MIAKA 16 YA MAAJABU YA LIVERPOOL MBELE YA AC MILAN JIJINI ISTANBUL |Shamteeblog.


Charles James, Michuzi TV

UNAWEZA kutaja fainali zote bora za Michuano ya Ulaya, unaweza kutaja mechi bora za Ulaya, lakini fainali ya Liverpool vs AC Milan mwaka 2005 inabaki kuwa ya mfano wake.

Ni Jumatano bora ya muda wote kwetu sisi Liverpudlian wala haikua Jumatano ya Majivu, bali ilikua Jumatano yenye historia ya kukumbukwa kwa sisi mashabiki wa Soka.

Ilikua ni Jumatano ya Tarehe 25/05/2005. Liverpool tuliposhinda ubingwa wetu wa Tano mbele ya wababe wa Italia, AC milan.

Ubingwa wetu haukutarajiwa, tulikua na msimu mbovu kwenye Ligi Kuu. Tukimaliza nje ya nafasi nne za juu.

Maana yake tulihitaji kushinda ubingwa wa UEFA ili kupata nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa kwa msimu uliofuata.

Tungesema nini mbele ya Milan ile ya Carlo Ancellot? Milan yenye huduma ya Kilokole kutoka kwa Ricardo Kaka, Milan yenye Wafashisti Andre Pirlo, Gennaro Gattuso, Nesta na Paolo Maldini?

Kila jina la Milan lilikua kubwa na bora. Liverpool ilikua na Steven Gerrard tu. Ungemlinganishaje Milan Baros na Myahudi Andriy Shevshenko wa Milan? Wapi Harry Kewel angeweza kumsogelea Clarence Seedorf?

Wala tusingejaribu kusema beki yetu yenye Jamie Carragher, Sammy Hyppia na Traore eti ilikua bora mbele ya Maldin, Nesta, Stam na Cafu. Hatukugusa hata theluthi ya ubora wao.

Kocha Ancellot tayari alikua na taji la Ulaya mwaka 2003 akimfumua Juventus pale Trafford. Rafa Benitez ndio kwanza alikua akijaribu bahati yake kwa mara ya kwanza.

Hatukua na ubavu mbele ya Milan. Hatukua na ubora wa kuwazidi. Hatukua na kikosi imara zaidi yao. Ila tuliwazidi kwa u-Liverpool wetu. Sijui kama unanielewa😅😅

Tusogee hapa: Kipindi cha kwanza kinamalizika kwa Liverpool kuwa nyuma kwa Magoli 3-0. Goli la Nahodha Maldin na Magoli mawili ya Hernan Crespo yalishaipa uongozi Milan.

Liverpool tukaufyata mkia. Ngoma ikawa nzito, kumbuka hapo kipindi cha kwanza tushalazimishwa kufanya 'sub' baada ya Harry Kewell kuumia na kuingia Vladimir Smicer.

Tunafika vyumbani madaktari wanathibitisha kwamba beki wa kulia Steve Finnan hatoweza kuendelea na mchezo kwa sababu ya majeraha.

Tunafanya sub ingine nje ya mipango anaingia Didi Hamman ambaye anaenda kucheza na Xabi Alonso kwenye eneo la kiungo.

Tatu bila kipindi cha kwanza ,Milan wanaonekana kuwa wamoto sana, Na hapo bado Ricardo Kaka, Seedorf na Shevshenko hawana Magoli, hali ilikua mbaya kwetu. Bado walihitaji kutufunga zaidi. Njaa ilikua ipo tumboni mwao.

Jukwaani kwenye uwanja wa Atatürk jijini Istanbul, Uturuki mashabiki wa Liverpool walikua wanalia na mikono yao ikiwa kwenye tama. Milan walikua wanakula Piza na Chocolate. Walishaamini game imeisha.

Mmoja wa Wasaidizi wa kocha Rafa Benitez, Mzee Sammy Lee anasema baada ya zile goli tatu za kipindi cha kwanza, ni mwanadamu mmoja tu ambaye aliamini Liverpool itashinda usiku ule.

Nae ni Rafael Maudes Benitez. Wao walishakata tamaa.

Wakiwa vyumbani, Kocha Benitez anawaambia wachezaji tafuteni goli moja likipatikana mjue kila kitu kitabadilika na kuwa upande wetu.

TURUDI KIPINDI CHA PILI

Wakati wanatoka vyumbani, Sammy Lee anamuita Gerrard (Nahodha) anamwambia tengeneza kizimba uzungumze na watu wako. Waeleze kuhusu hii Jumatano.

" Niliwaambia, tazameni umati wa watu hawai usiku huu, wote wameacha shughuli zao kuja kutusapoti sisi, hamjui baada ya leo maisha yenu yatabadilika kwa kiasi gani mbele ya watu wetu.

Sisi ni Liverpool na Liverpool mahali kwake ni fainali ya Ulaya, huu ni usiku wetu, ni nafasi yetu tumepigana kufika hapa tusiiache ikaondoka zake, twendeni tukawaonesha kuwa sisi ni Liverpoo," Maneno ya Captain Fantastic, Steve G.

Bado Milan walianza game kwa kasi lakini kuingia kwa Didi kulimpa nafasi Gerrard kucheza huru na kuhaha kila kona.

Ungemkuta kulia akimpiga 'tackling' Seedorf, angeraruana na Gattuso katikati, dakika mbili mbele angekua mbele kugombea krosi ya Riise na Jap Staam.

" Hello Hello, Here we go, Steven Gerrard puts a grain of doubts to the back of Milan minds and gives hope to all of many thousands Liverpool Fans"

Hii ni sauti ya mtangazaji akisumilia goli la kwanza la Steven Gerrard dakika ya 53 ya kipindi cha pili. Sasa Uwanja ukalipuka, Atatürk ikageuka Anfield. Gerrard akawafuata mashabiki kuwaambia nyanyukeni.

Dakika mbili mbele kushoto mwa Uwanja, Riise anaigusa pasi kwa Alonso ambaye anausogeza mpira kwa Didi. Didi anatoa pasi kwa Smicer ambaye anapiga shuti 'dhaifu' linalomshinda golikipa wa Milan, Nelson Dida.

Hofu inawakumba Milan, presha inakua upande wao. Sasa ni 3-2 na Liverpool wanazidi kusogea bila hofu. Mtangazaji anaongeza hii " Miracle are Possible here, Unbelievable "

Punde baada ya Milan kuanzisha mpira Gerrard anamnyang'anya mpira Gattuso. Zinapigwa Pasi za haraka sana, kelele za mashabiki wa Liverpool zinayazidi masikio ya Milan. Ngoma imegeuka.

Oke. Nusu ya Milan, Carragher anapiga pasi kwa Milan Baros. Hapo wachezaji wa Liverpool wako wanne dhidi ya nane wa Milan. Spidi ya kuwafuta Milan ni kubwa.

Baros anamuekea Gerrard pasi ya kisigino kwenye 18 yards ya Milan. Gattuso na mahasira yake anamkwatua Gerrard na mwamuzi Manuel Mejuto Gonzalez anapuliza filimbi kuashiria penati.

Xabi Alonso anautenga mpira kwa ajili ya kupiga, shuti lake linaokolewa na Dida lakini mpira unatua miguuni mwake anafunga goli la tatu. Ubao unabadilika matokeo yanasoma 3-3.

DAKIKA ZA FURAHA NA MATESO

Asikuambie mtu hakuna muda tuliishi kwa mateso kama dakika zile baada ya kuchomoa goli tatu. Nguvu tuliyotumia ndani ya dk 15 za kipindi cha pili ilikuwa ni kubwa yenye faida.

Matokeo yanasoma 3-3. Milan wanafufuka kuja kwa hasira. Shevshenko kila saa anashinda golini mwetu.

Ukimuangalia Djimi Traore, Carragher na Hyppia kule nyuma wanaonekana kutepeta. Didi na Alonso wanapambana sana katikati lakini ubora wa Milan kwenye kiungo uliwapa homa.

Gerrard alikua anahaha kila kona, beji yake ya unahodha kuna muda ilikua haionekani kwa namna alivyochafukwa. Roho ilishabadilika.

Benitez hakuchoka kusimama kwenye 'touchline', mkono wa kushoto mfukoni, mkono wa kulia ukitoa maelekezo. Sasa tulikua tayari kufia uwanjani.

Dakika 90 za kawaida zinamalizika kwa Magoli 3-3, dakika 30 za nyongeza zilikua chungu zaidi ya sindano za Chloroquine. Homa ilipanda, presha ilitutesa.

Sitosahau ile tackling ya Jamie Carragher na save ya Jerzy Dudek ya shuti la Shevshenko. Kwenye mahojiano fulani Gerrard anasema mkojo ulikaribia kumtoka wakati Dudek anasave shuti la Shevishenko. Alidhani ilishakua goli.

Wachezaji wetu wanne, Carra, Didi, Lui Garcia na John Arne Riise walipata majeraha 'dead leg' lakini iliwabidi wamalize dakika. Hatukua na namna.

Ni nyakati zile ambazo nililiona jasho la Gerrard liking'aa kama Dhahabu..miguu ya wachezaji wetu ikateseka bila kusikia maumivu.

Historia ikaandikwa baada ya kushinda kwa mikwaju
ya penati. Sura ya Rafa Benitez ikaongezeka kwenye bango kubwa la wazee wenye heshima Anfield.

Bill Shankly, Bob Paisley, Joe Fagan, Kenny Dalglish, Benitez na sasa kuna Klopp.

Jumatano ikageuka siku ya heshima kwetu. Ubingwa wa Tano, Siku ya Jumatano, Mwezi wa Tano, Tarehe 25 mwaka 2005. Na wala haikua Jumatano ya majivu bali Jumatano ya 'Merseyside'. Na leo ni miaka 16 imepita.




0683 015145


By Mpekuzi

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post