WANACHAMA SIMBA JAMII WAADHIMIA KUIJENGA TAASISI HIYO KWA PAMOJA |Shamteeblog.





Wanachama wa Taasisi ya Simba  Jamii Tanzania (SJTE) wakifuatilia kwa umakini agenda za Mkutano Mkuu wa Taasisi hiyo.

Na Zainab Nyamka, Michuzi Tv

TAASISI ya Simba Jamii Tanzania (SJTE) imesema haitaangalia changamoto zilizojitokeza katika uongozi uliopita zaidi wanataka kuendelea kuijenga taasisi hiyo ili iweze kuendelea kusaidia jamii katika nyanja mbalimbali.

Hayo yameazimiwa katika mkutano wake Mkuu wa Kwanza toka kuingia madarakani kwa uongozi mpya na ku baada ya uchaguzi uliofanyika Januari 31 mwaka huu.

Akizungumza na wanachama wa Simba Jamii, Mwenyekiti Mwanakatwe amesema ndani ya muda mfupi toka kuingia madarakani wamewezesha masuala mbalimbali kufanyika ikiwemo usajili wa taasisi hiyo ambayo kwa sasa inatambulika rasmi kiserikali.

Mwanakatwe amesema,SJTE ilianzishwa kwa lengo la kusaidia jamii katika masuala mbalimbali wakiangalia hususani upande wa watu wasiojiweza (walemavu) na watoto wanaoishi katika mazingira magumu.

"Simba jamii ni taasisi iliyoundwa na wanachama wa Simba lengo letu likiwa ni kusaidia jamii ila hatuangalii tunatoa msaada kwa mtu gani hata akiwa shabiki wa timu nyingine ikiwemo Yanga, Azam hata Prisons,"amesema Mwanakatwe.

Amesema, kulikua na changamoto mbalimbali katika uongozi uliopita ila kwa pamoja katika mkutano mkuu wameazimia kuziweka kando na kuendelea kufanya mambo ya kimaendeleo ikiwemo kuwa na ofisi rasmi na kuanzisha vitega uchumi vitakavyoongeza mapato kwenye mfuko wa tasisi.

Hata hivyo, Mwanakatwe amesema menejimeti yake kwa pamoja wameweza kufuatilia akaunti ya benki iliyokuwa imefungiwa na kupelekea usumbufu kwa wanachama kushindwa kulipa ada zao za kila mwezi.

"Katika uongozi wetu tumeweza kufuatilia akaunti ya benki iliyokuwa imefungiwa na kwa sasa tunaenda kufuatilia taarifa ya benki (bank statement) ili kuanza kuruhusu wanachama kulipia ada zao kupitia njia ya kibenki tofauti na sasa ambapo mnalipa kwa njia ya simu,"amesema

Naye Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya SJTE Nuru Mbegu amesema ndani ya taasisi hiyo wameweza kufanya mambo mbalimbali ikiwemo kuandaa safari za wanachama kwenda mkoani wakati timu ya Simba inacheza, kutoa msaada kwa kituo cha watoto Yatima cha UMRA kilichopo  Magomeni.

Kwa sasa SJTE ina jumla ya wanachama 157 wakiwa ndani na nje ya nchi ikiwemo Marekani,Japan na Afrika Kusini na wamewaomba wanachama wa Simba kujitokeza kujiunga na taasisi hiyo kwa maendeleo zaidi.

Mkutano huo Mkuu uliambatana pia na uchaguzi mdogo wa kujaza nafasi zilizokuwa wazi na uliweza kudhaminiwa na kampuni ya ulinzi ya K4S ambao wamevutiwa na madhumuni ya taasisi hiyo ukiachilia masuala ya mpira ya kuwa mashabiki na kuamua kujikita zaidi katika kusaidia jamii zaidi.



By Mpekuzi

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post