Na Jusline Marco-Arusha
Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mjini,Kenan Laban Kihongosi amewaomba wadau wa elimu kushirikiana na serikali kuhakikisha wanatoa mchango wao ili kuwezesha kuwepo kwa mazingira bora ya kujifunzia wanafunzi ambayo yatatoa elimu nzuri zaidi.
Akiweka mawe ya msingi katika majengo ya shule tatu(3) za sekondari zilizopo ndani ya jiji la Arusha,Kihongosi amesema kuwa serikali inawekeza fedha nyingi kwenye ujenzi wa madarasa na kuboresha ofisi za walimu.
"Tukio la uwekaji wa mawe ya msingi umefanyika kwenye shule ambazo zimejengwa na serikali kwa kushirikiana na wananchi kwa kutoa nguvu kazi zao katika kufanikisha ujenzi wa miundombinu hiyo kukamilika kwa asilimia kubwa."alisema Kihongosi
"Nasisi kama viongozi tunawajibu wa kushirikiana na wananchi kuhakikisha maendeleo ya kweli yanaletwa na wananchi wenyewe kwa kushirikiana na serikali yao ambayo ipo madarakani"alisisitiza Kihongosi
Ameongeza kuwa takribani madarasa 16 yameweza kujengwa katika kipindi cha mwezi wa 12 mwaka jana pamoja na majengo ya utawala katika shule mbalimbali ambayo yameshakamilika na yanatumika hivyo kupelekea kutumika kwa zaidi ya shilingi Milioni 900 kwenye ujenzi wa miundombinu hiyo ya shule ikiwa ni mapato ya ndani ya halmashauri ya jiji la Arusha.
Afisa Elimu Sekondari jiji la Arusha Mwl.Valentine Makuka katika ziara hiyo amesema kuwa majengo hayo yamejengwa kwa lengo la kukidhi mahitaji katika shule hizo ambapo amesema katika bajeti ya mwaka jana hadi mwezi juni mwaka huu ilikusudia kujenga ofisi za walimu 5 na madara 16 hai ili kuweza kukidhi mahitaji ya wanafunzi wanaoingia muhula mpya.
"Jengo la utawala ambalo limejengwa katika shule ya sekondari Moivaro litapelekea kuachwa wazi kwa vyimba viwili vya madarasa ambavyo vilikuwa vikitumiwa na walimu kama ofisi,shule ya sekondari Mkonoo vyumba viwili vya madarasa vimebaki wazi baada ya jengo la utawala kukamilika na katika shule ya sekondari Kinana vyumba viwili vya madarasa pia vimeacha wazi baada ya kikamilika kwa ujenzi wa jengo la utawala katika shule hiyo."Alisema Makuka
Aliongeza kuwa katika jiji la Arusha kwa mwaka huu kutakuwa na vyumba vya madarasa 23 badala ya vyumba 16 ambavyo ndivyo vilikuwa mahitaji halisi ambapo katika majengo ya utawala yaliyojengwa yataokoa vyumba 11 vya madarasa ambavyo awali vilikuwa vikitumika kama ofisi za walimu.
Katika hatua nyingine Mwl.Makuka amesema kuwa katika jiji la Arusha walikuwa wamefaulisha takribani wanafunzi elfu kumi na moja na mia saba kati ya hao wanafunzi elfu tisa na mia nane tayari wameripoti katika shule walizopangiwa ambapo wanafunzi waliobaki wamejiunga na shule za binafsi.
"Kupitia maafisa elimu kata tumefanya sensa na wametuletea kila mwanafunzi yupo wapi na katika jiji la Arusha kila mwaka huwa tunakuwa na wanafunzi asilimia 15 mpaka 20 huwa hawaripoti katika shule zetu kwasababu moja ya wale wanafunzi wanaosoma kwenye shule za mchepuo wa kingereza huwa hawaji kwenye shule zetu."alisema Makuka
Naye diwani wa kata ya Moivaro,Bwn.Philemon Meijo Mollel alisema pamoja na ujenzi wa vyumva vya madarasa na majengo la utawala bado kuna changamoto ya upatikanaji wa maji ambapo ameiomba serikali kutengenezea gata za kuweka maji kwenye tenki kwaajili ya kuvuna maji ya mvua ambayo yatakuwa yanatumika katika shule hiyo ya Moivaro wakati ambao wakisubiri mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira(AUWSA) kuwafikishia huduma ya maji.
"Kama kutakuwa na gata za maji hapa maju ya mvua yatakuwa yanaingia kwenye tenki ambayo yatakuwa yanatumika hapa shuleni hivyo yatasaidia watoto hawa kutokwenda kuchota maji kwenye makorongo,"Alisema Diwani Meijo.
Mmoja wa wanafunzi katika shule ya Sekondari Moivaro Jackline Laizer aliishukuru serikali kwa kuboresha miundombinu ya shule yao kwani awali walikuwa wanasoma kwa kubanana ambapo tatizo lililobaki kwa sasa ni changamoto ya maji ambayo inawafanya kwenda kuchota maji kwenye makorongo hali inayopelekea kuchelewa kuingia darasani.
Mkuu wa Wilaya ya Arusha mjini Ndg.Kenani Kihongosi akizindua jiwe la msingi katika jengo la utawala kwenye shule ya sekondari Moivaro,pembeni ni Diwani wa Kata ya Moivaro Philemon Meijo Mollel akishirikiana na Mkuu wa wilaya ya Arusha.
Afisa elimu sekondari halmashauri ya jiji la Arusha,Mwalimu Valentine Makuka akizungumza katika ziara ya uwekaji wa mawe ya msingi kwenye ujenzi wa vyumba vya madarasa na majengo ya utawala katika shule za sekondari za Moivaro,Mkonoo na Kinana zilizopo ndani ya halmashuri ya jiji la Arusha.
Jengo la ghorofa la vyumba 6 vya madarasa katika shule ya sekondari ya Moivaro ambalo lipo katika hatua za mwisho kukamilika.
By Mpekuzi
Post a Comment