MKOA WA SONGWE WAOMBA MAHAKIMU NA MAJENGO YA KUDUMU YA MAHAKAMA |Shamteeblog.

Na Mwandishi Maalum-Songwe

Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Profesa Sifuni Mchome amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa wa Songwe Dkt Seif Shakilaghe kuandaa andiko linaloainisha changamoto mbalimbali zinazoathiri kwa namna moja ama nyigine  utoaji hakijinai katika Mkoa wa Songwe na  mapendekezo ya namna ya kuzikabili changamoto hizo  ili ziwezekupatiwa ufumbuzi .

 Ametoa agizo hilo jana (jumatatu) baada ya kutoa fursa kwa Mahakimu wa  Wilaya za Ileje, Momba na Mbozi pamoja  watendaji wengine wanaohusika na suala ya utoaji haki  katika Mkoa wa Songwe akiwako Wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya  Taifa ya Mashtaka, TAKUKURU, Ustawi wa Jamii na Wasaidizi wa Kisheria kuelezea mafanikio na changamoto zinazowakabili katika utekelezaji wa  kila siku wa utoaji hakijinai kwa wananchi.

Baadhi ya changamoto   hizo  zilizowasilishwa mbele ya  Makatibu Wakuu Watatu   kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Ofisi ya Rais Menejienti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na  Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia ,Wazee na Watoto ni pamoja na upungufu mkubwa wa idadi ya Mahakimu, wakiwamo Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo,  ukosefu wa Majengo ya  Mahakama na Magereza, ucheleweshwaji wa  upepelezi wa kesi na  uhaba wa watumishi wa kada nyingine wakimo makatibu sheria, maafisa ustawi wa jamii, walinzi na wahudumu.

Akiwasilisha  changamoto zinazoikabili Mahakama ya Wilaya ya  Momba,  Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Wilaya hiyo  Mhe.Timothy Lyon amesema, pamoja na Mahakama yake  kuendelea vema na jukumu la kutoa hakijinai  lakini  inakabiliwa na tatizo kubwa la kutokuwa na  Jengo la Mahakama.

 “Waheshimiwa  Makatibu  Wakuu, suala la  utoaji wa haki katika Wilaya ya Momba linakwenda vizuri, hata hivyo tunakabiliwa na changamoto ya kutokuwa na Jengo la Kudumu la Mahakama. Kwa  mfano, Jengo  ambako shughuli za mahakama zinaendelea katika Mahakama ya  Wilaya ya Momba  ni la kupanga na lipo eneo moja na  Nyumba ya Kulala Wageni (Lodge)”

 Akabinisha zaidi kwa  kusema.“Lakini cha zaidi, lango la kuingia Jengo la Mahakama na kuingia kwenye Nyumba ya Wageni ni Moja, hali hii si salama sana kwasababu  watu wa aina mbalimbali wanaingia  kwa kutumia  lango hilo kana kwamba wanakwenda Mahakamani kumbe wanakwenda katika nyumba ya wageni. Muingiliano huu  si salama na unaathiri  shughuli za Mahakama na  suala utoaji haki” akasema  Hakimu Mkazi Mfawidhi Timothy Lyon.

Mhe. Timothy Lyon amewaeleza  Makatibu  hao kwamba,  Wilaya ya Momba pia haina Gereza lake  bali inategemea Gereza la Mkoa ambalo lipo mbali na athari zake ni kwa wakati mwingine mahabusu  kuchelewa kufika mahakamani na hivyo  kesi kuchelewa kuanza kwa wakati

 Kuhusu  ucheleweshaji wa kesi, Hakimu Mkazi  Mfawidhi Timothy Lyon amesema, malalamiko  ni mengi kutoka kwa mahabusu  hasa wale wenye kesi za mauaji na kesi za uhujumu  uchumi na malalamiko hayo  yanahusu kuchelewa kwa upelelezi na hivyo kuziomba mamlaka husika kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa kwa nini upepelezi unachelewa  ikiwamo pia ucheleweshaji wa vibali vya  dhamana.

Kwa upande wake, Hakimu  Mkazi  wa Wilaya ya Ileje, Mhe.Shughuli Mwampashe, yeye pia alielezea changamoto ya ukosefu wa Jengo la Mahakama ambapo kwa sasa shughuli za  utoaji hakijinai zinafanyika katika  Jengo la Chama  cha Mapinduzi  jambo alilosema wakati mwingine huzua tafrani pale inapokuwapo kesi ya pande mbili kinzani.

 Vile vile ameelezea changamoto ya uhaba mkubwa wa watumishi katika  Mahakama za Mwanzo ambazo zipo  Tano katika  wilaya hiyo ya Ileje lakini kuna Mahakimu wawili tu na wote wapo katika kituo  kimoja.

“tunazo mahakama za mwanzo tano na mahakimu wawili,  hawa wanapotakiwa kwenda nje ya kituo usafiri wanaoutumia ni wa pikipiki na maeneo wanayokwenda  ni ya mvua kipindi chote, lakini kama hiyo haitoshi anakuwa Hakimu yeye, Karani yeye na Mhudumu yeye, hii inaadhiri sana utendaji wa majukumu yetu hivyo tunaomba tuongezewa mahakimu na watumishi wa kada nyingine” akasema  Hakimu Mkazi Shughuli Mwampashe.

Kwa upande wa Mahakama ya Wilaya ya Mbozi, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Wilaya hiyo, Mhe. Nemes Chami , yeye pia alielezea  kutokuwapo wa Jengo la Mahakama na kukosekana kwa Gereza na kwamba wanatumia jengo la mahakama ya mwanzo kuendesha shughuli za utoaji wa haki jinai.

“Kama walivyosema  Mahakimu wenzangu, hatuna jengo la mahakama, hatuna Gereza, mahabusu inabidi waletwe Mbozi ambako ni mbali lakini kutokna na umbali huo hata mashahidi wanashindwa kufika mahakamani kutoka na gharama kubwa ambazo wanatakiwa kuzitumia na athari zake ni ucheleshwaji wa utoaji wa haki na kuadhiri shughuli za mahakama na mlundikano wa mahabusu. Ombi langu ni kama la wenzangu tuongezewe watumishi na kupatiwa majengo ya kudumu kwaajili ya shughuli za  mahakama” akasisitia Mhe. Chami.

Uhaba wa  watumishi  ni suala pia ambalo aliongelea Wakili wa Serikali anayesimamia Ofisi ya  Taifa ya Mashtaka ya Mkoa wa Songwe ambaye alisema kwa sasa Ofisi hiyo ina Mawakili wa Serikali wawili  tu ambao wanatakiwa kushughulikia majalada ya kesi za mauaji 120 na kesi za kawaida 254 jambo ambalo amesema ndilo kwa kiasi kikubwa linachelewesha uendeshaji wa kesi hizo.

“Ni kweli kunauchelewaji wa kesi lakini hili linatokana na uhaba wa mawakili wa Serikali hivi sasa tupo wawili tu na mwanzoni nilikuwa peke yangu, sisi wawili tusome na kupitia majalada yote ili tuweze kutoa ushauri wa kupeleke mbele  mashauri, hii si kazi nyepesi, ili kupunguza mzigo huu tumeanzisha  utaratibu wakuwatumia wenzetu wa Jeshi la Polisi  wale wenye uwezo wa kuendesha kesi watusaidie, lakini tunaomba tupatiwe mawakili wa serikali wengi zaidi ili   utoaji wa haki uweze kutekelezwa kwa haki na kwa wakati”

Makatibu Wakuu hao, Dkt. Laurean Ndumbalo kutoka   Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. John Jingu kutoka  Wizara ya  Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto na Prof. Sifuni Mchome Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria  wapo katika ziara ya  takribani wiki moja ya kuitembelea  Mikoa  mipya na ile ya pembezoni na kwa kuanzia wameanza na Mkoa wa Songwe.

Akielezea  madhumuni ya ziara hiyo ya makatibu wakuu  hao na ambao shughuli zao zinaingiliana kwa namna moja ama nyingine ,Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Profesa Sifuni Mchome amesema ziara hiyo ya mikoa ya mipya na ya pembezoni  inalenga katika  kujifunza  na kubadilishana  mawazo  kuhusu mafanikio  na changamto zinazowakabili  wadau  na  Taasisi zinazohusika  na masuala ya utoaji wa haki,   changamoto wanazokabiliana nazo watumishi, na changamoto zinazowakabili  maafisa wa ustawi wa jamii katika utekelezaji wa majukumu yao hususani yale yanayohusu masuala ya unyanyasaji wa kijinsia kwa watoto, wanawake na wazee na kuona namba  bora na ya  kudumu ya kuzitatua changamoto hizo

Baadhi ya hoja  katika siku ya kwanza ya ziara hizo zikiwamo za  uhaba mkubwa wa watumishi zilizotolewa  maelekezo ikiwamo ya  wahusika  akiwamo Wakili wa Serikali wa Ofisi ya  Taifa ya Mashtaka kuwasilisha mapendekezo  ya watumishi  wanaoweza kuhamishwa kutoka Halmashauri zingine na kupelekwa Songwe ili liweze kufanyiwa kazi. 

Awali Mkuu wa Mkoa wa Songwe Mhe. Omari Mgumba aliwashukuru Makatibu Wakuu hao kwa kuuchagua Mkoa wa Songwe kuwa mmoja ya  Mikoa ambayo wameamua kuitembelea na  kuangalia  na kutambua changamoto wanazokabilia nazo likiwamo la uhaba mkubwa wawatumishi pamoja na changamoto wanazokabiliwa nazo watumishi pamoja na suala la utoaji wa haki.

Katibu Mkuu Wizara ya Katibu na Sheria, Profesa Sifuni Mchome, akielezea madhumuni ya ziara ya  pamoja   ya Makatibu Wakuu watatu kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala  Bora katika Mkoa wa Songwe  wakati wa Kikao na Wadau wa Sekta ya Utoaji wa hakijinai katika mkoa huo. Makatibu hao  watatu Profesa  Sifuni Mchome, Dkt Laurean Ndumbalo na Dkt. John Njigu  wapo katika ziara ya kikazi ya kawaida   katika mikoa  mipya na ya pembezoni  kwa madhumuni ya kujifunza, kubadilishana mawazo na kutafuta njia  za kutatua changamoto zinazoikabilia  mikoa hiyo.

Makatibu Wakuu wakijitambulisha kwa Mkuu wa Mkoa wa Songwe Mhe. Omar Mgumba walipomtembelea Ofisi  kwake  ambako Mkuu wa Mkoa huyo aliwashukuru Makatibu Wakuu hao kwa kuuchagua  Mkoa wa Songwe kuwa miongoni ya  Mikoa wanayoitembelea  kujifunza na hatimaye kuzitafutia ufumbuzi changamoto mbalimbali zinazoikabili  Mkoa wake.

  Katibu Mkuu wa  Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt Laurean Ndumbalo, akijibu na kufafanua hoja mbalimbali zilizowasilishwa na Watumishi katika  Mkoa wa Songwe.  Wengine pichani ni Profesa Sifuni Mchome, Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Dkt. John Jingu.

Sehemu Kubwa ya Watumishi wa Kada mbalimbali katika Mkoa wa Songwe waliojitokeza kuwasikiliza Makatibu Wakuu  pamoja na kuwasilisha  kero zao zikiwamo  za sintofahamu  ya kupandishwa  madaraja,  kutolipwa stahiki zao kwa muda mrefu, na uhaba mkubwa wa watumishi katika   Idara na vitengo na hivyo kupunguza kasi ya kuwahudumia wananchi inavyostahili.
Wakili  Wa Serikali anayesimamia Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ya Mkoa wa Songwe akielezea uchache wa Mawakili wa Serikali katika ofisi yake jambo linaloathiri na kuchangia ucheleweshaji wa  upelelezi wa kesi zikiwamo na  mauaji na uhujumu uchumi, naye akaomba kupatiwa  Mawakili zaidi wa Serikali.
Afisa  kutoka TAKUKURU  Emmanuel Ndembeka akizungumza kuhusu ukosefu wa nyezo za  kufanyika kazi kwa Mawakili ( Instrument) kunavyochangia ukwamishwaji wa utoaji wa hakijinai kwa mawakili wengi kukosa  nyenzo hizo.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya  Mbozi Mhe. Nemes Chami naye akiwasilisha changamoto za Mahakama  ya Wilaya ya Mbozi katika utoaji wa Hakijinai, ambapo pamoja na mambo mengine aliomba kuongezwa kwa idadi ya Mahakimu  na watumishi wa kada nyingine.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Wilaya ya Momba, Mhe Timothy  Lyon akielezea changamozo zinazoikabili  Mahakama ya Wilaya hiyo, ikiwamo  ukosefu wa Jengo la Mahakama,  uhaba wa watumishi, ukosefu wa  Gereza na ucheleweshaji wa upelelezi wa kesi. pembeni yake ni Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Ileje, Mhe Shughuli Mwampashe.



By Mpekuzi

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post