Wanafunzi wawili waliojulikana kwa majina ya Salome Joseph na Neema Kulwa ambao ni wa kidato cha pili katika shule ya Sekondari Makuru iliyopo kijiji cha Msemembo kata ya Makuru wilayani Manyoni mkoani Singida, wamefariki dunia.
Vifo hivyo vimetokea baada kuingiza ndani ya nyumba jiko la mkaa walilokuwa wakipikia hali inayosadikiwa kusababisha kifo chao kwa hewa nzito ya mkaa.
Hali ya majonzi imetawala kwa wakazi wa Kata hiyo ya Makuru kufuatia tukio hilo la kusikitisha kwa wanafunzi hao ambao ni wasichana waliokuwa wamepanga chumba ili kuendelea na masomo yao, wakitoka kijiji cha Hika.
Mwenyekiti wa kijiji cha Msemembo Onesmo Mwaja amesema chanzo cha tukio hilo ni kukosa hewa iliyosababishwa na moto wa jiko la mkaa walilokuwa wakitumia majira ya usiku.
Kwa upande wa Afisa Elimu Sekondari Halmashauri ya Manyoni Ramla Munisi, akizungumza na waombolezaji amesema idara yake itaanza ziara ya kutoa elimu kwa wanafunzi wanaoishi kwenye nyumba za kupanga.
Hata hivyo diwani wa kata hiyo ya Makuru Moses Matonya amehimiza kuanza ujenzi wa mabweni ili kuepukana na matukio kama hayo.
Chanzo - EATV
By Mpekuzi
Post a Comment