Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo (Taliri) kanda kati, Dk Harun Chawala na mkewe Neema Mwasanganga waliofariki dunia usiku wa juzi baada ya gari lao kusombwa maji wakati wakivuka daraja la Shaaban Robert mjini Mpwapwa kuagwa leo.
Akizungumza leo Jumapili Machi 7 2021 Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Dk Archard Rwezaura amesema kuwa miili ya wanandoa hao inaagwa leo nyumbani kwao Taliri wilayani humo.
“Sasa hivi ndio tunakwenda kuaga miili halafu itasafirishwa kwenda nyumbani kwa mwanaume (Dk Chawala) Wilayani Kilolo mkoani Iringa,”amesema.
Amesema mazishi ya wanandoa hao yatafanyika kesho nyumbani kwa Dk Chawala Wilayani Kilolo mkoani Iringa.
Kwa mujibu Kaimu Mkurugenzi mkuu wa taasisi ya utafiti Tanzania Dk Jonas Kizima, Dk Chawala alikuwa anampeleka mkewe kazini katika Hospitali ya Wilaya ya Mpwapwa lakini walipo fika kwenye daraja la Shaban Robert maji yaliwazidi na kusombwa.
Tukio hilo lilitokea juzi saa mbili usiku kwa gari lao aina ya Nissan X-trae yenye usajili namba T483 BRR kusombwa na maji kwenye daraja hilo lililopo mita chache kutoka ilipo ofisi ya mkuu wa wilaya.
CHANZO- MWANANCHI
By Mpekuzi
Post a Comment