Na Said Mwishehe, Michuzi TV
UKUMBI mkubwa wa kisasa wa kupumzikia wageni wa Twiga Business Lounge uliopo katika Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere Terminal III jijini Dar es Salaam umezinduliwa rasmi leo ukiwa na hadhi ya kimataifa.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati akizindua ukumbi huo, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Dk.Leonard Chamriho amesema Serikali imeamua kutoa kumbi hizo za abira kwa ajili ya kupumzikia pamoja na kuongezea tija na ufanisi katika usafiri wa anga , pia ATCL watazitumia vizuri kutangaza shirika hilo.
Hivyo ametoa rai kwa ATCL kuendelea kuboresha na kukidhi viwango vya kimataifa."Tunasema hivi kwasababu Uwanja wetu huu wa Kimataifa wa Julius Nyerere unaotumiwa na kampuni nyingi za ndege kwa sasa, hivyo ni fursa yenu kutangaza biashara na kampuni hizo."
Ametumia nafasi hiyo kueleza Serikali itaendelea kuboresha majengo mengine ya abiria ikiwemo kumbi za kupumzikia ambapo ATCL wanategemewa kutoa huduma.
Ameongeza pamoja na kuwapa kumbi hizo Serikali itaendelea kufanya uchambuzi wa maeneo mengine kuona kama wakipewa wanaweza kuongeza tija na kushindana vema katika biashara hiyo.
"Nawapongeza ATCL kwa kuanza safari za China licha changamoto zilizopo kutokana na masharti mengi yanayotokana na udhibiti wa janga la Corona , ambayo mengi tunaendelea kuyafanyia kazi kwa ukaribu,"amesema .
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Miundombinu ya Bunge Selemani Kakoso pamoja na jitihada ambazo Seerikali imefanya yapo mambo ambayo yanahitajika kufanyiwa kazi , la kwanza ni kubeba sehemu ya madeni chechefu yanayoikabili ATCL.
"Madeni haya yatalifanya shirika hili lisiweze kufanya kazi iliyofikiriwa, naamini Serikali ikibeba yale madeni tutalifanya shirika letu liweze kusimama,"amesema Kakoso.
Awali akizungumza wakati wa uzinduzi huo Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Ndege ATCL Mhandisi Ladslaus Matindi amesema mbali ya kuongeza mapato lakini na ubora wa huduma zao ni kiwango cha hali ya juu na kwamba ukumbi huo unaweza kuhudumia watu 200 kwa wakati mmoja na unahudumia mtu yoyote aliyetamani kutumia huduma zao kwa gharama nafuu kabisa.
"Uwapo ndani unaweza kupata chakula , vitafunwa pamoja na vinywaji vya mbalimbali.Lakini ukumbi wetu utakuwa na sehemu ya watoto kwa ajili ya michezo,pia tutakuwa na sehemu ambayo wafanyabiashara wanaweza kufanya kazi zao wakati akisubiri huduma zetu,"amesema.
By Mpekuzi
Post a Comment