MKUTANO WA SITA WA TUME YA PAMOJA KATI YA TANZANIA NA BURUNDI KUFANYIKA MKOANI KIGOMA |Shamteeblog.
Tanzania na Burundi zimejipanga kuutumia Mkutano wa Sita wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kama njia mojawapo ya kuhamasisha wananchi wa pande zote mbili kuchangamkia fursa mbalimbali za uchumi zinazopatikana katika nchi hizi ili kunufaika nazo.
Kauli hiyo imetolewa kwa pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali, Wilbert Ibuge na mwenzake kutoka Burundi, Mhe. Isidore Ntirampeba walipokutana na Waandishi wa Habari leo mjini Kigoma kwa ajili ya kuwajulisha kuhusu mkutano huo utakaofanyika mjini humo kuanzia tarehe 3 hadi 5 Machi 2021.
Balozi Ibuge alieleza kuwa, Tanzania na Burundi zimeendelea kuwa na ushirikiano wa kihistoria na kindugu kwa muda mrefu huku kila nchi ikinufaika kwa kiasi kikubwa na ushirikiano huo. Hata hivyo alieleza kuwa, bado upo umuhimu mkubwa wa kuendelea kuwahamasisha wananchi wa Tanzania na Burundi kuchangamkia fursa mbalimbali zinazopatikana kwenye nchi hizo ili ziwanufaishe kiuchumi. Fursa hizo ni pamoja na biashara na uwekezaji.
“Mikutano ya Tume za Pamoja za Kudumu pamoja na mambo mengine inaangalia namna ya kuhakikisha kila mwananchi kutoka nchi husika ananufaika na fursa zilizopo na jukumu letu ni kuendelea kuwahamasisha kuzichangamkia fursa hizo” alisema Balozi Ibuge.
Akizungumzia ukuaji wa sekta ya uchumi kati ya Tanzania na Burundi, Balozi Ibuge alisema pamoja na changamoto mbalimbali, biashara kati ya Tanzania na Burundi imeendelea kukua mwaka hadi mwaka na kutoa mfano wa kipindi cha kuanzia mwaka 2015 hadi 2019 ambapo Tanzania na Burundi zilifanya biashara zenye thamani ya shilingi Bilioni 619.9 ukiwa ni wastani wa Shilingi Bilioni 123.9 kwa mwaka. Katika kiasi hicho, Tanzania iliuza nchini Burundi bidhaa zenye thamani ya shilingi bilioni 604.9 na Burundi iliuza Tanzania bidhaa zenye thamani ya Shilingi Bilioni 7.4.
Aidha, akizungumzia huduma ya wakimbizi, Balozi Ibuge alieleza kuwa, Tanzania imeendelea kuhifadhi wakimbizi kutoka Burundi huku Serikali ya Burundi ikiendelea kuwahimiza wakimbizi hao kurejea nchini kwao kwa hiari kutokana na kuimarika kwa hali ya amani na utulivu nchini humo.
“Tanzania imeendelea kuhifadhi wakimbizi kutoka Burundi, hata hivyo kutokana na kuimarika kwa hali ya amani na usalama nchini kwao Serikali yao imeendelea kuwahimiza kurejea ili kwenda kushiriki katika shughuli za ujenzi wa Taifa lao. Itakumbukwa kuwa, zoezi la kuwawezesha wakimbizi hao kurejea kwa hiari Burundi limeendelea kuratibiwa na Kamati ya Utatu inayojumuisha Tanzania, Burundi na Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) ambapo kati ya mwezi Septemba 2017 na Februari 2021, jumla ya wakimbizi 113,488 wamerejea nchini Burundi kwa hiari” alifafanua Balozi Ibuge.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje kutoka Burundi, Mhe. Isidore Ntirampeba alisema tume ya pamoja ya ushirikiano ni nyenzo muhimu katika kuimarisha ushirikiano baina ya nchi na nchi kwani hutoa nafasi kwa nchi mbili kutathmini mafanikio yaliyofikiwa kupitia ushirikiano uliopo, kutafuta suluhu kwa changamoto mbalimbali na kuainisha hatua imara zaidi za kufikia malengo kusudiwa. Alieleza kuwa, mikutano hii ni fursa nzuri kwa pande zote mbili kujipanga na kuboresha utendaji kulingana na mabadiliko mbalimbali yanayotokea duniani na katika nchi yakiwemo yale ya kisera na kimazingira.
Kadhalika, alitumia fursa hiyo kuishukuru na kuipongeza Tanzania na kuitaja kama nchi ya kupigiwa mfano katika kuhudumia wakimbizi wakiwemo wale wa kutoka Burundi ambao wamekuwa wakipokelewa tangu mwaka 1972. Aliongeza kuwa, Burundi inajivunia mchango wa Tanzania kwenye ustawi wa nchi hiyo na kwamba nchi hiyo inavutiwa na uongozi imara wa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao unalenga kuwaletea wananchi wote maendeleo.
Mkutano wa Sita wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kati ya Tanzania na Burundi ambao unafanyika miaka 15 baada ya Mkutano wa Tano uliofanyika jijini Dar es Salaam mwaka 2006 unalenga kuendeleza, kuimarisha na kudumisha uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Burundi. Mkutano huu ambao utaanza kwa ngazi ya wataalam kutoka Tanzania na Burundi tarehe 3 Machi 2021utahitimishwa na Mkutano wa Mawaziri kutoka nchi hizo tarehe 5 Machi 2021.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) kuhusu Mkutano wa Sita wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kati ya Tanzania na Burundi utakaofanyika mkoani Kigoma kuanzia tarehe 3 hadi 5 Machi 2021. Kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Burundi, Mhe. Isidore Ntirampeba.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Burundi, Mhe. Ntirampeba akiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara wa Tanzania, Prof. Riziki Shemdoe (katikati) pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji wa Tanzania, Mhandisi Nadhifa Kemikimba wakiwa kwenye Mkutano kati ya Balozi Ibuge na Waandishi wa Habari kuhusu Mkutano wa Sita wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kati ya Tanzania na Burundi utakaofanyika mkoani Kigoma kuanzia tarehe 3 hadi 5 Machi 2021.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma, Mhe. Rashid Mchata (kushoto) na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Jim Yonazi wakiwa kwenye Mkutano kati ya Balozi Ibuge na Waandishi wa Habari kuhusu Mkutano wa Sita wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kati ya Tanzania na Burundi utakaofanyika mkoani Kigoma kuanzia tarehe 3 hadi 5 Machi 2021.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Burundi, Mhe. Isidore Ntirampeba naye akizungumza wakati wa mkutano na Waandishi wa Habari kuhusu Mkutano wa Sita wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kati ya Tanzania na Burundi utakaofanyika mkoani Kigoma kuanzia tarehe 3 hadi 5 Machi 2021.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma, Mhe. Rashid Mchata naye akizungumza wakati wa mkutano na Waandishi wa Habari kuhusu Mkutano wa Sita wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kati ya Tanzania na Burundi utakaofanyika mkoani Kigoma kuanzia tarehe 3 hadi 5 Machi 2021
Balozi wa Tanzania nchini Burundi, Mhe. Dkt. Jily Maleko akifuatilia Mkutano kati ya Balozi Ibuge na Waandishi wa Habari kuhusu Mkutano wa Sita wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kati ya Tanzania na Burundi utakaofanyika mkoani Kigoma kuanzia tarehe 3 hadi 5 Machi 2021
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Frank Mwega akifuatia Mkutano kati ya Balozi Ibuge na Waandishi wa Habari kuhusu Mkutano wa Sita wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kati ya Tanzania na Burundi utakaofanyika mkoani Kigoma kuanzia tarehe 3 hadi 5 Machi 2021
Sehemu ya wadau kutoka sekta mbalimbali za Tanzania na Burundi walioshiriki mkutano kati ya Baloiz Ibuge na Waandishi wa Habari kuhusu Mkutano wa Sita wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kati ya Tanzania na Burundi utakaofanyika mkoani Kigoma kuanzia tarehe 3 hadi 5 Machi 2021
Sehemuu nyingine ya wadau
Sehemu ya wadau wakifuatilia mkutano
Wadau wa Mkutano wa Sita wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kati ya Tanzania na Burundi
Mkutano ukiendelea
By Mpekuzi
Post a Comment