INAELEZWA kuwa Kocha Mkuu wa Simba, Didier Gomes Da Rosa ameueleza uongozi wa timu hiyo kuachana na kiungo mshambuliaji Ibrahim Ajibu na beki wa kushoto, Gadiel Michael kutokana na kutofurahishwa na uchezaji wao.
Simba kwa sasa ipo katika mkakati mzito wa kuboresha kikosi chake kwa kuwaongezea mikataba baadhi ya wachezaji wao na mpaka sasa tayari wameshamalizana na Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, John Bocco na Shomari Kapombe.
Ajibu na Gadiel walijiunga na Simba kwa mkataba wa miaka miwili kila mmoja wakitokea Yanga huku Ajibu akiwa nahodha wa timu hiyo aliyekuwa na rekodi ya kufunga mabao saba na kutoa pasi za mwisho 17 msimu wa 2017/18.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo Championi Jumamosi limezipata kutoka ndani ya Simba zinasema kuwa, tayari Gomes ameshatoa maelekezo yake kwa uongozi wa timu hiyo juu ya wachezaji hao kutokana kutoridhishwa na haina ya uchezaji wao, hivyo ametaka waachwe katika usajili ujao.“Unajua bado timu inafanya maboresho kwa kuongeza mikataba ya wachezaji ambao tayari inaelekea kuisha mwishoni mwa msimu huu kutokana na maelekezo ya mwalimu anavyoona wachezaji anaofanya nao kazi katika mashindano yote.“
Ukiangalia Shomari, Bocco na Tshabalala licha ya viwango ubora kuonekana hadharani lakini bado mwalimu alipitisha majina yao, Ajibu na Gadiel mambo yamekuwa tofauti kwa sababu hafurahishwi na uchezaji wao hivyo ametoa maelekezo ya kuwa waachwe msimu ukiisha,” alisema mtoa taarifa.
MWANDISHI WETU, Dar es Salaam
from Author
Post a Comment