Charles James, Michuzi TV
TUNATESEKA! Ndiyo kauli ambayo Wananchi wa Kata ya Nkuhungu jijini Dodoma wameitoa leo kufuatia mvua kubwa zinazonyeesha kuharibua miundombinu ya makazi yao hali iliyopelekea wengine kuishi kwa majirani.
Michuzi Blog imefika katika eneo hilo na kujionea athari ambazo zimesababishwa na mvua hizo ambapo nyumba nyingi zimezungukwa na maji huku nyingine zikiwa na maji ndani jambo linalosababisha wananchi hao washindwe kuishi kwenye nyumba zao.
Akizungumzia hali hiyo mmoja wa wakazi wa eneo hilo, Rose Kiondo amesema kwa muda mrefu wamekua wakiwasilisha malalamiko yao kwa uongozi wa Jiji la Dodoma lakini hakuna hatua zozote za kuwasaidia ambazo zimechukuliwa na serikali.
" Kama ambavyo mnajionea hali ni mbaya kwa kweli, mvua ndio kwanza kila siku zinanyeesha na maji yanazidi kutuama hapa, nyumba zetu zimebomolewa na maji zingine maji yamejaa ndani tunaishi kwa kutanga tanga tu hatuna pa kwenda.
Hapa sisi tuna watoto wetu ambao wanasoma, asubuhi wanapata tabu sana kwenda mashuleni na hata jioni wakati wa kurudi majumbani wanapata changamoto kubwa, tunaomba serikali isikie kilio chetu na itusaidie," Amesema Rose Kiondo.
Kwa upande wake mkazi mwingine, Leonard Swai ameiomba serikali kuangalia namna ambayo inaweza kutengeneza njia ya kuchepusha maji ili yawe yanatembea na kuacha kutuhama sehemu moja.
" Hapa naamini jitihada zikifanyika za kutengeneza mtaro mkubwa haya maji yatatembea na hii changamoto itaisha, ni suala la kuamua tu kwani tunateseka ilihali serikali ipo na inaweza kutusaidia," Amesema Swai.
Wanafunzi na wananchi wakipita katikati ya maji yaliyotuama katika eneo la Nkuhungu jijini Dodoma ambalo limeathiriwa na mvua zinazonyeesha.
Hii ni miongoni mwa uharibifu uliofanywa na mvua zinazonyeesha katika eneo la Nkuhungu jijini Dodoma. Mmoja wa Wananchi wa Kata ya Nkuhungu, Rose Kiondo ambaye nyumba yake imeharibiwa na mvua zinazonyeesha mfulululizo jijini Dodoma Akizungumza na wandishi wa habari kuelezea adha wanayoipata.
By Mpekuzi
Post a Comment