Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ameipongeza Sekretarieti ya Kamati ya Pamoja ya Kushughulikia Masuala ya Muungano kwa kufanikisha utatuzi wa hoja za Muungano.
Mhe. Hemed ametoa pongezi hizo leo Mei 20, 2021 alipokutana na kufanya mazungumzo na Sekretarieti hiyo ofisini kwake Vuga, Zanzibar.
Alisema pamoja na mafanikio hayo ipo haja sasa ya kuzimaliza kabisa hoja za Muungano zilizosalia ili kuendelea kujenga imani kwa wananchi kwa Serikali zao katika kutatua hoja hizo.
“Ninafarijika sana na hoja kuona namna Sekretarieti hii mnavyofanya kazi na ninaamini hoja nane zilizosalia itafika pahala zitafika mwisho, kuna mambo yanayogusa wananchi katika nyanja mbalimbali tuyaangalie na tuone namna ya kuyamaliza,” alisema.
Aidha, Makamu wa Pili alisema ushirikiano baina ya Ofisi yake pamoja na Ofisi ya Makamu wa Rais ni kutokana na maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa watendaji wakuu chini ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muunano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango.
Alimshukuru na kumpongeza Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa kwa ushirikiano wake kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) ambao umekuwa kiungo kikubwa katika kufanikisha utatuzi wa hoja za Muungano.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Mary Ngelela Maganga alimuahidi Makamu wa Pili wa Rais kuwa Sekretarieti hiyo inaendelea na vikao vyake kujadili na kuzipatia ufumbuzi hoja za Muungano.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akizungumza na wajumbe wa Sekretarieti ya Kamati ya Pamoja ya Kushughulikia Masuala ya Muungano (hawapo pichani) ofisini kwake Vuga, Zanzibar.
Wajumbe wa Sekretarieti ya Kamati ya Pamoja ya Kushughulikia Masuala ya Muungano kutoka Sakretarieti ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) wakiwa katika kikao na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla walipomtembela ofisini kwake Vuga, Zanzibar.
Wajumbe wa Sekretarieti ya Kamati ya Pamoja ya Kushughulikia Masuala ya Muungano kutoka Sekretarieti ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) wakiwa katika kikao na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla walipomtembela ofisini kwake Vuga, Zanzibar.(PICHA NA OFISI YA MAKAMU WA RAIS).
By Mpekuzi
Post a Comment