujipatia maendeleo yao.
Aidha alilitaka kanisa hilo kuendelea kumuombea, kumtia moyo na kumkubali ili yale anayopaswa kuyatekeleza yazae matunda.
“Niwaeleze mambo muhimu matatu ambayo ni muhimu kuyafahamu kuhusu uwepo wa askofu huyu, moja ni kumkubali, kumuombea na kumtia moyo ,”alisema Nkonki
Pia alitumia fursa hiyo kuendelea kuwaasa wanajamii kuhakikisha wanaendelea kuiombea nchi ili Mungu aiepushe na uwepo wa majanga mbalimbali ikiwemo magonjwa kama Corona.
“Kanisa ni lazima lisimame katika nafasi yake kuliombea Taifa ili Mungu aturehemu na kuiponya nchi yetu na gonjwa hili la corona, maana yeye hakuna linalomshinda,” alisisitiza
Aidha alipongeza jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa hatua anazozichukua za kiimani kuwataka Watanzania kuendelea kuomba kwa bidii kila wakati.
“Kwa sababu Mungu anaheshimu na kujali kauli ya Kiongozi Mkuu wa nchi, hivyo tuungane naye na kuendelea kuomba kwa ajili ya Taifa huku tukizingatia taarifa zinazotolewa na Wizara ya Afya,”alieleza.
Naye Askofu Mkuu wa Kanisa la EAGT Dkt. Mwakipesile akihutubia wakati wa hafla hiyo alieleza furaha yake kwa namna Mungu alivyoendelea kuilinda na kuiponya nchi yetu pamoja na kulifikisha taifa katika uchumi wa kati.
Aidha alieleza, kanisa lake litaendelea kuunga mkono jitihada hizo kwa kuzingatia tayari kanisa linatekeleza Mpango Mkakakti wa miaka 15 ambao unalenga kuinua kanisa na jamii kwa ujumla.
Askofu Mwakipesile alifafanua kuwa, kanisa lake litaendelea kuyafikia malengo yake muhimu ikiwemo la kuendelea kuihubiri injili kwa kila kiumbe ili jamii ibadilike na kuache uovu na kumrudia Mungu.
“Tunaamini kuwa, watu wakiacha maovu, nchi yetu itakuwa yenye amani na utulivu mkubwa, na kuisaidia Serikali kuondokana na gharama ya kushughulikia masuala hayo hivyo tutahakikisha tunayasimamia kwa nguvu zote na weledi wa hali ya juu ili kuwa na mchango chanya katika Taifa letu.
AWALI:
Kanisa la EAGT lilisajiliwa rasmi tarehe 18 Julai 1991 na Wizara ya Mambo ya Ndani Jijini Dar es Salaam chini ya uongozi wa aliyekuwa Askofu Mkuu wa kanisa hili, Mwinjilisti Dkt. Moses S. Kulola ambapo lililenga kueneza injili duniani kote. Tangu usajili 1991, EAGT imeenea mikoa yote kila wilaya ambapo hadi sasa lina zaidi ya makanisa 5,000 ya mahali pamoja kwa Tanzania Bara na Visiwani. Kanisa limefanikiwa pia kufungua makanisa nje ya nchi kama vile Malawi, Zambia na Msumbiji.
Askofu Mkuu wa Kanisa la EAGT Dkt. Brown Mwakipesile akihutubia wakati wa hafla hiyo.
Sehemu ya wachungaji waliohudhuria hafla hiyo wakifuatilia hotuba ya Askofu Mkuu wa Kanisa la EAGT Dkt. Brown Mwakipesile (hayupo pichani).
Askofu Mkuu wa Kanisa la EAGT Dkt. Brown Mwakipesile pamoja na viongizi wa kanisa hilo wakiombea nchi ya Tanzania kuendelea kuwa na amani na uponyaji wa Mungu katika mapito mbalimbali.
By Mpekuzi
Post a Comment