Na Said Mwishehe, Michuzi TV
HALMASHAURI ya Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani kwa sasa ipo kwenye mchakato wa kuhakikisha Stendi mpya ya mabasi wilayani humo inaanza kufanya kazi kwa ukamilifu na tayari wameweka mikakati ya kuhakikisha mabasi yote safari zake zinaanzia kwenye stendi hiyo.
Hatua hiyo ya halmashauri inakuja baada ya wananchi wa Wilaya ya Kisarawe kutoa ombi la kwamba stendi hiyo inatakiwa kutumika kikamilifu kutoa huduma ikiwa pamoja na mabasi yote yanayotoka vijiji kuja mjini na yanayotoka Mjini kwenda Kisarawe yanaanzia hapo tofauti na ilivyo sasa.
Kwa mujibu wa wananchi waliozungumza na waandishi wa habari wamesema tangu stendi hiyo kuanza kazi mwaka mmoja uliopita, kuna changamoto ya mabasi kutoingia stendi na hasa mabasi yanayotoka vijijini jambo ambalo limesababisha kukwamisha shughuli za ukuaji wa uchumi , hivyo wameitaka Halmashauri ya Kisarawe kuhakikisha inasimama imara katika kuweka utaratibu wa mabasi yote kufika hapo kwa ajili ya kufanya safari zake.
Wananchi hao wamesema wanaimani kubwa na viongozi wa Halmashauri ya Kisarawe, hivyo wakiamua stendi hiyo ifanye kazi inawezekana na wanaamini kwamba stendi hiyo ikisimamiwa vizuri mbali ya kukua kwa uchumi wa eneo hilo utakwenda kuchangamsha Wilaya hiyo ambayo ni kati ya Wilaya kongwe nchini Tanzania.
Akizungumza kuhusu maombi ya wananchi kutaka stendi hiyo ifanye kazi kwa asilimia 100, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe Mussa Gama amesema wanafahamu takwa au hitaji la kubwa la wananchi hao ni kuwa na stendi ya mabasi itakayokuwa inafanya kazi yaq kusafirisha abiria kutoka vijiji kuja wilayani na kutoka wilayani kwenda mikoa ya jirani ukiwemo wa Dar es Salaam.
"Katika kuhakikisha hilo linafanikiwa halmashauri kupitia mapato yake ya ndani ilianza ujenzi wa stendi mpya ambayo imewekwa miundimbinu yote ya msingi kwa maana kuna vibanda vya kusubiria abiria , vyoo na taa za usiku ili shughuli za stendi zifanyike mchana na usiku .
"Katika hilo tulishirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo wa vyombo vya usafiri, na jambo hilo lilikuwa lifanyike Aprili mwaka 2020 lakini kutokana na janga la Corona baadhi ya shughuli zilisimamishwa , lakini kituo hiki kimekuwa ni kiu kubwa ya wana Kisarawe,"amesema.
Amesema wamekuwa wakiandika barua mara kwa ili kulimaliza suala hilo na maamuzi yaliyofikiwa ni kuendelea na utaratibu wa awali, hivyo wanakwenda kufanya Kisarawe kulikuwa na stendi ndogo ndogo nyingi, hivyo wanakwenda kuzifuta ikiwemo stendi ya Noah.
"Zinatakiwa kuanzia safari zake katika stendi mpya ya Kisarawe, kwa hiyo Noah zitakuwa zinaanzia safari zake hapo na kwenda maeneo mengine ya vijiji vya kisarawe, lakini kutakuwa na mabasi kwa maana ya daladala zitakazokuwa zinakwenda Dar es Salaam lakini mpango mkubwa ni kuhakikisha
magari yote yanaanzia safari zake kwenye kituo cha mabasi Kisarawe kwenda Vijijini na kwenda Dar.
"Mchakato wa kuhakikisha stendi hiyo inatoa huduma zitaanza Aprili mwaka huu hadi ifikapo Desemba mwaka huu kitakuwa kinatoa huduma kwa asilimia 100, na sasa kua mipango endelevu ya kuendeleza miundombinu na kuna fedha ambazo zinafanyiwa kazi na michoro imekamilika na kazi iliyobakia ni kuingia makubaliano na mkanadarasi kumalizia miundombinu mchache.
"Hivyo Tutahakikisha stendi hii inafanya kazi kama matakwa ya wananchi wanavyotaka na, Serikali zetu za mitaa ziliundwa ili kuhakikisha madaraka yanakwenda kwa umma kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 145 na ibara ya 146 , hivyo na sisi tutawajibika ipasavyo kuhakikisha matakwa ya msingi ya wananchi ambayo yenye tija wanakwenda kuyatekeleza,"amesema Gama.
Muonekano wa vibanda vya abiria wanavyokaa wakati wa kusubiri mabasi kwa ajili ya kufanya safari ndani na nje ya Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani.Jinsi kituo cha mabasi cha wilaya ya Kisarawe kinavyoonekana kwa sasa ambapo Halmashauri ya wilaya hiyo kupitia Mkurugenzi wake Mussa Gama ameeleza mikakati iliyopo kuhakikisha kituo hicho kinafanya kazi kwa asilimia 100 pamoja na kuendelea na ujenzi wa miundombinu iliyobakia.
Muonekano wa nje wa choo cha abiria kilichopo katika Stendi ya mabasi ya Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani.
Tanki la kuhifadhia maji ambalo lipo katika Stendi mpya ya mabasi wilayani Kisarawe.
By Mpekuzi
Post a Comment