Na Muhidin Amri,Tunduru
MRATIBU wa kitengo cha kifua kikuu na ukoma kutoka Hospitali ya wilaya Tunduru mkoani Ruvuma Dkt Mkasange Kihongole, ameonya tabia ya baadhi ya wananchi kutumia dawa bila kupata ushauri wa Daktari kwani matumizi holela ya dawa inaweza kushusha kinga ya mwili na hivyo kuwa rahisi kupata magonjwa mbalimbali ikiwemo kifua kikuu.
Dkt Kihongole amesema hayo jana katika kijiji cha Namwinyu kata ya Namwinyu,wakati akizungumza katika kampeni ya uelimishaji na uchunguzi wa vimelea kwa ugonjwa huo kwa watoto walio chini ya umri wa miaka 19.
Aidha,amewahimiza mama wajawazito kuwa na mazoea ya kwenda kupima afya zao mara kwa mara ili kufahamu maendeleo ya mtoto aliye tumboni na kujifungulia katika vituo vya kutolea huduma ili kuepuka uwezekano wa kupata magonjwa na kuzuia vifo vifo visivyo vya lazima wakati na baada ya kujifungua.
Alisema, kujifungulia kwenye vituo vya kutolea huduma inasaidia sana mama mjamzito kupata msaada wa kitaalam wakati wote wa ujauzito na wakati wa kujifungua na mtoto anayezaliwa kwa kuchomwa sindano ya BCG ambayo ni muhimu kwa afya ya mtoto dhidi ya magonjwa mbalimbali.
Alisema,watoto ni kundi mojawapo lililopo kwenye hatari kubwa ya kupata kifua kikuu na pia kundi lililosahaulika kutokana na mfumo wa maisha hasa kwa familia maskini ambapo ni rahisi kwa mzazi kumuacha mtoto bila kuchunguza afya na kutompa chakula kwa muda mrefu.
Dkt Kihongole alisema, katika mwaka 2020 jumla ya watoto 169 wenye umri kuanzia miaka 0-4 walipata kifua kikuu, miaka 5-9 watoto waliopata maambukizi walikuwa 33 na wale wenye umri kati ya miaka 10 hadi 14 walikuwa 18 watoto hao wote walianzishiwa dawa.
Alitaja dalili za ugonjwa wa kifua kikuu kwa watoto ni kukosa raha,kulia lia,kupungua au kutoongezeka uzito, makuzi duni kwa hiyo mzazi akimuona mtoto wenye dalili hizo ni vyema kuwahi katika vituo vya kutolea huduma kwa ajili ya ushauri na kupata matibabu.
Kampeni ya kutokomeza ugonjwa wa kifua kikuu inafanyika vijiji mbalimbali ambapo wataalam wa kitengo cha kifua kikuu Hospitali ya wilaya wanakwenda kila kijiji cha ajili ya kutoa elimu ya uelimishaji,uibuaji na kuwaanzishia dawa wanaobainika kuwa na ugonjwa huo.
Fatuma Mikila mkazi wa kijiji hicho ameishukuru Hospitali ya wilaya Tunduru kupitia wataalam hao kwenda kutoa elimu juu ya ugonjwa huo, kwani itawasaidia sana kuokoa maisha ya watoto pamoja na watu wazima na wao wenyewe.
Hata hivyo,ameiomba Serikali kupitia wizara ya Afya kuwa na utaratibu wa kwenda mara kwa mara kwa wananchi kutoa elimu ya kujikinga na ugonjwa huo pamoja na magonjwa mengine ambayo yamekuwa yakiathiri sana afya na maisha ya wananchi walio wengi.
Kwa upande wake,muuguzi wa zahanati ya Namwinyu Hidaya Kandulu alisema, tatizo la kifua kikuu kwa watoto katika kijiji hicho sio kubwa sana ikilinganisha na magonjwa mengine kama malaria ambayo inachangiwa na wazazi kutowapa chandarua watoto wao wakati wa kulala.
Amewataka wazazi, kuhakikisha wanawalaza watoto wao kwenye vyandarua ili kuzuia mbu ambao ndiyo chanzo cha kukithiri kwa ugonjwa wa malaria kwa watoto wengi katika kijiji hicho.
Ameiomba serikali kuangalia upya utaratibu wa sasa kutoa chandarua kwa mama wajawazito wanaokwenda kliniki wenye hudhurio la kwanza na kwa mtoto mwenye umri wa miezi tisa wanaopata chanjo ya surua ndiyo wanaopata chandarua, ambapo ameshauri chandarua zitolewa kwa watoto wote walio chini ya umri wa miaka mitano.
Alisema, baadhi ya wazazi wana watoto zaidi ya mmoja wanaohudhuria kliniki na hawana uwezo wa kuwapatia chandarua, kwa hiyo ameiomba serikali iwasaidie watoto hao kuwapatia chandarua ili kuwakinga wasipate malaria ugonjwa unaotajwa miongoni mwa magonjwa yanayoongoza kupoteza maisha ya watu wengi hapa nchini.
Mratibu wa kitengo cha kifua kikuu na ukoma wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma Dkt Mkasange Kihongole kushoto akifuatilia maendeleo ya Afya ya mtoto Fatma Ali(3) ambaye anasumbuliwa na homa za mara kwa mara wakati wa kampeni ya uelimishaji na uchunguzi wa vimelea vya kifua kikuu kwa watoto iliyofanyika katika kijiji cha Namwinyu wilayani humo,kulia ni mama wa mtoto Daima Kazembe.
Muuguzi wa Zahanati ya Namwinyu kijiji cha Namwinyu wilaya ya Tunduru Hidaya Kandulu akiongea na baadhi ya akina mama waliofika kwenye zahanati hiyo kwa ajili ya huduma ya kliniki kwa watoto wao, hata hivyo baadhi ya watoto hao wamebainika kuwa na maradhi mbalimbali ikiwemo ugonjwa wa kifua kikuu unaosababisha watoto wengi kutokuwa na maendeleo mazuri katika suala zima la ukuaji.
By Mpekuzi
Post a Comment