WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania, Mamlaka ya Bandari Tanzania na Mamlaka ya Serikali Mtandao kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuboresha utendaji wa Bandari ya Dar es Salaam
Ameyasema hayo jana(Jumatano, Mei 12, 2021) alipotembelea bandari ya Dar es Salaam ili kuona utendaji wa bandari hiyo.
“TPA endeleeni kuiimarisha bandari yetu, hii ni sura ya uchumi wa nchi yetu, zungumzeni lugha moja ya uwajibikaji, TRA muwepo maeneo yote yanayohitaji uwepo wenu na muda wote wateja wetu wahudumiwe ili bandari yetu iendelee kuwa bora. Nchi nyingi zinatutegemea”
Amesema kuwa Mamlaka ya Mapato Tanzania ihakikishe mfumo wa pamoja wa forodha Tanzania (TANCIS) unafanya kazi kwa ufanisi ili kupuinguza malalamiko ya wateja kuhusu mfumo huo.
“Dosari zote za mfumo wa TANCIS zifanyiwe kazi, mfumo usituharibie, mnapoona kuna madhaifu fanyeni marekebisho ya haraka, tunataka wateja waingie na kutoka kwa muda mfupi” Amesema.
Aidha, Waziri Mkuu amemuagiza Kamishna Mkuu wa TRA apeleke watumishi katika mizani ya TANROADS iliyopo Kurasini Dar es Salam ili kurahisisha ukaguzi wa ‘seal’ pale ambapo magari yamezidisha uzito na yanahitaji kukaguliwa
“TRA kuna foleni kwenye mizani, hakuna watu, kuanzia leo peleka watumishi pale tunataka ukaguzi uwe muda wote”.
Akitolea ufafanuzi kuhusu video iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii ya uwepo wa foleni bandarini hapo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania Eric Hamissi amesema suala hilo halina ukweli na hakuna dereva anayekaa bandarini kwa siku tatu.
“Hata sisi tulishangaa sana kuona ile clip, haina ukweli wowote, dereva Omari Mambo Mei 10, 2021 aliingia saa nane mchana, na ilipofika saa 10.38 alishusha mzigo na kuondoka saa 11.00 jioni”
Aliongeza kuwa kwa sasa asilimia arobaini ya eneo la bandari lipo kwenye ujenzi ikihusisha ujenzi wa njia nne za barabara na ujenzi wa gati namba moja mpaka saba lengo ni kuifanya bandari iweze kuhudumia wateja kwa ufanisi mkubwa “mpaka sasa gati namba moja mpaka tano zimekamilika na gati namba sita na saba zitakamilika mwezi Agosti,2021”
Wakizungumza kwa nyakati tofauti madereva wa malori wanaoingia na kutoka kwenye Bandari ya Dar es Salaam wamesema wanaridhishwa na utendaji kazi wa bandari kwani hawatumii muda mrefu kuingia na kutoka bandarini hapo.
(Mwisho)
IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU,
from Author
Post a Comment