Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt Zainab Chaula akizungumza katika kikao cha wadau wataalamu wa mawasiliano na TEHAMA cha kujadili kuhusu miundombinu ya kimkakati ya mawasiliano kilichofanyika jijini Dodoma. Kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya TEHAMA wa Wizara hiyo Mulembwa Munaku.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt Jim Yonazi (Kulia) akizungumza katika kikao cha wadau wataalamu wa mawasiliano na TEHAMA kujadili kuhusu miundombinu ya kimkakati ya mawasiliano kilichofanyika jijini Dodoma anayefuatia ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt Zainab Chaula na Kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya TEHAMA wa Wizara hiyo Mulembwa Munaku
Mkurugenzi wa Idara ya TEHAMA wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mulembwa Munaku Mkuu wa Shirika la Mawasiliano akizungumza katika kikao cha wadau wataalamu wa mawasiliano na TEHAMA kujadili kuhusu miundombinu ya kimkakati ya mawasiliano kilichofanyika jijini Dodoma kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt Zainab Chaula
Mkurugenzi wa Kitengo cha Sheria Lugano Rwetaka (Kulia) akifuatiwa na Mkurugenzi wa Idara ya Utumishi Utawala Kitolina Kippa wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wakiwa katika kikao cha wadau wataalamu wa mawasiliano na TEHAMA kujadili kuhusu miundombinu ya kimkakati ya mawasiliano kilichofanyika jijini Dodoma
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt Zainab Chaula (waliokaa katikati) Kulia ni Naibu wake Dkt Jim Yonazi na Kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya TEHAMA wa Wizara hiyo Mulembwa Munaku wakiwa katika picha ya pamoja baadhi ya wadau wataalamu wa mawasiliano na TEHAMA waliokuwa katika kikao cha kujadili kuhusu miundombinu ya kimkakati ya mawasiliano kilichofanyika jijini Dodoma.
……………………………………………………………………………
Na Faraja Mpina – WMTH
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt Zainab Chaula amefungua kikao cha wadau wataalamu wa mawasiliano na TEHAMA kilichoitishwa na Wizara hiyo ili kujadili, kutoa maoni na ushauri juu ya namna bora ya kuboresha miundombinu ya kimkakati inayowezesha upatikanaji wa huduma ya mawasiliano nchini.
Akizungumza katika kikao cha wataalamu hao kilichofanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma, Dkt chaula amewaambia wataalamu hao kuhakikisha wanaibua hoja zenye tija zitakazoleta msingi wa kuboresha na kulinda miundombinu hiyo itakayosaidia kuinua uchumi wa nchi na kuongeza mchango wa Wizara kwenye Pato la Taifa.
Ameongeza kuwa miundombinu hiyo inawezesha upatikanaji wa fursa mbalimbali ikiwemo biashara mtandao na upatikanaji wa huduma mbalimbali za kijamii kupitia mifumo ya TEHAMA huku akizitaja changamoto zinazoambatana na fursa hizo ni pamoja na wizi, uhalifu wa njia ya mtandao na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii.
“Tumewaita hapa wadau wataalamu wa mawasiliano na TEHAMA kutoka katika taasisi za Serikali na binafsi ili watoe maoni na ushauri kwa Wizara ili kuisaidia Wizara pindi inapotengeneza sheria, kanuni, mifumo na miongozo mbalimbali iwe na majumuisho na michango ya wadau wataalamu katika maeneo hayo”, Dkt Chaula
Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt Jim Yonazi ametoa rai kwa wataalamu hao kutumia utaalamu wao wote kuhakikisha wanatoa mchango ambao utaifanya nchi ya Tanzania kuwa kinara wa miundombinu bora ya mawasiliano kuanzia katika ujenzi, uendelezaji na ulinzi wa miundombinu hiyo.
Aidha, ametoa maagizo kwa kikao hicho kuainisha wadau muhimu waliosahaulika kupewa mualiko wa kikao hicho ili waweze kushiriki katika kikao kijacho kwasababu ni muhimu sana kupata mchango wa wataalamu wote muhimu ili kuboresha miundombinu ya mawasiliano nchini.
Kwa upande wa Mkurugenzi wa TEHAMA wa Wizara hiyo, Mulembwa Munaku amesema miundombinu ya kimkakati ni ile inayosaidia matumizi ya TEHAMA nchini ambayo ikiharibika au kuhujumiwa inaathiri uchumi wa nchi, usalama na huduma za kijamii.
Amesema kuwa kikao hicho kinajadili vigezo vya miundombinu hiyo ili Wizara kuweka utaratibu wa kuiendeleza, kuilinda na kuiepusha na hujuma mbalimbali zinazofanyika katika miundombinu hiyo.
Naye Nkundwe Mosaga Mhadhiri kutoka Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam ambaye ni mtaalamu wa TEHAMA amesema kuwa mifumo ya TEHAMA ndio inayobeba maono na muelekeo wa nchi kwa kuchangia ukuaji wa uchumi na kutengeneza ajira kwa wananchi
Meneja wa miundombinu ya mawasiliano kutoka Kampuni ya simu ya Vodacom Michael Bujaga ameishukuru Wizara kuandaa kikao hicho ili kutafuta ufumbuzi kwenye masuala ya miundombinu hiyo inayonufaisha taasisi za mawasiliano, watumiaji wa huduma za mawasiliano na nchi kwa ujumla.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari
By Mpekuzi
Post a Comment