Na Jumbe Ismailly IGUNGA
BARAZA la Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Igunga, Mkoani Tabora limepitisha rasimu ya mapendekezo ya mapango na bajeti ya jumla ya shilingi bilioni 46,819,314,038/= kwa mwaka wa fedha wa 2021/2022.
Hayo yalibainishwa na Afisa Mipango wa wilaya ya Igunga,Joel Nsekela alipokuwa akiwasilisha mapendekezo ya bajeti hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo,Pascrates Kweyamba katika mkutano maalumu wa Baraza la madiwani uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya mapendekezo ni kwamba kwa mujibu wa sheria ya fedha ya serikali za mitaa No. 9 ya mwaka 1982 kifungu cha 43 kifungu kidogo (1) cha sheria hiyo inamtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya kuandaa mpango na bajeti kila mwaka na kuwasilisha kwenye vikao vya wadau kwa ajili ya kutoa maoni kurekebisha mapungufu na kurekebisha maboresho stahiki.
Aidha Nsekela alivitaja vyanzo vya mapato vitakavyowezesha kupatikana kwa shilingi bilioni 46,819,314,038/= kuwa ni pamoja na vyanzo vya ndani,ruzuku kutoka serikali kuu,wadau wa maendeleo kutoka vyanzo vya mapato vya ndani na kwamba Halmashauri hiyo inakisia kukusanya shilingi bilioni 3,266,638,000.00/= ambazo ni sawa na ongezeko la asilimia 2.4 ikilinganishwa na makisio ya mwaka wa fedha wa 2020/2021.
Hata hivyo Afisa Mipango huyo alibainisha kuwa ruzuku kutoka serikali kuu kwa ajili ya matumizi ya kawaida na miradi ya maendeleo itakuwa shilingi bilioni 37,801,076,038.00/= ruzuku kutoka kwa wahisani ni shilingi bilioni 5,771,600,000.00/= ambazo ni sawa na ongezeko la asilimia 15.12 ikilinganishwa na makisio ya mwaka wa fedha wa 2020/2021 ambapo pia mpango na bajeti hii unategemewa kuchangiwa na wananchi katika miradi mbalimbali ya maendeleo inayopendekezwa.
Kwa mujibu wa Nkesela mapendekezo ya bajeti ya Halmashauri kwa mwaka wa fedha wa 2021/2022 yatatumika kulipa mishahara shilingi 33,382,067,032.00 sawa na asilimia 71 matumizi mengine 3,607,102,000.00/= sawa na asilimia 8,miradi ya maendeleo 9,830,145,006.00 sawa na asilimia 21 na kwamba jumla kuu itakuwa ni shilingi bilioni 46,819,314,038.00 ambazo ni sawa na asilimia 100.
Afisa Mipango huyo hata hivyo aliyataja mapato ya ndani yatokanayo na vyanzo vya ndani ya Halmashauri kuwa ni CHF shilingi 15,182,000/=,vyanzo vya ndani(Ownsouce Proper) 2,286,909,000.00/=,Bima ya afya 285,805,000.00/=, uchangiaji wa huduma ya afya (Cost sharing 48,300,000.00/=) ada ya wanafunzi kidato cha tano na sita 1,284,660.00/=na kwamba jumla ndogo ya vyanzo vya ndani itakuwa 931,429,000/= na hivyo kufanya mapato ya ndani kuwa 3,266,638.00/=.
Wakichangia mapendekezo ya bajeti hiyo,baadhi ya madiwani wa viti maalumu,Rukia Mwakibinga Kata ya Igunga pamoja na Eva Godfrey wa Kata ya Iborogelo,walisema kuwa bajeti hiyo ni nzuri kwani itasaidia kukamilisha miradi mbali mbali iliyojengwa kwa nguvu za wananchi.
Hata hivyo Mwakibinga alisema wao kama madiwani watahakikisha wanashirikiana na watumishi wa Halmashauri ili fedha hizo ziweze kutumika kama ilivyokusudiwa.
Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Igunga,Nikolaus Ngassa aliwashauri baadhi ya wataalam wa maji kuacha utaratibu wa kutumia fedha nyingi kufanya utafiti kwenye maeneo ambayo wanajua uwezekano wa kupata maji kwa njia ya visima haupo na badala yake fedha hizo wazitumie kuchukua maji ya ziwa Victoria na kuwafikishia wananchi kwenye maeneo yao ambayo yapo karibu.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Igunga,Mkoani Tabora,Lucas Bugota(wa pili kutoka kulia) akiongoza mkutano maalumu wa baraza la Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Igunga. Baadhi ya wajumbe wa Baraza maalumu la Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Igunga,Mkoani Tabora wakipitia hatua kwa hatua mapendekezo ya bajeti ya mwaka wa fedha wa 2021/2022 kabla ya kuipitisha.Mkuu wa wilaya ya Igunga,Mkoani Tabora,John Mwaipopo akiwasilisha salamu za serikali katika mkutano maalumu wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Igunga.(Picha zote Na Jumbe Ismailly) Baadhi ya watendaji wa idara mbali mbali za Halmashauri ya wilaya ya Igunga,Mkoani Tabora wakiwa kwenye mkutano maalumu wa Baraza la madiwani kusikiliza kitakachopitishwa na wajumbe wa mkutano huo.
By Mpekuzi
Post a Comment