MBUNGE WA LUDEWA AUNGA MKONO JUHUDI ZA WANANCHI |Shamteeblog.

Na Shukrani Kawogo, Njombe.

Mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga ametoa mifuko ya saruji 100 pamoja na bati 200 kwaajili ya kuendeleza ujenzi wa kituo cha afya kilichopo katika kijiji cha Ludewa kijijini kata ya Ludewa mjini.

Akikabidhi vifaa hivyo mbunge huyo amempongeza diwani wa kata hiyo Monica Mchiro pamoja na viongozi wa ngazi ya kijiji kwa kuhamasisha wananchi kujenga kituo hicho mpaka walipofikia.
 Amesema ni wajibu wake kuunga mkono juhudi za wananchi kama mtanzania mzalendo na kwa nafasi ya ubunge aliyonayo anakila sababu ya kuambatana na wananchi katika kuleta maendeleo hivyo  bati  hizo zitatosheleza kuezeka jengo la utawala ambalo tayari limesha pauliwa na mifuko hiyo ya saruji itatumika kupiga lipu.

Aliongeza kuwa wananchi wanatumia nguvu nyingi katika ujenzi huu hivyo ili jaso lao lisipotee bure pamoja na kutoa mchango huo ataendelea kuchangia zaidi ili kuhakikisha kuwa kituo hicho kinamalizika na wananchi wanaanza kupata huduma stahiki.

"Hiki kituo kikimalizika kitakuwa ni msaada mkubwa sana kwa wakazi wa Ludewa kijijini kwani watakuwa wanapata huduma mbalimbali za afya ikiwemo ya upasuaji pasipo kwenda hospitali ya wilaya", alisema Kamonga.

Aidha kwa upande wa mwenyekiti wa halmashauri ya Ludewa ambaye pia ni diwani wa kata ya Mundindi Wise Mgina amempongeza mbunge huyo na kuwataka wananchi kutumia mifuko hiyo ya saruji kwa wakati kwakuwa endapo wataiacha kwa muda mrefu inaweza ikaharibika kwa kuganda.

Ameongeza kuwa wananchi hao wamefanya jitihada kubwa za ujenzi wa kituo hicho ambapo jitihada hizo ndizo zilizomgusa mbunge huyo kutoa mchango wake hivyo wananchi wanapaswa kuendeleza juhudi hizo ili kituo hicho kiweze kumalizika kwa wakati.Monica mchiro ni diwani wa kata hiyo amemshukuru mbunge huyo kwa mchango wake na kuahidi kuutumia vyema mchango huo.

Amesema kituo hicho bado kinahitaji majengo mengi ikiwemo jengo la upasuaji, kuhifadhia maiti na mengineyo kwani kwa sasa wamejenga jengo moja tu ambalo ni jengo la utawala na linagharimu kiasi cha shilingi milioni 65 ambapo kiasi hicho kitagharimu kwa majengo yote.

"Majengo yote yanayohitajika yanagharimu kiwango hicho cha fedha hivyo bado tunauhitaji mkubwa wa michango kutoka kwa wananchi, viongozi na wadau mbalimbali ili tuweze kukamilisha zahanati hii", alisema Mchiro.

 Naye mmoja wa wakazi wa kijiji hicho ambaye alizungumza kwa niaba ya wenzake Winifrid Mtewa amesema matunda ya mbunge huyo yameanza kuonekana mapema sana hivyo wanatumai kupata maendeo makubwa sana katika siku zijazo.

"Kwa sisi wakulima tukipanda mahindi halafu tukiona yametoa mbelewele nzuri basi huwa tunafurahia kwakuwa tunajua kwa dalili hizo ni ishara kwamba mahindi yatayobeba yatakuwa makubwa na yenye afya, hivyo mbunge wetu ni sawa na aina hiyo ya mahindi", alisema Mtewa.

Mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga (kulia) akimkabidhi mifuku 100 ya saruji diwani wa kata ya Ludewa mjini Monica Mchiro(kushoto)
Mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga akiongea na wananchi wa Ludewa kijijini (hawapo pichani) alipowasili kijijini hapo kwa lengo la kukabidhi mifuko 100 ya saruji pamoja na bati 200 kwaajili ya ujenzi wa zahanati. Kulia ni Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Ludewa Stanley Kolimba na Kushoto kwake ni katibu wa CCM wilaya Bakari Mfaume, Mwenyekiti wa halmashauri ya Ludewa ambaye pia ni diwani wa kata ya Mundindi Wise Mgina, Mwenyekiti wa wazazi CCM wilaya John Kiowi, diwani wa kata ya Ludende Vasco Mgimba.
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Ludewa ambaye pia ni diwani wa Mundindi Wise Mgina akiongea na wananchi wa kijiji cha Ludewa kijijini alipiambatana na mbunge kukabidhi mifuko 100 ya saruji pamoja na bati 200. Kulia kwake ni katibu wa CCM wilaya Bakari Mfaume, Kushoto kwake ni Mwenyekiti wa wazazi CCM wilaya John Kiowi na diwani wa Ludende Vasco Mgimba
Mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga (kushoto) akimkabidhi bati 100 diwani wa kata ya Ludewa mjini Monica Mchiro kwaajili ya ujenzi wa zahanati iliyopo katika kijiji cha Ludewa kijijini.
 


By Mpekuzi

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post