MRADI wa elimu ya unawaji mikono na usafi wa mazingira kwa ujumla inayotolewa na Taasisi ya Enviromental Conservation Community of Tanzania (ECCT) inatarajia kuwafikia wanafunzi zaidi ya 5,817 katika Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani.
Akizungumza leo Mei 21 ,2021 wakati wa uzinduzi wa mradi huo , Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Jokate Mwegelo ameipongeza taasisi hiyo kwa kuamua kuupeleka mradi huo ndani ya wilaya hiyo kwani utakwenda kusaidia kutoa elimu ambayo itabadilisha mtazamo wa jamii.
"Mradi huu wa unazungumzia umuhimu wa unawaji mikono na usafi wa mazingira kwa ujumla nimeuzindua rasmi ndani ya Wilaya yetu ya Kisarawe.Mradi huu utaanza katika shule 12 , wanafunzi 5817 watanufaika na elimu hiyo itawafikia pia walimu na wafanyakazi wa shule hizo,"amesema Jokate.
Amefafanua zaidi utoaji elimu na ugawaji vifaa shuleni unalenga kujikinga na maambukizi ya magonjwa ya mlipuko kama Virusi vya Corona, kipindupindu , homa ya tumbo.
"Mradi huu utaanza rasmi leo (Mei 21)baada ya kuuzindua rasmi na utakamilia Febrauri mwaka 2022, lengo la mradi huu ni kupunguza magonjwa ya mlipuko kwa kuelimisha jamii ya wanafunzi na wananchi kwa ujumla kuhusu umuhimu wa kunawa mikono na usafi kwa ujumla,"amesema.
Amezitaja shule ambazo zitaanza kupata elimu hiyo pamoja na vifa vya kunawia mikono ndani ya Wilaya ya Kisarawe ni Sekondari za Mwanalumango,Chanzige, Kibuta, Masaki, na shule za Msingi chanzige A na B , Kibasila, Masaki, Chang'ombe A na B , Madubike na Kibuta.
"Kupitia mradi huu wanafunzi 5,817 na jamii ya wafanyakazi wa shule tajwa watanufaika moja kwa moja.Afya, ustaaraba na ustawi wa Taifa letu kwa ujumla vinategemea sana hali ya usafi wa mazingira inayotuzunguka.
"Changamoto nyingi za kiafya zinatokana na magonjwa ya mlipuko kama homa za kipindupindu, upumuaji na homa za matumbo ambazo zinaongezeka siku hadi siku, athari zake ni kubwa kwani ripoti ya benki ya dunia mwaka 2013 inasema kuna gharama kubwa za kiafya zitokanazo na kutokuwepo kwa maji safi na usafi kwa ujumla ambazo zinakadiriwa kuwa dola za Marekani milioni saba hadi dola milioni 10.
"Hivyo basi utoaji wa elimu na vifaa vya kunawa mikono shuleni una manufaa , sio tu kiafya bali itapunguza gharama kubwa ambazo Serikali na wadau wengine wanatoa kwa ajili ya kutibu magonjwa kwani fedha hizo zingeweza kuelekezwa kwenye miradi mingine.
"Mikono safi ni uhai wetu , mikono safi ni afya yetu, mikono safi ni uchumi wetu, hivyo kila mmoja wetu ajitafakari namna anavyoweza kuwa na mchango chanya katika jamii yetu hasa wanafunzi wetu kuwahamasisha kunawa mikono kwa sabuni mara kwa mara ili kujikinga na magonjwa,"amesema Jokate.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya Enviromental Conservation Community of Tanzania (ECCT) Lucky Michael amesema kwa kushirikiana na Serikali ya JAPAN kupitia JICA , wamezindua mradi huo wa kutoa elimu na kugawa vifaa vya 24 kwa shule 12 wilayani humo.
"Tunashukuru kwa ushirikiano ambao tumeupata kutoka kwa viongozi na tunaamini tutaifikia jamii kubwa sana.Kupitia mradi huu wanafunzi ambao watapata elimu tunaamini elimu itakwenda ndani na nje ya wilaya ya Kisarawe,"amesema.
Amesema elimu hiyo ambayo itatolewa kwa wanafunzi na walimu, itakwenda kubalisha tabia na jamii ya watu wa Kisarawe kwa kuwa na mtazamo chanya katika kutunza mazingira na afya zao.
Alipoulizwa kwanini wamechagua Kisarawe, amesema miradi mingi ya aina hiyo na nyingine imekuwa ikitolewa zaidi Dar es Salaam , hivyo wanakila sababu ya kuchagua Kisarawe kwani ni sehemu ambayo inauhitaji zaidi.
"Baada ya Kisarawe tutakwenda katika wilaya nyingine za Mkoa wa Pwani, hata hivyo tumeanza na shule 12 na kisha tutakwenda katika shule 30 za Kisarawe na tutukapomaliza tutakwenda maeneo maeneo mengine ya Pwani,"amesema.
By Mpekuzi
Post a Comment