MBUNGE DITOPILE ATOA MAHITAJI KWA WAFUNGWA GEREZA LA KONDOA, AAHIDI KUMALIZIA UJENZI WA ZAHANATI |Shamteeblog.

Charles James, Michuzi TV

MBUNGE wa Viti Maalum Wanawake Mkoa wa Dodoma, Mariam Ditopile akiambatana na Jumuiya ya Waislamu (DMC) wa Mkoa wa Dodoma wametembelea Gereza la Wilaya ya Kondoa na kupeleka mahitaji mbalimbali ikiwemo Futari kwa wafungwa na mahabusu wa gereza hilo.

Akizungumza baada ya kukabidhi mahitaji hayo, Mbunge Mariam Ditopile ameahidi kushirikiana na uongozi wa Gereza hilo katika kukamilisha ujenzi wa Zahanati inayojengwa ambayo pia itakua msaada kwa wananchi wa maeneo jirani.

Amesema pia amepokea changamoto kutoka kwa Mkuu wa Gereza hilo, Julius Nachunga kumuomba awasaidie kupata mashine ya kupasulia mawe kwani wanao mradi wa kupasua mawe ambao kama wakipata mashine wataufanya kwa ufanisi zaidi na utawaingizia kipato kikubwa ambacho kitawasaidia kama Gereza katika kujiendesha.

" Mimi kama Mbunge wa Mkoa wa Dodoma na mwanachama wa DMC leo tumefika kuwasilimu wafungwa na mahabusu hawa, pamoja na kuwafariji pia tumewaletea mahitaji mbalimbali ikiwemo Futari kama tunavyofahamu huu ni Mwezi Mtukufu wa Ramadhan, Nguo za aina zote kama Kanzu kwa ajili ya kuswalia, Taulo za Kike kwa ajili ya Wafungwa Wanawake, tunafanya hivi kwa upendo tukitambua hawa ni ndugu zetu na wanahitaji faraja,

Kama Gereza wana miradi yao ikiwemo wa kupasua mawe, lakini hawana vifaa kama Mashine ile ya kupasulia na badala yake wanatumia mikono, nimemuahidi pia Mkuu wa Gereza kushirikiana nao tuweze kupata mashine hiyo ili waitumie pia katika kuwaingizia kipato kitakachowasaidia katika mahitaji yao mbalimbali

Mkuu wa Gereza ametueleza changamoto zao wana ujenzi wa Zahanati yao ambayo pia itahudumia wananchi wa Kondoa, nimemuahidi kuwa nimelibeba hilo na nitashirikiana nao kuhakikisha Zahanati hii inamalizika ili iwe msaada kwa wafungwa na wananchi wetu wa Kondoa," Amesema Mariam Ditopile.

Mbunge Ditopile pia ameahidi kuongea na uongozi wa Mkoa wa Dodoma ili Gereza hilo liweze kupatiwa Shamba kwa ajili ya kufanya kilimo na kulima mazao ambayo siyo tu yatawapatia chakula chao wenyewe lakini pia yatawaingizia kipato kwa kufanya biashara ya mazao.

Kwa upande wake Mkuu wa Gereza hilo, SP Julius Nachunga amemshukuru Mbunge Mariam na Taasisi hiyo kwa kuwatembelea na kueletea mahitaji hayo huku akimuomba kutochoka kuwatembelea na kusaidia kutatua changamoto zao.

" Nikushukuru sana Mbunge Ditopile kwa kufika hapa wewe na wenzako, huu ni moyo wa kipekee ulioonesha, nikuombe usituchoke sisi tuna mahitaji mengi tumekueleza tunaomba utusaidie kama ulivyoahidi na mengine tutayawasilisha ofisini kwako, " Amesema SP Nachunga.





 



By Mpekuzi

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post